Jumapili 21 Desemba 2025 - 09:00
Kudharauliwa Qur’ani Tukufu na Mgombea wa Marekani ni Dalili ya Kushindwa kwa Utamaduni wa Magharibi

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji amelaani vikali kitendo cha mmoja wa wagombea wa Bunge la Marekani cha kudharau hadhi tukufu ya Qur’ani Tukufu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, Imamu wa Swala ya Ijumaa ya Najaf Ashraf, katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa alizozitoa katika Husseinia Kuu ya Fatimiyya mjini Najaf Ashraf, amelaani vikali kitendo cha mmoja wa wagombea wa Bunge la Marekani cha kudharau hadhi ya Qur’ani Tukufu, na akakitaja kuwa ni ushahidi wa “kushindwa kwa utamaduni na ustaarabu wa Magharibi” pamoja na kushindwa kwake kuukabili Uislamu kwa njia sahihi.

Aidha, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya Kiislamu katika sherehe za mwisho wa mwaka, na akabainisha kwamba fatwa za wanazuoni zinathibitisha kuwa sherehe zinazokuza mambo yasiyo ya Kiislamu ni haramu; huku wakati huohuo akisema kwamba sisi tunawapongeza Wakristo katika sikukuu zao.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji, mwanzoni mwa hotuba yake, huku akilaani waziwazi kitendo cha mgombea huyo wa Marekani, alikitaja kuwa ni jaribio ovu la kutumia vibaya tofauti za kikabila na ni mfano wa “kukuza chuki za kidini”, ambacho hakiwezi kamwe kuhesabiwa kuwa kiko ndani ya mipaka ya uhuru wa kujieleza.

Alisema kuwa kitendo hicho ni dharau kwa jamii yenye mchanganyiko wa Marekani, na ni kuvunja heshima ya vitakatifu vya wafuasi wa dini za mbinguni, zikiwemo Ukristo na Uyahudi, na akaonya juu ya madhara yanayoweza kujitokeza katika kuchochea vitendo vya kulipiza kisasi.

Katika muktadha huo, Imamu wa Swala ya Ijumaa ya Najaf Ashraf aliwasilisha hoja na madai yafuatayo:

Taasisi za kisheria za Marekani: zinatakiwa kumuadhibu mgombea huyo kwa kudharau vitakatifu na kuchochea dhidi ya amani ya ndani.

Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC): umuhimu wa kuchukua hatua stahiki katika ngazi ya kimataifa kwa ajili ya kulaani na kusitisha vitendo vya aina hii.

Mashirika ya kiraia ya Marekani: kuchochea maoni ya umma na mhimili wa mahakama ili kuingilia kati katika kesi hii.

Mashirika ya kiraia ya Kiislamu: kuacha majibu ya muda mfupi pekee, na badala yake kupanga na kuratibu hatua, kukusanya vielelezo na kuwasilisha kesi katika vyombo vya kisheria vya nchi iliyofanya kosa.

Kumalizika kwa dhamana ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanji pia alieleza kuwa; kumalizika kwa dhamana ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq ni ishara ya usalama na uthabiti wa kisiasa, na akasisitiza kwamba, Iraq imeingia katika hatua mpya ambayo ndani yake migogoro ya ndani na ya kimadhehebu, pamoja na juhudi za kuuangusha mfumo, kuigawa Iraq, na kudhoofisha uzoefu mpya wa kisiasa, zimefikia mwisho.

Tukio la Australia

Imamu wa Swala ya Ijumaa ya Najaf Ashraf, alilaani shambulio dhidi ya mkusanyiko wa Kiyahudi nchini Australia lililosababisha kuuawa na kujeruhiwa kwa makumi ya watu, na akaeleza fahari yake juu ya msimamo wa kishujaa wa Ahmad al-Ahmad, kijana Mwislamu ambaye kwa ujasiri alimshambulia mmoja wa washambuliaji na kumkamata.

Alitaja kitendo hicho kuwa ni mfano wa maadili ya Kiislamu mbele ya maadili ya ukandamizaji na dhulma, jambo ambalo pia lilipongezwa na Waziri Mkuu wa Australia.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha