Alhamisi 1 Januari 2026 - 22:47
Mwanazuoni Mashuhuri Nchini Tanzania Afariki Dunia

Hawza/ Innā lillāhi wa inna ilayhi rājiuun, Jamii ya Kiislamu nchini Tanzania imekumbwa na pigo kubwa kufuatia kufariki dunia kwa Mwanazuoni mashuhuri, mtetezi mahiri wa Madhehebu ya Ahlulbayt (a.s) na mwandishi mashuhuri wa Kiislamu, Sheikh Ali Jumaa Mayunga, aliyefariki dunia leo tarehe 1 Januari 2026, jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Kwa mujibu wa  Shirika la Habari la Hawza, marehemu Sheikh Ali Jumaa Mayunga alikuwa miongoni mwa wanazuoni waliotumia maisha yao yote katika kuhudumia dini ya Kiislamu, kuutetea ukweli wa Ahlulbayt (a.s), pamoja na kuwaelimisha Waislamu kupitia mihadhara, maandiko na tafiti za kina za kielimu.

Wasifu na Asili ya Maisha

Sheikh Ali Jumaa Mayunga alizaliwa mwaka 1947, katika Mkoa wa Tabora, Wilaya ya Igunga, Tarafa ya Simbo. Tangia ujana wake, alionesha mapenzi makubwa kwa elimu ya dini, tafakuri ya masuala ya Kiislamu na utafiti wa historia ya Uislamu.

Akiwa na ari ya kutafuta ukweli, marehemu hakuridhika na elimu ya juu juu, bali alijitosa katika kusoma kwa kina vyanzo vya Kiislamu, jambo lililompelekea kuwa mmoja wa wanazuoni waliobobea katika masuala ya Aqida, Tafsiri, Historia ya Kiislamu na Fiqhi.

Safari ya Ushia na Kuufahamu Ujumbe wa Ahlulbayt (a.s)

Safari ya marehemu ya kufuata Madhehebu ya Ahlulbayt (a.s) na kuufahamu ushia ilianza rasmi mwaka 1986, alipofanya safari kwenda Mombasa, Kenya. Katika safari hiyo, alipata fursa ya kukutana na mwanazuoni mashuhuri Sheikh Abdillah Nasir, ambapo walifanya mazungumzo ya kina kuhusu historia ya Uislamu, Uongozi baada ya Mtume (s.a.w.w) na nafasi ya Ahlulbayt (a.s) katika dini ya Kiislamu.

Baada ya mazungumzo hayo, Sheikh Mayunga alipata vitabu mbalimbali vya kielimu vilivyomsaidia kufanya utafiti huru na wa kina. Utafiti huo ulimfikisha katika kuutambua na kuufuata ukweli wa Ahlulbayt (a.s), hatua iliyobadilisha kabisa mwelekeo wa maisha yake ya kielimu na da‘wah.

Juhudi za Kielimu na Da‘wah

Katika kipindi chote cha uhai wake, Sheikh Ali Jumaa Mayunga alijulikana kwa uthabiti, ujasiri na hekima katika kuwasilisha hoja za kielimu. Hakujikita katika mihemko, bali alitumia Qur’ani Tukufu, Hadithi sahihi na rejea za kihistoria kuwasilisha ukweli.

Alikuwa mhadhiri, mwalimu na mlezi wa wanafunzi wengi wa elimu ya dini, ambao leo wanaendelea kunufaika na misingi aliyowaachia. Aidha, alitumia kalamu yake kama silaha ya elimu kwa kuandika vitabu na tafsiri mbalimbali zilizoacha alama kubwa katika jamii.

Vitabu Alivyo Andika

Marehemu Sheikh Ali Jumaa Mayunga ataendelea kukumbukwa kwa hazina kubwa ya maandiko ya kielimu aliyoyaacha, miongoni mwa kazi zake maarufu ni kma vile: Tafsiri ya Qur’ani Tukufu, Tarehe ya Kiislamu, Zao la Saqifa, Tafsiri ya Dua Kumayl, Meza ya Uchunguzi pamoja na vitabu vingine vingi vilivyolenga kufafanua misingi ya Uislamu, historia ya Mtume (s.a.w.w) na haki ya Ahlulbayt (a.s). Vitabu hivi vimekuwa rejea muhimu kwa wanafunzi wa elimu ya dini, wahadhiri na watafiti wa masuala ya Kiislamu ndani na nje ya Tanzania.

Pengo Kubwa kwa Umma wa Kiislamu

Kufariki kwa Sheikh Ali Jumaa Mayunga ni hasara kubwa kwa Umma wa Kiislamu, hususan wafuasi wa Ahlulbayt (a.s) nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Ameacha pengo lisilo rahisi kuzibwa katika nyanja ya elimu, da‘wah na uandishi wa Kiislamu.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu amsamehe madhambi yake, aipokee roho yake miongoni mwa waja Wake wema, aipandishe daraja yake Peponi, na awape subira na faraja familia yake, wanafunzi wake na Waislamu wote.

Innā lillāhi wa innā ilayhi rājiʿūn

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha