Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Shab-Zendadar, katika mazungumzo na mwandishi wa Habari wa Shirika la Habari la Hawza, huku akibainisha vipengele mbalimbali vya tukio la Ashura, alisisitiza: Tukio la Ashura, harakati ya Hazrat Sayyid al-Shuhadaa (a.s) na wafuasi wake watukufu, si harakati ya muda mfupi wala iliyofungamana na mwaka 61 Hijria pekee; bali ni harakati ya kimataifa na inayoendelea katika mkondo wa historia kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu.
Mhubiri ni kiungo cha kukamilisha malengo ya Qiyamu ya Sayyid al-Shuhadaa (a.s)
Akirejelea malengo ya harakati hii kubwa, aliongeza kuwa: bila shaka, azma na lengo hili, kwa kuzingatia hali na mazingira tofauti, linahitaji wahubiri na tablighi; kwa sababu mhubiri ndiye kiungo na mkamilishaji wa yale malengo ambayo Sayyid al-Shuhadaa (a.s) alisimama ili kuyatekeleza.
Ayatullah Shab-Zendadar alibainisha kwamba: Lau kujitolea na kujinyima Sayyid al-Shuhadaa (a.s) kusingeambatana na uenezaji wa ujumbe na ufuatiliaji wa malengo hayo kupitia Bibi Zaynab (s.a) na Imam Sajjad (a.s), tukio hili lingebaki bila kujulikana, lingepotea taratibu na hatimaye lingesahaulika.
Aliendelea kusema kuwa: mikusanyiko yote ya maombolezo, maandamano, kupiga kifua na taratibu za kuomboleza ambazo zimehimizwa na kuagizwa na Uislamu, kwa hakika ni mwendelezo wa njia ile ile ambayo Imam Hussein (a.s) aliuwawa kishahidi kwa ajili yake.
Mfanano wa Arbaeen ya Imaam Husseini (a.s) na Hija
Katibu wa Baraza Kuu la Hawza, akirejelea taswira za kisasa za mkondo huu, alisema: mojawapo ya madhihirisho muhimu ya harakati hii, hususan katika zama za sasa, ni suala la Arbaeen ya Imaam Husseini na matembezi yake makubwa; matembezi ambayo kadiri yanavyozidi kupanuka na kuwa ya kimataifa zaidi, na mataifa mbalimbali kushiriki, ndivyo yanavyozidi kufanana na ibada ya Hija.
Akilinganisha Arbaeen na Hija, alisema: kama ambavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu katika faradhi ya Hija, pamoja na ibada na kujikurubisha Kwake, amepanga pia Waislamu wa mataifa mbalimbali wakusanyike katika sehemu moja, wafahamiane, wafahamu matatizo ya wenzao na watafute njia za kuyatatua; vivyo hivyo, suala la Ashura na Arbaeen lina kazi hiyo hiyo, na kwa hakika Arbaeen ni dhihirisho la maana hiyo.
Ayatullah Shab-Zendadar, akirejelea msisitizo mkubwa wa Kiislamu kuhusu ziara ya Sayyid al-Shuhadaa (a.s), alisema: Kupewa umuhimu huu maalumu kwa ziara ya Imam Hussein (a.s), ziara ya mgeni, ziara ya mbali, hata kushauriwa kumkumbuka kila siku na mara kadhaa baada ya swala na ibada, pamoja na kushauriwa kutumia udongo wa kaburi lake tukufu kama muhuri wa swala—yote haya ni kwa ajili ya kukumbusha ukweli huu kwamba tukio kubwa lenye malengo na azma ya juu lilitokea.
Vipengele binafsi na vya kijamii katika kuhuisha maombolezo ya Imam Hussein (a.s)
Aliongeza kwamba: kwa hiyo, mikusanyiko ya maombolezo, kusoma masaibu na kukumbusha dhulma iliyowapata wale watukufu, kila moja linafuata malengo mengi. Mojawapo ya malengo hayo ni kipengele binafsi; yaani kila mtu, kwa kuwazingatia Ahlul-Bayt (a.s), husafishwa na upotovu na maovu, moyo wake huoshwa na uchafu, na wilaya pamoja na mapenzi ya Ahlul-Bayt (a.s)—ambayo ni nguzo thabiti ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu—huimarishwa ndani yake.
