Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi katika ujumbe wake wa tatu wa televisheni kwa wananchi alisema:
Salamu na rehema nyingi ziwe juu ya taifa tukufu na kubwa la Iran. Kwanza, nawakumbuka kwa heshima mashahidi wa thamani wa matukio ya hivi karibuni – mashujaa waliouawa kishahidi, wanachuoni waliouawa kishahidi – ambao kwa hakika walikuwa wana thamani kubwa kwa Jamhuri ya Kiislamu na walilitumikia taifa, na leo hii wako mbele ya Mwenyezi Mungu wakipokea malipo ya huduma zao mashuhuri, inshaa-Allah.
Ninaona kuwa ni wajibu kuwapongeza watu wakubwa wa Iran.
Ninatoa pongezi kadhaa kwa taifa:
Pongezi ya kwanza, ni kwa ushindi dhidi ya utawala bandia wa Kizayuni. Utawala wa Kizayuni, pamoja na makelele yake yote na madai yake yote, umeporomoka karibu kabisa chini ya mapigo ya Jamhuri ya Kiislamu na umesagwasagwa. Wazo la kuwa mapigo kama haya yangeweza kutokea kutoka katika Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya utawala huo halikuwahi hata kupita katika fikra zao, lakini limekuwa kweli. Tunamshukuru Mungu ambaye avisaidia vikosi vyetu vya kijeshi kuvuka ngome zao za ulinzi wa hali ya juu na kuweza kuyaangamiza maeneo mengi ya miji yao na ya kijeshi kwa makombora yao na mashambulizi ya silaha za hali ya juu. Hili ni mojawapo ya neema kubwa zaidi za Mwenyezi Mungu. Ni ishara kwamba utawala wa Kizayuni unapaswa kufahamu kuwa, kufanya uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kunagharimu – na kunaleta gharama kubwa juu yake.
Alhamdulillah, jambo hili limetokea. Heshima ya ushindi huu ni ya vikosi vya kijeshi na ya watu wetu wapendwa waliowalea, kuwasaidia, kuwaunga mkono, na kuwapa nguvu hadi wakawa na uwezo wa kutekeleza kazi hii kubwa.
Pongezi ya pili, ni kwa ushindi wa Iran yetu tukufu dhidi ya utawala wa Marekani. Utawala wa Marekani uliingia kwenye vita ya moja kwa moja kwa sababu uliona kuwa iwapo hautaingia, utawala wa Kizayuni utateketezwa kabisa. Uliingia vitani kwa ajili ya kuunusuru, lakini haukupata mafanikio yoyote. Walishambulia vituo vyetu vya nyuklia – jambo ambalo kwa kweli linastahili kufikishwa mahakama ya kimataifa ya mashtaka ya jinai – lakini hawakuweza kufanya chochote cha maana. Rais wa Marekani alizungumza kwa kuongea kupita kiasi kuhusu kile kilichotokea. Ikabainika wazi kwamba alikuwa na haja ya propaganda hizi kupita kiasi. Yeyote aliyesikia maneno hayo, alielewa kwamba nyuma ya maneno hayo kuna ukweli tofauti. Hawakuweza kufanikisha lengo lao, walikuwa wakifanya propaganda tu ili kuuficha ukweli. Hapa pia, Jamhuri ya Kiislamu imeshinda na imempa Marekani kibano kikali – kwa kuulishambulia moja ya ngome muhimu ya Marekani katika ukanda huu ambayo ni "kambi ya al-‘Udeid", na kuisababishia hasara. Wale wale waliokuwa wakifanya propaganda kubwa katika tukio la awali, hapa wakajaribu kulifanya jambo hilo lionekane kuwa dogo, wakasema hakuna kilichotokea – ilhali tukio hili ni kubwa lilikuwa limetokea.
Kwamba Jamhuri ya Kiislamu imeweza kufikia vituo muhimu vya Marekani katika ukanda huu, na ina uwezo wa kuchukua hatua dhidi yao wakati wowote inapohitajika – hili si jambo dogo; ni tukio kubwa, na linaweza kutokea tena siku zijazo. Iwapo uchokozi wowote utatokea, basi gharama kwa adui na kwa mvamizi hakika itakuwa kubwa.
