Jumamosi 27 Desemba 2025 - 16:30
Kumsahau Mwenyezi Mungu ndio mwanzo wa mwanadamu kuanguka

Hawza/ Kumsahau Mwenyezi Mungu ni mwanzo wa kuanguka kiroho kwa mwanadamu, jambo linaloishia katika kujisahau nafsi yake mwenyewe. Kwa mujibu wa Aya ya 19 ya Suratul Hashr, mwanadamu anayemsahau Mwenyezi Mungu, kutokana na ufuska na maasi, huingia katika mteremko wa kuanguka ambao hatima yake haijulikani. Kurejea katika njia ya kiroho kunahitaji uwepo wa Mwenyezi Mungu kila wakati wa maisha na kujiepusha na madhambi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, kuwa pamoja nasi katika darsa hizi za “mafunzo yanayopatika ndani ya Qur'ani”; mkusanyiko wa aya za Qur’ani Tukufu zenye tafsiri fupi, ambazo ni mwongozo wa maisha na mafanikio, ili kwa aya hizi, tuzitie nuru zaidi siku zetu kwa Maneno ya Mwenyezi Mungu.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Abbas Ashja‘ Isfahani:

Kipimo cha kutathmini hali ya kiroho ya mwanadamu


.وَلَا تَکُونُوا کَالَّذِینَ نَسُوا اللَّهَ فَأَنسَاهُمْ أَنفُسَهُمْ  أُولَٰئِکَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu; Aya ya 19 ya Suratul Hashr inajikita katika “mada muhimu ya kusahau”. Aya hii tukufu inatoa kipimo cha kutathmini hali ya kiroho ya mwanadamu na ni onyo kali kuhusu athari za kumsahau Mwenyezi Mungu. Hoja ya kwanza na ya msingi katika aya hii ni kwamba, ikiwa tunataka kujitathmini sisi wenyewe na kujilinganisha na wengine, Qur’ani inatupa onyo lifuatalo:

“Wala msiwe kama wale waliomsahau Mwenyezi Mungu.” Aya inaendelea kusema: “Basi Akawafanya wazisahau nafsi zao.” Yaani, kumsahau Mwenyezi Mungu husababisha mwanadamu kujisahau mwenyewe. Uhusiano huu wa moja kwa moja kati ya kumsahau Mwenyezi Mungu na kuisahau nafsi ni jambo lenye kina kikubwa sana.

Kwa hiyo, ikiwa mwanadamu anataka kujitathmini ili ajue kama amejisahau au la, ajue yuko katika nafasi gani na kama yuko katika njia sahihi, anapaswa kuangalia: je, amemsahau Mwenyezi Mungu katika maisha yake, au anamkumbuka Mwenyezi Mungu katika mambo yote ya maisha yake?

Akiona kuwa amekuwa kama wale wasiomtaja Mwenyezi Mungu katika jambo lolote la maisha yao, basi ajue kuwa pia amejisahau mwenyewe. Hoja muhimu sana katika aya hii ni kwamba safari yetu kuelekea kwa Mwenyezi Mungu huanzia katika kuijua nafsi.

Kama ilivyokuja katika hadithi maarufu:


من عرف نفسه فقد عرف ربه

“Yeyote anayeitambua nafsi yake, basi amemtambua Mola wake.”

Tunamfikia Mwenyezi Mungu kupitia kuitambua nafsi. Hivyo basi, kuisahau nafsi kunatokana na kumsahau Mwenyezi Mungu, na hapo ndipo kunapoanzia.

Hoja nyingine katika aya hii inaashiria sababu inayomfikisha mwanadamu katika kumsahau Mwenyezi Mungu na kuisahau nafsi. Mwisho wa aya unasema: أولئك هم الفاسقين “Hao ndio wafasiq.” Yaani wale wanaomsahau Mwenyezi Mungu ni watu wa ufuska. Ufuska na uasi, dhambi na maasi, pamoja na kufuata njia ya Shetani, humpelekea mwanadamu kumsahau Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa sifa za wale wanaomsahau Mwenyezi Mungu ni kufanya ufuska na maovu, na kutumbukia katika dhambi na maasi.

Hitimisho muhimu la aya hii ni kwamba, ikiwa tunataka Mwenyezi Mungu awepo katika maisha yetu, ni lazima tujiepushe na maasi. Na ikiwa, Mungu aepushe mbali, tutafanya dhambi, tunapaswa kutubu mara moja ili kumsahau Mwenyezi Mungu kusiishie katika kuzisahau nafsi; kwa sababu kuisahau nafsi humweka mwanadamu katika mteremko wa kuanguka ambao hatima yake haijulikani.

Haijulikani kama mtu atapata mwisho mwema au la, wala ataondoka duniani akiwa katika hali gani. Kwa hiyo, mwanadamu anapaswa kumkumbuka Mwenyezi Mungu katika kila wakati wa maisha yake, ili ajikumbuke mwenyewe na, InshaAllah, asipatwe na maradhi ya kuisahau nafsi yake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha