Jumapili 1 Juni 2025 - 21:54
Mwenendo wa Kiserikali wa Imam Mahdi (as)

Hawza/ Mwenendo wa Imam Mahdi (as) ni ule ule wa Mtume Muhammad (saw), na jinsi ambavyo Mtume (saw) katika zama zake alipambana na ujahili kwa kila sura yake, na akausimamisha Uislamu Safi – ambao ni dhamana ya ufanisi wa duniani na Akhera – katika mazingira yake, vivyo hivyo, Imam Mahdi (as) pia, kwa kudhihiri kwake, atakabiliana na ujahili mpya ambao ni mbaya zaidi kuliko ujahili wa zamani, na ataisimika thamani ya uislamu na Mwenyezi Mungu kwenye mabaki ya ujahili wa kileo.

Shirika la Habari la Hawza - Kila mtawala katika serikali na nyanja tofauti za uongozi huwa na mbinu maalum, jambo ambalo ni miongoni mwa sifa za serikali yake. Imam Mahdi (as) pia, atakapokuja kushika hatamu ya uongozi wa ulimwengu, atakuwa na njia maalum katika kuusimamia mfumo wa dunia.

Jambo la kwanza linalopaswa kusisitizwa ni kwamba riwaya zimeeleza taswira ya jumla ya mwenendo wa mkubwa huyo, nayo ni kwamba mwenendo wa Imam Mahdi (as) ni ule ule wa Mtume Mtukufu Muhammad (saw), na jinsi ambavyo Mtume (saw) alipambana na ujahili katika kila sura yake na akauondoa, na akauanzisha upya Uislamu Safi, vivyo hivyo Imam Mahdi (as) atakabiliana na ujahili mpya ambao ni mbaya zaidi kuliko ujahili wa zamani, na ataisimika thamani za uislamu na Mwenyezi Mungu kwenye magofu ya ujahili wa kisasa.

Kutoka kwa Imam Swadiq (as) kunapatikana riwaya kuhusu mwenendo wa Imam Mahdi as ambapo amesema:

«یَصْنَعُ کَمَا صَنَعَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّی اَللَّهُ عَلَیْهِ وَآلِهِ یَهْدِمُ مَا کَانَ قَبْلَهُ کَمَا هَدَمَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّی اَللَّهُ عَلَیْهِ وَ آلِهِ أَمْرَ اَلْجَاهِلِیَّةِ وَ یَسْتَأْنِفُ اَلْإِسْلاَمَ جَدِیداً.»

"Imam Mahdi as atafanya kama alivyotenda Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw); ataangusha yote yaliyokuwa kabla yake kama vile Mtume (saw) alivyoangusha masuala ya ujahili, na ataianzisha upya dini ya Uislamu." (al-Ghaybah an-Nuʿmānī, juz. 1, uk. 230)

Hii ni sera ya jumla ya Imam Mahdi (as) wakati wa utawala wake. Bila shaka, tofauti za nyakati huleta mabadiliko katika mbinu za utekelezaji na uendeshaji wa serikali, jambo ambalo limetajwa katika baadhi ya riwaya.

Mwenendo wa Jihadi na Mapambano wa Imam Mahdi (as)

Imam Mahdi (as) kwa mapinduzi yake ya kimataifa ataangamiza ueneaji wa ukafiri na ushirikina duniani na atawalingania watu wote katika dini tukufu ya Uislamu. Mtume Mtukufu Muhammad (saw) amesema kuhusu hili:

«سُنَّتُهُ سُنَّتِی یُقِیمُ النَّاسَ عَلَی مِلَّتِی وَشَرِیعَتِی.»

"Mwenendo wake [Imam Mahdi (as)] ni mwenendo wangu, atawaweka watu juu ya mila na sheria yangu."(Kamal ad-Din, juz. 2, uk. 411)

Hata hivyo, Imam Mahdi (as) atadhihiri katika hali ambayo haki imekwisha kufafanuliwa wazi na hoja imekamilika kwa watu wote duniani. Hata hivyo, kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, Imam (as) atazungumza na kila dini na kundi kwa mujibu wa misingi ya itikadi yao.

«یَسْتَخْرِجُ التَّوْرَاةَ وَ سَائِرَ کُتُبِ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ مِنْ غَارٍ بِأَنْطَاکِیَةَ وَ یَحْکُمُ بَیْنَ أَهْلِ التَّوْرَاةِ بِالتَّوْرَاةِ وَبَیْنَ أَهْلِ الْإِنْجِیلِ بِالْإِنْجِیلِ وَبَیْنَ أَهْلِ الزَّبُورِ بِالزَّبُورِ وَ بَیْنِ أَهْلِ الْقُرْآنِ بِالْقُرْآنِ.»

Ataitoa Taurati na vitabu vingine vyote vya Mwenyezi Mungu kutoka katika pango lililoko Antakiya, na atahukumu baina ya watu wa Taurati kwa mujibu wa Taurati, na baina ya watu wa Injili kwa mujibu wa Injili, na baina ya watu wa Zaburi kwa mujibu wa Zaburi, na baina ya watu wa Qur'an kwa mujibu wa Qur'an. (al-Ghaybah an-Nuʿmānī, uk. 237)

Mwenendo wa Kihukumu wa Imam (as)

Kwa kuwa Mtarajiwa ameandaliwa kwa ajili ya kusimamisha uadilifu katika dunia nzima, ili atekeleze jukumu hili anahitaji mfumo thabiti wa hukumu. Hivyo basi, katika sehemu hii, Imam Mahdi (as) atafuata njia ya babu yake mtukufu, Imam Ali (as), na kwa jitihada na nguvu atatafuta haki za watu walionyang'anywa haki zao, na atazirejrsha kwa wenyewe popote watakapokuwa.