Pongezi ya tatu, ni kwa ajili ya muungano na mshikamano wa hali ya juu wa taifa la Iran. Alhamdulillah, taifa lenye takriban watu milioni tisini, limeungana, linasema kwa sauti moja, liko bega kwa bega, liko pamoja bila tofauti yoyote katika matakwa na malengo yao. Wamesimama, wamesema kauli moja, wameunga mkono mwenendo wa vikosi vyao vya kijeshi – na hali hii itaendelea.
Taifa la Iran limeonesha utukufu wake, haiba yake ya kipekee, na limethibitisha kwamba wakati wowote inapohitajika, sauti moja tu itasikika kutoka kwa taifa hili – na Alhamdulillah jambo hili limetokea.
Jambo muhimu, ambalo nataka kuliweka wazi kama kiini cha hotuba yangu ni hili:
Rais wa Marekani katika moja ya matamshi yake alisema: Iran inapaswa kujisalimisha. “Kujisalimisha”! Sasa si tena suala la urutubishaji wa nyuklia, wala la teknolojia ya nyuklia; kwa sasa suala ni "kujisalimisha kwa Iran."
Bila shaka, kauli hii ni kubwa mno kwenye mdomo wa Rais wa Marekani, Iran hii tukufu, Iran yenye historia hii, Iran yenye utamaduni huu, Iran yenye azma ya kitaifa – kutamka neno "kujisalimisha" kwa nchi kama hii ni jambo la kuchekesha kwa yeyote anayelifahamu taifa la Iran.
Hata hivyo, kauli hiyo ilifunua ukweli mkubwa kwamba: Wamarekani tangia mwanzo wa Mapinduzi ya Kiislamu wamekuwa wakipigana dhidi ya Iran ya Kiislamu; wamekuwa wakiishambulia kwa kila namna, kila wakati kwa kisingizio kipya: mara haki za binadamu, mara demokrasia, mara haki za wanawake, mara urutubishaji wa nyuklia, mara silaha za nyuklia, mara makombora… Sababu mbalimbali wanazotumia, lakini kiini cha mambo kiko wazi – nacho ni: "wanataka Iran ijisalimishe."
Waliopita hawakuthubutu kusema hilo waziwazi kwa sababu haikubaliki. Katika akili yoyote ya mwanadamu haikubaliki kuwaambia watu: “njooni mjisalimishe.” Ndiyo maana walikuwa wakilificha hilo kwa maneno mengine. Lakini huyu (rais wa sasa) amelisema wazi. Amefichua ukweli: kuwa Wamarekani hawataridhika na chochote pasi na kujisalimisha Iran.
Na hili ni jambo muhimu mno,Taifa la Iran linapaswa kujua kwamba sababu ya mapambano ya Marekani dhidi ya Iran ni hili – ni dharau kubwa kwa taifa la Iran – na jambo kama hilo halitotokea kabisa; kamwe halitatokea.
Taifa la Iran ni taifa kubwa, Iran ni nchi yenye nguvu na pana, Iran ina ustaarabu wa kale. Utajiri wetu wa kitamaduni na kielimu ni mara mia zaidi kuliko wa Marekani na wa walio kama Marekani. Mtu yeyote anayetarajia Iran ijisalimishe kwa nchi nyingine, anasema maneno ya upuuzi yasiyo na msingi – ambayo hakika yatachekesha na kuwashangaza watu wenye busara na akili.
Taifa la Iran ni tukufu, na litaendelea kuwa tukufu. Ni mshindi, na kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, litaendelea kushinda. Tunatumaini kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atalihifadhi daima taifa hili chini ya kivuli cha fadhila Zake, atainua daraja la Imam wetu mkubwa, na BaqiyyatuLlāh (arwāhunā fidaah) awe radhi na taifa hili na msaada Wake uwe daima nyuma ya taifa hili.
Maoni yako