Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kipindi cha ghaiba ya Imamu Mahdi (as) ni kipindi cha fitna, hatari na kukengeuka. Wafuasi wa Imamu aliye ghaiba wanapaswa katika vipindi vyote vya zama hizi, kuwa walinzi wa itikadi zao na walinzi wa mienendo yao, ili wasije wakatoka nje ya mkondo wa kumfuata Imamu, na wakaingia katika mitego ya shetani.
Moja ya nyenzo muhimu kabisa ni dua – kuwasiliana na Mwenyezi Mungu, na pia kuwasiliana na Imamu – ili wasimsahau, na kwa sura ya dhikri, dua na ziara, waendelee kuwa na uhusiano naye.
Imamu Swādiq (as) amesema:
«سَتُصِیبُکُمْ شُبْهَةٌ فَتَبْقَوْنَ بِلاَ عَلَمٍ یُرَی وَلاَ إِمَامٍ هُدًی وَ لاَ یَنْجُو مِنْهَا إِلاَّ مَنْ دَعَا بِدُعَاءِ اَلْغَرِیقِ قُلْتُ کَیْفَ دُعَاءُ اَلْغَرِیقِ قَالَ یَقُولُ یَا اَللَّهُ یَا رَحْمَانُ یَا رَحِیمُ یَا مُقَلِّبَ اَلْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِی عَلَی دِینِکَ.»
“Shubha na fitna zitakupateni, na mtabaki bila ya kiongozi wa kuonekana, wala Imamu wa kuwaongoza. Na hatasalimika kutoka katika fitna hiyo isipokuwa yule ambaye atasoma "du‘ā’ al-gharīq". Nikamwuliza: “Dua ya mtu anayezama ni ipi?” Akasema: “Sema: "Ewe Mwenyezi Mungu, Ewe Mwingi wa Rehema, Ewe Mwingi wa Huruma, Ewe Mgeuza mioyo, thibitisha moyo wangu juu ya dini Yako." (Kamaal al-Dīn, juzuu ya 2, uk. 351)
Katika dua hii imesisitizwa kuwa katika zama za ghaiba ya Imamu ambaye bendera ya uongofu imo mikononi mwake, lazima mtu aombe kwa Mwenyezi Mungu athibitishe hatua zake na imani yake katika dini. Na hili linaonyesha nafasi ya juu sana ya dua.
Imamu Hasan al-‘Askari (as) anasema:
«وَ اللَّهِ لَیغِیبَنَّ غَیبَةً لَا ینْجُو فِیهَا مِنَ التَّهْلُکَةِ إِلَّا مَنْ یثَبِّتُهُ اللَّهُ عَلَی الْقَوْلِ بِإِمَامَتِهِ وَ وَفَّقَهُ لِلدُّعَاءِ بِتَعْجِیلِ فَرَجِه.»
“Naapa kwa Mwenyezi Mungu, ataghaiibu ghaiba ndefu, ambayo hakuna atakayeokoka ndani yake isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu atamthibitisha katika kuamini uimam wake, na amfanikishe katika kumuombea dua ya kuharakisha faraja yake.” (Bihār al-Anwār, juzuu ya 52, uk. 23)
Aidha, kwa mtazamo mwingine, kumuombea dua Imamu wa Zama (as) ni wajibu muhimu kwa wanaomsubiri, ambao umesisitizwa sana na Maimamu (as). Katika baadhi ya riwaya imepokelewa kuwa Imamu Ridha (as) alikuwa akiwaamrisha watu wamwombee dua Sāhib al-Amr (as) na kusema: “Ombeni hivi kwa ajili yake”:
«اللَّهُمَّ ادْفَعْ عَنْ وَلِیکَ وَ خَلِیفَتِکَ وَ حُجَّتِکَ عَلَی خَلْقِکَ… وَ احْفَظْهُ مِنْ بَینِ یدَیهِ وَ مِنْ خَلْفِهِ وَ عَنْ یمِینِهِ وَ عَنْ شِمَالِهِ وَ مِنْ فَوْقِهِ وَ مِنْ تَحْتِه… وَ أَیدْهُ بِنَصْرِکَ الْعَزِیزِ وَ أَیدْهُ بِجُنْدِکَ الْغَالِبِ … وَ وَالِ مَنْ والاهُ وَ عَادِ مَنْ عَادَاهُ.»
Ewe Mola! Muepushe na kila uovu mteule Wako, Khalifa Wako, na Hujja Wako juu ya viumbe Wako… mpatie hifadha kutoka mbele yake, nyuma yake, kulia kwake, kushoto kwake, juu yake na chini yake… Mpe msaada wa ushindi wako mtukufu, na mpe nguvu kwa jeshi lako lisiloshindwa… na mpenda ampendaye, na mchukie amchukiaye. (Bihār al-Anwār, juzuu ya 92, uk. 330)
Kwa hivyo, kumuombea dua Imamu aliye ghaiba na kuwasiliana naye kwa njia ya kiroho na kimaanawi ni miongoni mwa misingi ya kitabia ya Kishia katika zama za ghaiba, ambayo ina athari na manufaa mengi.
Dua na ziara kuhusu Mahdi zinaweza kugawanywa sehemu mbili:
1: Dua na ziara ambazo zimepokelewa moja kwa moja kutoka kwa Imamu Mahdi (as), na ambazo ziliwafikia Mashia kupitia kwa naibu wake maalumu katika kipindi cha Ghaiba ndogo; kama vile Ziara ya Āl Yāsīn na Du‘ā’ al-Faraj.
2: Dua na ziara ambazo zimenukuliwa kutoka kwa Maimamu Ma‘sūmīn (as) kuhusu Imamu Mahdi (as); kama vile Du‘ā’ al-‘Ahd na \Ziara ya Sāhib al-Amr (as) katika Sardāb tukufu huko Samarrā’.
Kumuombea dua Imamu Mahdi (as), kutawassal, na kwenda kumzuru, hakuna muda wala mahali maalumu. Mashia na wanaomngoja mpenzi huyo wanaweza kuzungumza naye, kumtolea salamu na kurejelea ahadi yao kila wakati na kila mahali. Hata hivyo, miongoni mwa siku za juma, siku ya Ijumaa kwa mujibu wa riwaya, imetengwa mahsusi kwa ajili ya Imamu wa Zama (as). Kwa hiyo, kwa siku hiyo kuna ziara maalumu ambayo husomwa kwa jina la "Ziara ya Imamu wa Zama (as)" siku ya Ijumaa.
Katika vitabu vya dua na ziara vilivyoandikwa na maulamaa wa Kishia kama Sayyid Ibn Tāwūs, ‘Allāma Majlisī, na Shaykh ‘Abbās Qummī, dua na ziara nyingi zimepokewa kwa ajili ya Imamu wa Zama (as). Baadhi ya hizo zimekuwa na msisitizo maalumu na mapendekezo kutoka kwa maulamaa hao, na zimepata umaarufu mkubwa zaidi miongoni mwa Mashia.
Utafiti huu unaendelea…
Imenukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho "Negin-e Āfarinish", huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi
Maoni yako