Jumanne 6 Januari 2026 - 14:40
Manispaa ya Rovigo yapinga ujenzi wa makaburi ya Kiislamu kwa ajili ya Wislamu kuzikana

Hawza/ Jumuiya ya Waislamu wa Rovigo, baada ya kugharamia kikamilifu mradi huo, imeomba kuanzishwa makaburi ya Kiislamu yaliyo huru, lakini manispaa ya mji huu, licha ya kutokuwepo kiwango chochote cha kifedha, imekataa ombi hilo; uamuzi unaozua maswali mazito kuhusu heshima ya uhuru wa dini, utu wa kibinadamu na usawa wa kweli nchini Italia.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, likinukuu gazeti la Corriere del Veneto, katika mji wa Rovigo kaskazini mwa Italia, ombi lililo wazi, la kisheria na lililogharamiwa kikamilifu la jumuiya ya Waislamu la kuanzisha makaburi ya Kiislamu yaliyo huru, limekumbana na upinzani mkali kutoka kwa manispaa. Hii ni licha ya ukweli kwamba wawakilishi wa Waislamu wamesisitiza kuwa mradi huu hauiletei manispaa mzigo wowote wa kifedha, na kwamba gharama zote — kuanzia ununuzi wa ardhi hadi usanifu, ujenzi na usimamizi — zitagharamiwa kikamilifu na jumuiya ya Waislamu wenyewe.

Abdul-Kabir Luzna, rais wa chama cha “Solidale Senza Frontiere” huko Rovigo na Padova, anasisitiza kuwa ombi hili si dai la kidini pekee, bali linahusiana moja kwa moja na utu wa kibinadamu, heshima ya uhuru wa dini na utambuzi wa tofauti za kitamaduni katika jamii ya kisasa ya Italia. Kwa mujibu wake, “kuanzishwa kwa makaburi ya Kiislamu hakutatui tu tatizo la kivitendo, bali ni jibu la lazima kwa hitaji letu la kina la kuheshimiwa kwa mila na imani zetu.”

Katika ibada ya Kiislamu, kuzikwa kiwiliwili moja kwa moja ardhini na mwelekeo wa kaburi kuelekea Kaaba ni miongoni mwa misingi ya dini, na kuzikwa katika makaburi ya umma yaliyopo hakuhakikishi daima utekelezaji kamili wa masharti haya. Aidha, kusafirisha miili ya marehemu kwenda katika nchi za asili ni jambo gumu au lisilowezekana kwa familia nyingi kutokana na gharama kubwa, hasa ikizingatiwa kwamba idadi kubwa ya Waislamu wameishi Italia kwa miaka mingi na wanapendelea wapendwa wao wazikwe katika mahali walipoishi.

Katika jimbo la Veneto, baadhi ya miji ina sehemu maalumu kwa ajili ya maziko kulingana na taratibu za Kiislamu, lakini katika eneo la Rovigo, makaburi pekee ya Kiislamu yaliyopo yako katika mji wa Adria, na kwa mujibu wa tamko la meya wa mji huo, matumizi yake yamewekewa ukomo kwa wakazi wa Adria pekee. Hivyo basi, licha ya uwepo wa vituo kadhaa vya Kiislamu na idadi kubwa ya Waislamu katika eneo la Polesine, katika mji wa Rovigo wenyewe hakuna nafasi yoyote maalumu iliyotengwa kwa ajili ya maziko kwa mujibu wa ibada ya Kiislamu.

Tukio hili haliwezi kuzingatiwa kama kesi ya pekee au ya kiutawala tu, bali lazima litazamwe katika muktadha wa ubaguzi wa kimuundo dhidi ya Waislamu nchini Italia; ubaguzi wenye mizizi ya kiitikadi ambao kwa miaka mingi umekuwa ukirudiwa katika mijadala ya kisiasa ya mihimili ya mrengo wa kulia. Kusisitiza kile kinachoitwa “mizizi ya Kiyahudi-Kikristo” ya Italia na kuwasilisha Uislamu kama dini ya kigeni na isiyolingana na utamaduni wa Kiitaliano, ni mwelekeo unaofuatwa na sura kama Matteo Salvini na Giorgia Meloni, na kwa makusudi hupuuza uhalisia wa maisha ya mamilioni ya Waislamu wanaoishi nchini humo. Mtazamo huu, katika miaka ya karibuni, sambamba na kuimarika kwa mikondo ya misimamo mikali katika ngazi ya kimataifa na hususan sera za Donald Trump, umeongezeka nguvu, na serikali ya sasa ya Italia pia kwa vitendo inaendelea na mkondo huo huo; mkondo ambao badala ya kukubali tofauti za kidini na mshikamano wa kijamii, unasababisha kupunguzwa kwa haki halali za Waislamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha