Jumatatu 22 Desemba 2025 - 10:23
Haki na Uadilifu ni Dhamana ya Amani, wajibikaji na Usalama Katika Jamii

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Baqir al-Husseini, katika hotuba yake, alisisitiza kwamba kuzingatia misingi ya haki na uadilifu si tu kunadhamini uhifadhi wa amani na usalama katika jamii, bali pia kunakuza uwajibikaji wa kimaadili na kijamii wa wanadamu, na kuandaa mazingira ya ukuaji wa kibinadamu pamoja na kuheshimiwa haki za watu wote.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Baqir al-Husseini, Rais wa Jumuiya ya Imamiyya ya Baltistan, Pakistan, katika hotuba yake aliyotoa kwenye Msikiti Mkuu wa Baltistan, alisisitiza umuhimu wa kuishi maisha kwa kuzingatia misingi ya haki na uadilifu. Aliongeza kuwa; kuzingatia haki na uadilifu, sambamba na kushikamana na majukumu ya kimaadili na kijamii, kupata riziki halali, na kujishughulisha na matendo mema na ya haki, si tu ni misingi ya mtu binafsi na ya kijamii, bali pia ni chachu ya kuleta amani, usalama na uwazi katika jamii.

Mwanachuoni huyu wa Pakistan, akiendelea na hotuba yake, alirejelea umuhimu wa haki na uadilifu katika ngazi ya kimataifa, na akasisitiza kwamba; serikali na taasisi za kimataifa zinapaswa kufanya maamuzi na kutekeleza hatua zao zote kwa kuzingatia misingi hii, ili mpangilio wa kijamii udumishwe na mazingira ya ukuaji na maendeleo ya kibinadamu yaandaliwe. Alionya kwamba dhulma na kutotenda haki huvuruga mizani ya kijamii, na huwanyima watu uwezo wa kutekeleza majukumu yao binafsi na ya kijamii.

Umuhimu wa kuheshimu uhuru wa dini na haki za binadamu

Akiendelea na hotuba yake, na akirejelea masuala ya kimataifa, hususan heshima ya uhuru wa dini na haki za binadamu, alisema: kila mtu, na kila mfuasi wa dini au madhehebu yoyote, anapaswa kuwa na haki ya kuendesha maisha yake kwa mujibu wa itikadi na imani yake. Aidha, alizitaka taasisi za kimataifa, hususan Umoja wa Mataifa, kuchukua hatua madhubuti za kulinda haki za mataifa yote, na kuzuia kukanyagwa haki ya mwanadamu yeyote yule.

Ushauri wa kimaadili na kiroho

Mwishoni, Hujjatul-Islam Sayyid Baqir al-Husseini, aliishauri jamii kujipamba na taqwa, daima wakumbuke mauti na Siku ya Kiyama katika maisha yao, na wajitahidi kurekebisha tabia na matendo yao, pamoja na kutekeleza ipasavyo majukumu yao ya kijamii.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha