Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Nouri Hamadānī katika maandishi yake kuhusiana na kumbukumbu ya siku ya kufariki kwa Imam Khomeini (ra) amesema:
Muhtasari wa maandishi ya Marja‘ huyu wa taqlīd ni kama ifuatavyo:
Imam (ra) mara nyingi alikuwa akisisitiza kwamba harakati na Mapinduzi haya tuliyoyasimamisha hayawezi kuzimwa wala kumalizika, na ni utangulizi wa kudhihiri kwa Imam wa Zama (aj). Kurudia rudia kwa tamko hili kulionyesha kuwa lilikuwa ni imani ya kina aliyokuwa nayo, na alikuwa akilisema kwa itikadi, imani na hali ya juu ya kiroho:
“Khomeini popote atakapokuwa, yuko pamoja nanyi; bendera hii haitadondoka, na taa hii haitazimika.”
Mimi binafsi, iwe ni huko "Nofel-Loshato" au hapa Iran, katika baadhi ya usiku nilipata taufiki ya kuwa karibu na makazi na chumba chake. Nilikuwa nikishuhudia kuwa mwanzoni mwa usiku alikuwa akitandika jamvi la kuswalia, na kuweka taulo kando yake kwa ajili ya kufutia machozi yake. Alikuwa akiswali "Swalātul-layl" (swala ya usiku) ambayo katika kila “Istighf'ar” machozi yalikuwa yakimtoka.
Baada ya kuswali "Swalātul-layl" kwa namna hiyo, kila asubuhi kabla ya swala ya alfajiri alikuwa akitoka kwenda uani mwa nyumba, akiangalia mbinguni, na akitamka dhikri hii kwa ulimi wake:
“أَصْبَحْتُ فی دارٍ سَقْفُهَا لا إلهَ إلّا اللهُ وَ سُورُهَا مُحَمَّدٌ رَسُولُ اللهِ وَ بابُهَا عَلِیٌّ وَلِیُّ اللهِ وَ ذِکْرُهَا لا حَوْلَ وَ لا قُوَّةَ إلّا بِاللهِ.”
Hakika alikuwa na hali ya kiroho ya pekee. Mambo yote haya yalikuwa yakichimbuka kutoka katika itikadi, imani na fikra yake mahsusi; na msingi wa kazi ulikuwa huo.
Hakika, inapaswa katika "hawza" kuwepo na somo maalumu linalohusiana na hali za kiroho, athari na fikra za Imam.
Kwa vyovyote vile, kila tunapotazama mabadiliko ya ulimwengu, tunatambua kuwa harakati nyingi zenye mvuto wa kimungu zinatokana na Imam (ra). Ukweli huu unapaswa kufikishwa kwa watu ili daima iwe ni dira yetu sisi na ya ulimwengu, iwe ni mfano na chemchemi ya matumaini kwa mataifa, na iwe ni kichocheo cha mabadiliko katika fikra za watu duniani.
Maoni yako