Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ahmad Al-Qattan, rais wa Jumuiya ya “Qawluna wal-‘Amal” na kiongozi wa kidini wa Kisunni nchini Lebanon, katika hotuba aliyotoa wakati wa kushiriki kwake pamoja na ujumbe wa jumuiya ya “Qawluna wal-‘Amal” katika hafla ya kuadhimisha miaka thelathini na nane ya kuasisiwa kwa Harakati ya Hamas, aliwahutubia watu wote huru na wenye heshima duniani akisema: Hatutofautishi kati ya harakati yoyote ya muqawama. Kama tunavyosimama pamoja na muqawama wa Lebanon, ndivyo tunavyosimama pia pamoja na muqawama wa Palestina. Kama tunavyounga mkono muqawama wa Palestina, ni wajibu wetu kusimama pia pamoja na muqawama wa Lebanon na muqawama wowote mwingine, iwe ni Yemen au nchi nyingine. Kila anayekabiliana na adui Mzayuni, sisi tuko pamoja naye; tunamuunga mkono, na tunasimama pamoja naye ili kukabiliana na udikteta na utawala wa Kizayuni–Marekani.
Alisisitiza kuwa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu, Hamas, itaendelea kubaki imara kama zilivyo harakati nyingine za muqawama, maadamu kuna usiku na mchana, na maadamu bado kuna uvamizi na adui anayevizia ardhi na maeneo yetu matukufu.
Sheikh Al-Qattan aliongeza: Adui huyu, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, hataendelea kusimama milele. Huenda katika baadhi ya nyakati akapata ushindi wa kivita, lakini maadamu harakati za muqawama zipo, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu tutamfukuza kutoka katika ardhi zetu, tutarejea Palestina, na tutaswali pamoja katika Msikiti wa Al-Aqsa.
Kiongozi huyo wa Kisunni kutoka Lebanon pia alirejea kujitolea kwa muqawama nchini Lebanon na Ghaza, akisema: Kutoka kwa wapiganaji wa Ghaza tulijifunza jinsi muumini anavyosimama imara juu ya haki yake. Sisi Walebanoni pia tumeshuhudia ni sadaka zipi muqawama wa Lebanon umeutoa. Tumetoa mali zetu za thamani zaidi, tumewatoa muhanga makamanda wetu mashahidi kwa ajili ya kuiunga mkono Ghaza na kupambana na adui ambaye hanuki hata harufu ya ubinadamu.
Kwa upande mwingine, Sheikh Al-Qattan alikutana na Hussein Al-Nimr, kiongozi wa Hizbullah katika eneo la Biqaa, katika mji wa Baalbek. Katika kikao hicho, Sayyid Faisal Shukr, naibu kiongozi wa eneo hilo, pia alihudhuria.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja, katika kikao hicho pande zote mbili zilijadili maendeleo ya hivi karibuni ya kisiasa katika ngazi ya ndani na ya kikanda, na zikasistiza umuhimu wa kuwa na mtazamo wa pamoja wa kusoma na kuelewa matukio yanayoendelea kwa namna inayohudumia maslahi na uthabiti wa taifa.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa waliohudhuria wameyalaani mashambulizi ya kila siku ya adui wa Kizayuni–Marekani dhidi ya Lebanon, na wakasisitiza haki ya Lebanon ya kujilinda kwa kutumia njia zote zinazowezekana, wakitambua muqawama kuwa ni mojawapo ya aina za ulinzi wa Lebanon na watu wake.
Aidha, mkutano huo ulijadili masuala ya huduma yanayohusiana na eneo la Biqaa, hususan Biqaa ya Kati, pamoja na njia za kuimarisha ustahimilivu wa wakazi wa eneo hilo na kuhakikisha upatikanaji wa mahitaji yao ya msingi katika mazingira ya migogoro iliyopo.
Mwisho, pande zote mbili zilisisitiza juu ya kuendeleza mawasiliano na mikutano ya mara kwa mara, na wakabainisha kuwa jambo hilo linatokana na juhudi za pamoja za kuhudumia maslahi na utoaji wa huduma kwa eneo la Biqaa na watu wake waaminifu.
Katika hitimisho la mkutano huo imeelezwa kuwa, kazi ya pamoja itaendelea kwa msingi wa kipaumbele cha kuwahudumia wananchi na kusimama pamoja nao, kwa kuwa eneo la Biqaa linastahili kuunganishwa kwa juhudi zote ili kuondoa kunyimwa haki na kufanikisha maendeleo yanayohitajika.
Maoni yako