Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Akizungumza katika tamasha la Together for Palestine lililofanyika mjini London, Cantona alikumbushia jinsi mashirikisho ya kandanda ya FIFA na UEFA yalivyotoa uamuzi wa haraka na mapema ikiwa ni ndani ya siku nne tu, dhidi ya Urusi kufuatia uvamizi wake huko Ukraine.
Nguli huyo wa soka Barani Ulaya alisema: Siku nne tu baada ya Urusi kuanza vita dhidi ya Ukraine, FIFA na UEFA waliisimamisha mara moja Urusi kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa.
Akaendelea kusema huku akilinganisha na yale wanayoyafanya Israel, akisisitiza kuwa; licha ya ripoti nzito za ukiukwaji wa haki za binadamu na hata mashirika ya kimataifa kama Amnesty International kuutaja mzozo huo kuwa ni “mauaji ya kimbari,” bado Israel inaendelea kuruhusiwa kushiriki kwenye mashindano hayo.
Tumepita siku 716 tangu Amnesty International walipotaja kinachoendelea kuwa ni mauaji ya kimbari, hata hivyo, Israel bado inaruhusiwa kushiriki kwenye mashindano tofauti, hii ni mifumo ya viwango viwili,” aliongeza kusema.
Cantona alieleza wazi kuwa anaona upendeleo mkubwa katika namna vyombo vya soka vinavyoshughulikia mataifa tofauti, huku akisema kwamba hatua ambazo zilichukuliwa haraka dhidi ya Urusi zinapaswa pia kutekelezwa kwa Israel.
Kwa nini kuna ubaguzi huu wa viwango viwili? FIFA na UEFA lazima waifunge Israel, vilabu vyote navyo lazima vikatae kucheza dhidi ya timu kutoka Israel,” alisisitiza Cantona huku akishangiliwa na mamia ya hadhira.
Kwa maneno haya, Cantona amesimama mstari wa mbele miongoni mwa wanamichezo wachache maarufu duniani wanaotumia jukwaa lao kupaza sauti kuhusiana na haki za Wapalestina, na amezitaka taasisi kubwa za soka kushughulikia migogoro kwa misingi ya usawa na haki bila upendeleo wa kisiasa.
Maoni yako