Inasemwa kwamba baadhi ya riwaya zinaonyesha kwamba Imam Mahdi (as) katika kutoa hukumu atafanya kama vile Nabii Suleiman na Nabii Daud (as), na atahukumu kwa elimu ya kimungu aliyo nayo, si kwa kutegemea maneno ya mashahidi.

Imam Swadiq as amesema kuhusu hili:


«إذا قام قائم آل محمد حکم بحکم داود وسلیمان لا یسأل الناس بینة.»

"Atakaposimama Qa'im wa Aal Muhammad (as), atahukumu kwa hukumu ya Daud na Suleiman (as), (yaani) hatauliza watu ushahidi." (Bihar al-Anwar, juz. 52, uk. 320)

Mwenendo wa kiidara wa Imam (as)

Moja ya nguzo muhimu za utawala ni watendaji wake, wakati viongozi wa serikali ni watu wenye sifa bora, kazi ya serikali na taifa itakuwa katika hali nzuri, na kuyafikia malengo ya serikali itakuwa ni rahisi zaidi.

Mtume Mtukufu Muhammad (saw) amesema katika na hili:

«عَلامَةُ الْمَهْدی اَنْ یکُونَ شَدیداً عَلَی الْعُمّالِ جَواداً بِالْمالِ رَحیماً بِالْمَساکین.»

Alama ya Mahdi (as) ni kuwa mkali (na makini) kwa maafisa wake. Ana mkono wa kutoa kwa wingi na ni mwenye huruma kwa maskini. (Mu‘jam Ahadith al-Imam al-Mahdi as, j. 1, uk. 246)

Mwenendo wa Kiuchumi wa Imam (as)

Imam Mahdi (as), ambaye ni mfano wa uadilifu na haki, ataichukulia "Bayt al-Maal" kama mali ya umma ambayo kila mmoja anashirikiana nayo, kwa namna ambayo hakuna aina yoyote ya ubaguzi au upendeleo katika kugawa rasilimali hizo.

Mtume Mtukufu (saw) anasema:

«اِذا قامَ قائِمُنا اضْمَحَلَّت الْقَطائِعُ فَلاقَطائِع.»

Wakati Qaim wetu atakaposimama, ardhi zilizogawiwa (na tawala za kidhalimu kuwa mali yao au kugawa kwa wengine) zitaondolewa kabisa, kiasi kwamba hakutakuwa tena na ardhi zilizogaiwa kiholela. (Bihar al-Anwar, j. 52, uk. 309)

Miongoni mwa sifa za mfumo wa kifedha wa Imam ni kwamba, kwa lengo la kutatua mahitaji ya kiuchumi na kuhakikisha maisha yenye ustawi wa kutosha kwa watu wote, atawapa watu mali nyingi sana, na katika utawala wake, kila mtu mwenye haja atakayemuomba, atapewa mali nyingi mno.

Mtume Mtukufu (saw) anasema kuhusu hili:

«یکون فی آخر أمتی خلیفة یحثو المال حثوا.»

Mwisho wa umma wangu, kutakuwepo Khalifa atakayetoa mali kwa wingi mno. (Mu‘jam Ahadith al-Imam al-Mahdi as, j. 1, uk. 232)

Mwenendo binafsi wa Imam (as)

Mwenendo wa Imam Mahdi (as) katika mambo yake binafsi na pia katika mahusiano yake na watu wengine, utaonesha mfano wa utawala wa kiislamu ulio bora, ambaye kwa mtazamo wake, utawala ni chombo cha kuwahudumia watu na kuwapeleka kwenye vilele vya ukamilifu, siyo nafasi ya kujipatia mali, kudhulumu, au kuwafanya waja wa Mungu kuwa mateka wa tamaa.

Hakika, huyo Imam wa wacha Mungu katika kiti cha uongozi, ni kumbukumbu ya utawala wa Mtume Mtukufu (saw) na Amiru al-Mu’minin Ali (as). Licha ya kuwa na mali zote na utajiri mkubwa mikononi mwake, katika maisha yake binafsi, atakuwa katika kiwango cha chini kabisa na ataridhika na vitu vidogo zaidi.

Imam Sadiq (as) katika kumfafanua hili anasema:

«فَوَ اَللَّهِ مَا لِبَاسُهُ إِلاَّ اَلْغَلِیظُ وَ مَا طَعَامُهُ إِلاَّ اَلشَّعِیرُ اَلْجَشِبُ.»

Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Hayakuwa Mavazi yake ila mavazi magumu na magumu (ya kawaida kabisa), na hakikuwa chakula chake ila ni shairi. (Al-Ghaybah Shaykh Tusi, j. 1, uk. 459)

Imam Sadiq (as) pia anasema:

«اِنَّ قائِمَنا اِذا قامَ لَبِسَ لِباسَ عَلِی وَ سارَ بِسیرَتِهِ.»

Hakika Qaim wetu atakaposimama, atavaa mavazi ya Ali (as) na atafuata mwenendo wake. (Wasail al-Shia, j. 5, uk. 17)

Utafiti huu unaendelea…

Imenukuliwa kutoka kitabu “Negin-e Āfarinish”, huku ikifanyiwa marekebisho kiasi

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha