Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha S Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Maher Hammoud, Rais wa Muungano wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Muqawama, alisisitiza kwamba; tangazo la kuuawa kishahidi kwa kundi la makamanda wa Vikosi vya Izzuddin Al-Qassam, akiwemo msemaji wa kijeshi anayejulikana kwa jina la Abu Ubaida, ni tukio chungu na lenye maumivu makubwa; hata hivyo, wakati huohuo ni kitendo kinachoimarisha maana za subira na uthabiti, na kinathibitisha kuwa njia ya muqawama haitasimama, na damu ya mashahidi itaendelea kuwa akiba na nyenzo ya vizazi vijavyo katika kuendeleza safari ya mapambano.
Sheikh Hammoud, akibainisha kuwa, njia hii imeandikwa kwa kujitoa muhanga, aliongeza: Msafara huu, licha ya kupoteza makamanda na wapendwa, na licha ya uharibifu, uhamisho wa kulazimishwa na mateso yanayoandamana nao, unaendelea na safari yake bila kusita.
Rais wa Muungano wa Wanazuoni wa Muqawama, akisisitiza kwamba msafara huu utaendelea kuwepo, wazo halitaangamizwa na njia haitafungwa, alifafanua: Kuuawa kishahidi kwa viongozi mashuhuri wa uongozi, na katika mstari wa mbele, hakumaanishi kupotea kwa ujumbe wala kumalizika kwa chaguo la muqawama; bali ni kinyume kabisa cha hilo.
Ameeleza pia kuwa msemaji wa kijeshi katika kipindi cha miaka ya mapambano alikuwa amegeuka kuwa alama iliyo hai katika vita vya uhamasishaji na uelimishaji wa fikra, na athari yake itaendelea kubaki hai katika dhamiri ya watu hata baada ya kutokuwepo kwake.
Rais wa Muungano wa Wanazuoni wa Muqawama alieleza: Umma unapitia hatua iliyojaa changamoto na kushindwa, lakini mbele ya hali hiyo, mifano imejitokeza iliyokusanya ndani yake maana za heshima, uthabiti na kujitolea.
Aliendelea kusema: Mifano hiyo ni chanzo cha msukumo na inaimarisha imani katika uwezo wa mataifa kustahimili, hata kama ugumu na mashaka yatakuwa makubwa kiasi gani.
Sheikh Hammoud alifafanua kuwa; huzuni ya kuwapoteza mashahidi, pamoja na uharibifu na uhamisho uliolazimishwa kwa watu, ni maumivu ya kweli na yasiyoweza kukanushwa; lakini maumivu hayo hayaui matumaini. Tunahuzunika na kulia, lakini hatukati tamaa; bali tunazidi kusimama juu ya yakini kwamba kujitoa muhanga, hata kukiwa kukubwa kiasi gani, hakutapotea bure.
Rais wa Muungano wa Wanazuoni wa Muqawama, katika hitimisho la maneno yake, alisisitiza kuwa; mashahidi hawapo mbali wala hawajapotea, bali wako hai daima katika fahamu na utambuzi wa watu, na kile walichokitoa kitaendelea kubaki kama hazina ya kimaadili na kiroho kwa vizazi vijavyo. Njia ya uthabiti ni ndefu kuliko watu binafsi na ina nguvu kuliko muda mfupi wa tukio; nayo ina uwezo wa kuendelea bila kukatika, bila kujali mabadiliko ya mazingira na hali.
Maoni yako