Ayatullah Shab-Zendadar, akifafanua kipengele cha kijamii na kiustaarabu cha suala hili, alisisitiza: kipengele kingine cha harakati hii ni kipengele cha kijamii na kiustaarabu. Pale dhana hizi zisiposahaulika na zikisemwa na kuhuishwa daima, athari zake huonekana katika jamii.
Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na Mapinduzi ya Kiislamu uliundwa kwa baraka za Ahlul-Bayt (a.s). Katika tukio la tarehe tisa Dey, fitna ile kubwa iliondolewa kwa sababu gani? Pale kundi la wajinga lilipomvunjia heshima Sayyid al-Shuhadaa (a.s) kwa kudharau bendera na alama za kidini za watu, wananchi kwa sababu ya ile ile ya kushikamana na wilaya walikasirika na wakamiminika barabarani, kwa muunganiko ule ule na Ashura, Sayyid al-Shuhadaa (a.s) na malengo yake, waliiondoa fitna hiyo kubwa.
Muharram na Safar bado ni nguzo ya uhai wa Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu
Aliendelea kusema: pia katika zaidi ya miongo minne iliyopita, ukweli huu umeonekana wazi kwamba kila tatizo linapotokea nchini, kutokana na kufika siku za Ashura, Muharram, Safar na minasaba mengine inayohusiana na Ahlul-Bayt (a.s), matatizo hayo hupungua nguvu na kuyeyuka. Ukweli huu una mizizi katika ufahamu wa kina wa Imam Khomeini (r.a) kuhusu Uislamu na uchambuzi wake wa kiungu; pale aliposema: “Ni Muharram na Safar ndizlvyo vinavyouhuisha Uislamu.”
Ayatullah Shab-Zendadar alisisitiza pia: kila hatua inayochukuliwa kwa ajili ya kuhuisha Muharram na Safar ni yenye thamani, na mojawapo ya mifano iliyo wazi ni matembezi ya Arbaeen ya Husseini (a.s). Kutembea katika njia hii kunamaanisha kwamba uhusiano wetu na Imam Hussein (a.s) ni wa kina na thabiti kiasi kwamba tunajipatia ugumu na taabu hizi, na kutembea kwa miguu makumi ya kilomita; na hili lenyewe ni alama ya mapenzi na mahaba kwa Mtukufu huyo.
Akirejelea nafasi ya hawza za kielimu katika uwanja huu, alisema: Hawza Tukufu ya Kielimu pia hufuatilia mojawapo ya hatua zake muhimu kupitia uongozi wa hawza na programu za tablighi; programu ambazo chini ya uongozi wa Hujjatul-Islam wal-Muslimin Kuhsari na wenzake, kwa mfumo wa kuwatuma wahubiri katika minasaba mbalimbali—ikiwemo siku za Fatimiyya, I‘tikaf, mwezi wa Sha‘ban, mwezi mtukufu wa Ramadhani, Muharram na Safar, pamoja na minasaba mengine—hutekelezwa. Ujumbe huu wa wahubiri, iwe ndani ya nchi au nje ya nchi, wote uko katika mwelekeo wa kutekeleza jukumu la kiasili la hawza.
Ujumbe mkuu wa hawza ni tablighi
Katibu wa Baraza Kuu la Hawza, mwishoni, akitolea dalili Aya Tukufu isemayo:
“فَلَوْلَا نَفَرَ مِنْ كُلِّ فِرْقَةٍ مِنْهُمْ طَائِفَةٌ لِیَتَفَقَّهُوا فِی الدِّینِ وَلِیُنْذِرُوا قَوْمَهُمْ إِذَا رَجَعُوا إِلَیْهِمْ لَعَلَّهُمْ یَحْذَرُونَ”Lakini kwa nini hawatoki baadhi katika kila kundi miongoni mwao, wakajifunze vyema Dini, na kisha waje kuwaonya wenzao watakapo warejea, ili wapate kujihadharisha?
(Sura At-Tawbah, Aya ya 122),
Alisema: kujifunza hukumu za Mwenyezi Mungu na kufikia ufahamu wa kina wa dini ni utangulizi wa kutekeleza jukumu hili la kiungu; na kama ambavyo Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi amesisitiza mara nyingi na pia amebainisha katika ujumbe wa “Hawza Tangulizi”, uwasilishaji ulio wazi (balagh mubiin), tablighi na ufafanuzi ni miongoni mwa majukumu makuu ya hawza, na shughuli nyingine nyingi, kwa hakika, hufanyika katika mwelekeo wa kuandaa mazingira ya utekelezaji wa jukumu hili la msingi.
Maoni yako