Jumatatu 5 Januari 2026 - 13:00
Kilichotokea Venezuela ni kusambaratika mabaki ya mfumo wa dunia na kuanguka kwa maadili na utu wa kimataifa

Hawza/ “Jabha ya Amali ya Kiislamu nchini Lebanon” imetangaza kuwa uvamizi dhalimu na wa khiyana wa Marekani ni uvamizi dhidi ya mabaki ya mfumo wa kisasa wa dunia na ni dalili ya kusambaratika kwake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, “Jabha ya Amali ya Kiislamu nchini Lebanon” katika tamko lake imesema kuwa; uvamizi dhalimu, wa khiyana na unaolaaniwa vikali wa Marekani ni uvamizi dhidi ya mabaki ya mfumo wa kisasa wa dunia na kusambaratika kwake; uvamizi unaoonesha kilele cha unyama usio na mipaka, udikteta wa upande mmoja, na anguko baya na la aibu la maadili na utu wa kimataifa, ambavyo wale wanaodai kwa uongo uhuru, uadilifu, ubinadamu na demokrasia hujinasibisha navyo.

Jabha hiyo ilieleza kuwa: uvamizi huu na kisha kukamatwa kwa Rais wa Venezuela, Maduro, pamoja na mke wake, ni kilele cha ugaidi na uvamizi dhidi ya dola yenye mamlaka, mfumo na sheria, ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na inayotambulika kimataifa.

Jabha ya Amali ya Kiislamu iliongeza kuwa: huu ni uvamizi wa wazi kutoka kwa nchi inayojigamba kwa uadilifu, kulinda amani ya dunia, sheria za kimataifa na uhuru, ilhali kwa vitendo inavunja misingi hiyo yote, kwa sababu tu inataka nchi zote ziwe chini ya kivuli na mwavuli wake wa kisiasa, kiuchumi na wa kimaendeleo. Inasikitisha kwamba katika karne hii ya ishirini na moja, tunashuhudia vita vya mauaji ya kimbari, njaa mbaya, ya kutisha na ya kuogopesha, vita vya kupora mali na kuiba rasilimali za nchi, na vita vya kulazimisha utiifu, kujisalimisha na kunyenyekea chini ya majina na kauli mbalimbali ambazo Mwenyezi Mungu hajateremsha dalili yoyote juu yake; miongoni mwazo ni kile kinachoitwa “amani ya nguvu”.

Jabha hiyo ilibainisha kuwa: hii ni kauli mbiu ya kichokozi na dhalimu ambayo Donald Trump, Rais wa Marekani, anaitekeleza katika kipindi hiki ili kuutangazia ulimwengu kwamba yeye ndiye mtu mwenye nguvu zaidi katika zama hizi, na kama anavyotangaza na kusisitiza, ana haki ya kufanya lolote analotaka na kumshtaki yeyote anayemtaka, kwa sababu ni mwenye nguvu na amekalia kiti cha dola yenye nguvu zaidi duniani.

Jabha ya Amali ya Kiislamu, mwishoni mwa tamko lake, ilihitimisha kwa kusema: hakuna shaka kwamba kilichotokea leo nchini Venezuela ni jambo hatari sana na ni kengele ya wazi ya tahadhari kwa wote; dunia huru haipaswi kukaa kimya mbele ya jambo hili. Na ikiwa itakaa kimya, zamu yake pia itafika, na kisu kitakuwa shingoni mwa kila mmoja; na yule aliyetoa onyo, basi amekwisha toa hoja.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha