Jumapili 21 Desemba 2025 - 16:00
Umoja wa Kiislamu Utumie Nyenzo za Kisheria Katika Kupambana Dhidi ya Utawala wa Kizayuni

Hawzah/ Dkt. Hilya Dutaqi, mhadhiri wa sheria ya kimataifa, katika semina ya nne ya kimataifa iliyokuwa na anuani isemayo “Iran ya Kiislamu; Ngome ya Heshima ya Kiislamu katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni”, alisisitiza kwamba mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni si ya kijeshi pekee, bali ni vita ya hatima juu ya uhalali, sheria na simulizi ya kisheria ndani ya mfumo wa kimataifa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Dkt. Hilya Dutaqi, mhadhiri wa chuo kikuu na mwenye shahada ya uzamivu katika sheria ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Carleton nchini Kanada, katika semina ya nne ya kimataifa “Iran ya Kiislamu; Ngome ya Heshima ya Kiislamu katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni” iliyoandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Qadimun, alisisitiza umuhimu wa mhimili wa  muqawama kuingia kwa mpangilio katika uwanja wa sheria ya kimataifa, akasema: Kukabiliana kwa Ngome ya Heshima ya Kiislamu na utawala wa Kizayuni si mapambano ya kijeshi tu, bali ni vita ya kina juu ya maana, uhalali, sheria na simulizi ya kisheria katika mfumo wa kimataifa.

Akitaja kuundwa kwa mfumo wa sheria ya kimataifa baada ya Vita vya Pili vya Dunia, alisema: Mfumo huu ulijengwa kwa madai ya kuzuia maafa kama Holocaust na kulinda utu wa binadamu, lakini Palestina tangu mwanzo imekuwa kielelezo kikuu cha ubaguzi katika mfumo huo. Mfumo unaojitambulisha kuwa wa kimataifa na ulio juu ya siasa, kwa vitendo umefanya kazi ndani ya mahusiano ya nguvu na kuchangia kuendelezwa kwa mfumo wa utawala wa kiimla na kidhalimu.

Mhadhiri huyu wa sheria ya kimataifa, akieleza kuwa Mafuriko ya Al-Aqsa yaling’oa kizuizi cha uhalali wa kisheria wa Magharibi, aliongeza: Damu ya mashahidi wa Palestina imeonesha kwamba tatizo si ukosefu wa sheria; kwa kuwa leo, kwa mtazamo wa kisheria, mauaji ya kimbari huko Ghaza yametambuliwa, Mahakama ya Kimataifa ya Haki imethibitisha uwezekano wa mauaji ya kimbari, amri ya kusitisha operesheni Rafah imetolewa, na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai pia imetoa hati za kukamatwa dhidi ya maafisa wakuu wa utawala wa Kizayuni. Hata hivyo, tatizo kuu ni utekelezwaji wa sheria na udhibiti wa simulizi ya kisheria ndani ya muktadha wa nguvu.

Dkt. Dutaqi, akisisitiza kwamba mhimili wa muqawama haupaswi kuiona sheria ya kimataifa kama chombo kilicho mikononi mwa adui au kama muundo ulioshindwa kabisa, alibainisha: Hata ndani ya mfumo usio wa haki, sheria bado ni mojawapo ya nyanja za kutoa uhalali, na madola yenye nguvu za kijeshi hulazimika kuhalalisha vurugu zao kwa lugha ya kisheria. Pengo hili ndilo linalotoa fursa ya kimkakati kwa uingiliaji makini na wenye uhai wa muqawama katika vita vya kisheria.

Akitaja kanuni ya lazima (jus cogens) ya kupiga marufuku mauaji ya kimbari katika sheria ya kimataifa, alisema: Kuzuia kabla hayajatokea, na kukomesha mauaji ya kimbari ni wajibu wa jumla na wa lazima kwa dola zote, na wajibu huu si wa ishara tu. Kwa msingi huo, hatua za muqawama nchini Palestina, Lebanon, Yemen na Iran zinaweza kuundwa kisheria kama utekelezaji wa wajibu wa sheria ya kimataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari.

Dkt. Dutaqi alihitimisha kwa kusisitiza: Mustakabali wa sheria ya kimataifa hautaamuliwa katika kumbi za Baraza la Usalama au Geneva, bali katika medani za mapambano. Ngome ya Heshima ya Kiislamu haipingi tu, bali iko katika mchakato wa kufafanua upya dhana za sheria, uhalali na mpangilio wa dunia; na hasa katika hatua hii ndipo hatima ya mapambano haya itakapogeuka kwa faida ya mataifa yaliyodhulumiwa na kunyanyaswa katika eneo hili.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha