Alhamisi 19 Juni 2025 - 00:07
Taifa la Iran haliwezi kujisalimisha/ Uingiliaji wa kijeshi wa Marekani utakuwa na madhara yasiyorekebishika / Adui wa Kizayuni yupo katika hali ya kuadhibiwa

Hawza: Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba aina yoyote ya uingiliaji wa kijeshi wa Marekani bila shaka utasababisha madhara makubwa yasiyoweza kufidiwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo mchana, kupitia ujumbe wa televisheni, alisifu mwenendo wa staha, ujasiri na utambuzi wa wakati wa taifa la Iran katika kukabiliana na hujuma ya kijinga na ya kishetani ya adui wa Kizayuni, na akaiona kuwa ni ishara ya ukomavu wa taifa na uimara wa akili na kiroho. Alisisitiza kuwa: "Taifa la Iran litasimama kidete mbele ya vita vya kulazimishwa, kama lilivyosimama imara mbele ya amani ya kulazimishwa, na taifa hili halitakubali kulazimishwa wala kumnyenyekea yeyote."

Hadhrat Ayatollah Khamenei, huku akigusia kauli za kitisho na za kejeli zilizotolewa na Rais wa Marekani, alisema: “Watu wenye busara wanaoijua Iran, watu wake na historia yake, hawazungumzi na taifa hili kwa lugha ya vitisho, kwa kuwa taifa la Iran haliwezi kulazimishwa kutii. Na Wamarekani wajue kwamba aina yoyote ya uingiliaji wa kijeshi wa Marekani bila shaka utasababisha madhara makubwa yasiyorekebishika.”

Kiongozi wa Mapinduzi, katika mwanzo wa hotuba yake, aliisifu harakati adhimu ya watu walioshiriki matembezi ya siku ya Ghadir, na pia mikusanyiko na maandamano ya siku za hivi karibuni, hasa baada ya swala ya Ijumaa. Pia alirejelea kitendo kizuri na chenye maana kubwa cha mtangazaji wa kike wa televisheni aliyesimama kidete mbele ya hujuma ya adui, na kusema: “Kusema Allahu Akbar na kuonesha ishara ya nguvu ya taifa kwa dunia nzima ni tukio la kihistoria na lenye thamani kubwa sana.”

Ayatollah Khamenei, akielezea mazingira ya wakati ambao uvamizi wa kijinga na wa kishetani wa utawala wa Kizayuni ulifanyika, alisema: “Tukio hilo lilitokea wakati viongozi wetu walikuwa kwenye mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani, na hapakuwa na dalili yoyote ya hatua kali au kijeshi kutoka upande wa Iran.”

Akaongeza kuwa: “Kwa kweli, tangu mwanzo kulikuwepo na ishara kuwa Marekani ilikuwa na mkono katika uvamizi huo wa kishetani uliofanywa na utawala wa Kizayuni, na kwa matamshi ya hivi karibuni ya viongozi wa Marekani, hisia hizo zinazidi kuthibitishwa kila siku.”

Kiongozi wa Mapinduzi, kwa kusisitiza kuwa “taifa la Iran linasimama kidete mbele ya vita vya kulazimishwa, amani ya kulazimishwa, na aina yoyote ya kulazimishwa”, alisema: “Natarajia kutoka kwa watu wenye fikra, waandishi na wanaopasisha ujumbe kwa umma wa dunia, kuwa waeleze maana hizi kwa uwazi, na wasimruhusu adui kubadilisha ukweli kupitia propaganda zake za udanganyifu.”

Ayatollah Khamenei alisisitiza kuwa adui wa Kizayuni amefanya kosa kubwa na uhalifu mkubwa, na akabainisha: “Adui wa Kizayuni lazima aadhibiwe, na kwa kweli anaadhibiwa. Adhabu iliyotolewa na taifa la Iran na vikosi vyake vya kijeshi kwa adui huyu mwovu, na ile wanayoendelea kuitoa na wanayoipangia siku zijazo, ni adhabu kali ambayo imemdhoofisha vibaya.”

Akaongeza kuwa: “Hata kuingilia Marekani katika uwanja huu ni ishara ya udhaifu na kutoweza kwa utawala wa Kizayuni.”

Kiongozi wa Mapinduzi, pia akirejelea tena kauli za kejeli na za vitisho vya Rais wa Marekani, alisema: “Rais wa Marekani katika matamshi yake yasiyo ya busara amewataka moja kwa moja watu wa Iran wasalimu amri, lakini tunamwambia: Kwanza, toeni vitisho vyenu kwa wale wanaoogopa vitisho, kwa kuwa taifa la Iran linaamini katika aya tukufu inayosema: 'Wala msidhoofike wala msihuzunike, ninyi ndio wa juu zaidi ikiwa mtaamini’ – na vitisho havina nafasi yoyote katika fikra na mwenendo wa taifa la Iran.”

Ayatollah Khamenei alisema: “Pili, kusema maneno kama hayo kwa taifa la Iran kwamba 'njoo usalimu amri', si maneno ya mtu mwenye akili.

Watu wenye busara wanaoijua historia ya Iran na watu wake, kamwe hawasemi maneno kama hayo kwa kuwa taifa la Iran haliwezi kulazimishwa kutii na halitasalimu amri mbele ya yeyote.”Akaongeza kuwa: “Wamarekani, na wote wanaojua siasa za eneo hili, wanajua wazi kuwa kuingilia kwa Marekani katika suala hili kutakuwa na madhara kwao asilimia mia moja. Madhara watakayoyapata yatakuwa makubwa zaidi kuliko yale ambayo Iran inaweza kupata.”

Kiongozi wa Mapinduzi alieleza wazi: “Kujiingiza kwa kijeshi la Marekani katika uwanja huu bila shaka kutasababisha madhara makubwa yasiyorekebishika kwao.”

Ayatollah Khamenei, kwa mara nyingine, aliwashauri watu wa Iran kuzingatia aya tukufu isemayo: 'Wala msidhoofike wala msihuzunike, ninyi ndio wa juu zaidi ikiwa mtaamini’, na akasema: “Endeleeni na maisha kwa nguvu, hasa wale wanaotoa huduma kwa wananchi na wale walio na majukumu ya kuelimisha na kufafanua masuala. Waendelee na kazi zao kwa nguvu na wamtegemee Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ‘ushindi hutoka kwa Mwenyezi Mungu tu, aliye Mtukufu na Mwenye Hekima.’”

Mwisho, alisisitiza: “Hakika Mwenyezi Mungu atalipa ushindi taifa la Iran, na kwa ukweli na haki litashinda bila shaka yoyote.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha