Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Mashhad, Bi. Dalal Abbas, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Lebanon, siku ya Jumatano, katika jopo la kielimu la Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Teolojia ya Muqāwama, lililofanyika chini ya kaulimbiu ya “Vipengele vya Kistratejia vya Hotuba ya Kiteolojia ya Muqāwama”, alisema: Hotuba ya amani na muqāwama katika mwenendo wa Ahlul-Bayt (a.s.) kamwe si misimamo miwili iliyotengana, bali kila mmoja hupata maana yake kamili kulingana na nafasi na wakati wake, na yote mawili yanakamilishana.
Bi. Abbas, akirejea nafasi ya Imam Hasan (a.s.) katika historia ya Uislamu, alisema: Sulhu ya Imam huyo mtukufu haikutokana na udhaifu wala kulegea, bali ilikuwa uamuzi wa kielimu na wa busara kwa ajili ya kuilinda dini, kuzuia kupotoshwa kwa ukweli, na kufichua sura halisi ya dhulma na unafiki.
Alifafanua kuwa: Kukubali kwa Imam Hasan (a.s.) kufanya amani kuliwaondolea watu wasiwasi watu kuhusu Mu‘awiya, na kuliandaa uwanja wa kijamii na kifikra kwa hatua inayofuata ya Umma wa Kiislamu.
Bi. Dalal Abbas alisisitiza: Sulhu hiyo ya kulazimishwa ilikuwa hatua ya kistratejia ya kuzuia kusambaratika kwa jamii ya Kiislamu na kuhifadhi misingi ya dini; na mwenendo wa Imam Hasan (a.s.) ni mfano hai wa namna ya kusimamia hali ngumu na nyeti mbele ya dhulma na ubeberu.
Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Lebanon aliongeza kusema: Mapambano ya Imam Husein (a.s.) katika tukio la Ashura yalikuwa ni jibu la uelewa na la kuwajibika kwa hali ya kulegea, uzembe na kupoteza msimamo wa jamii ya Kiislamu baada ya amani ya Imam Hasan (a.s.).
Aliendelea kufafanua: Mapambano ya Imam Husein (a.s.) yalidhihirisha kwamba; muqāwama si mwitikio wa kihisia au wa ghadhabu ya muda mfupi, bali ni harakati ya kimaadili, yenye uelewa na uwajibikaji, ambayo misingi yake imejengwa juu ya Qur’ani Tukufu, Sunna ya Ahlul-Bayt (a.s.), amr bil-ma‘rūf na kukataza munkar. Mapambano ya Ashura yaliweka wazi mpaka kati ya haki na batili milele, na yakatangaza ukweli huu: Heshima na utu havipatikani bila muqāwama, na kufanya mapatano na dhulma ni usaliti dhidi ya ubinadamu.
Bi. Abbas, akirejea vigezo vya Ahlul-Bayt (a.s.), alisema: Uadilifu ni mhimili mkuu wa hotuba hii, na kila harakati inayompinga Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na maadili ya Kimungu — iwe imevalishwa joho la dini au imejisitiri katika kivuli cha siasa —inastahili kulaaniwa. Ahlul-Bayt (a.s.) hawakuwahi kuifanya dini kuwa chombo cha tamaa ya madaraka; bali kwa kimya chao au kwa msimamo wao, daima walilenga kulinda ukweli wa Uislamu.
Alisisitiza zaidi kuwa: Mapenzi ya kweli kwa Ahlul-Bayt (a.s.), hususan Imam Husayn (a.s.), hayaishii katika maombolezo na hisia pekee, bali hujidhihirisha katika vitendo halisi — katika kuwatetea waliodhulumiwa, kusimama imara dhidi ya dhulma, na kulinda heshima na utu wa mwanadamu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Lebanon aliendelea kwa uchambuzi wa kihistoria wa hotuba ya amani na mapambano katika mwenendo wa Imam Hasan na Imam Husein (a.s.), na kusema: Kwa mtazamo wa kistratejia, njia hizi mbili zinafuata mstari mmoja wa kifikra na kimapambano.
Akiashiria wazo lililowahi kutolewa na Shahid Sayyid Muhammad Baqir al-Sadr, alieleza: Imam Hasan (a.s.), kwa kukubali amani, aliondoa pazia la shubha juu ya Mu‘awiya; na pale jamii ilipofikia ukomavu wa harakati, Imam Hussein (a.s.) alisimama ili kufidia uzembe wa Umma wa Kiislamu na kukabiliana ana kwa ana na utawala wa kidhalimu.
Bi. Abbas alihitimisha kwa kusema: Njia ya amani ya Imam Hasan (a.s.) na njia ya muqāwama wa Imam Husayn (a.s.) zinakamilishana, na zinaonyesha kwa uwazi ulazima wa kuchagua ama amani au muqāwama kulingana na wakati, mazingira na maslahi ya Uislamu.
Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Lebanon, akirejea vipengele vya kistratejia vya hotuba ya muqāwama, alisema: Kufuata mkondo huu ni chanzo cha msukumo wa uhuru, uadilifu na heshima ya binadamu, na mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s.) bado ni mwanga unaoongoza jamii ya Kiislamu katika kukabiliana na dhulma, ufisadi na uistikbari katika dunia ya leo.
Bi. Dalal Abbas alibainisha pia kwamba: Muqāwama hauishii katika uwanja wa mapambano ya kijeshi pekee, bali kila harakati ya kijamii, kitamaduni na kisiasa inayolenga kusimamisha uadilifu na kulinda heshima ya binadamu, huhesabiwa kuwa sehemu ya hotuba ya kiteolojia ya muqāwama.
Maoni yako