Ijumaa 12 Juni 2026 - 14:48
Simulizi yenye Majeraha ya Watoto wa Ghaza; Waandishi wa Habari Walioshinda Tuzo Wataka Ukweli Usikike

Hawza/ Waandishi wawili wa habari kutoka Uholanzi ambao walifanikiwa kupata Tuzo ya Vyombo vya Habari ya Ulaya kwa kuandaa kumbukumbu za majeraha mabaya yaliyowaua watoto wa Ghaza, wameutaka umma na vyombo vya habari kutopuuza matokeo ya ripoti hiyo na kufuatilia ukweli mchungu wa Ghaza kupitia simulizi za madaktari na wahanga.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Shirika la Habari la Anadolu, waandishi wawili wa habari wa Kiholanzi waliotunukiwa tuzo kwa ripoti yao ya uchunguzi iliyopewa jina la “Majeraha Yanasimulia Nini”, kuhusu kuuawa kwa watoto huko Ghaza, wameutaka umma na vyombo vya habari kuonesha umakini zaidi kwenye matokeo ya ripoti hiyo na kutobaki bila kujali yanayotokea Ghaza.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Anadolu, Efting na Finstra, waandishi wawili wa gazeti la Kiholanzi De Volkskrant, waliotunukiwa tuzo kwa ripoti ya “Majeraha Yanasimulia Nini”, walitoa maelezo katika mahojiano yao na Shirika la Habari la Anadolu kuhusu tuzo hiyo na mchakato wa kuandaa ripoti hiyo.

Waandishi hao wawili walisisitiza kwamba; wanachukulia kupokea tuzo hiyo kuwa ni motisha ya kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kitaaluma wa uandishi wa habari na kushughulikia masuala magumu na nyeti zaidi.

Efting alisema kwamba; kwa kuwa waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia Ghaza, waliamua kuzungumza na madaktari ambao walikuwa mashahidi wa mwisho wa kimataifa waliokuwapo Ghaza, na kuwauliza kuhusu walichokiona na uzoefu wao.

Aliongeza kuwa: “Natumaini kwamba; yale yaliyotokea Ghaza na kulengwa kwa raia yataweza kuvutia umakini mkubwa zaidi. Tuliamua kuitazama Ghaza kupitia mtazamo wa madaktari, na hapo ndipo kazi ilipoanza, swali kuu katika mahojiano yetu na madaktari lilikuwa kwamba, walikuwa wameona watoto wangapi wenye umri wa miaka 15 au chini ya hapo waliolengwa kwa risasi moja kichwani au kifuani.”

Efting pia alisema: “Ripoti yetu inaonyesha kwamba aina ya majeraha ya watoto hawa yanaashiria uwepo wa mashambulizi yaliyolengwa kwa makusudi, kwa sababu hiyo ninaamini watu wanapaswa kuisoma tena ripoti hii ili wafahamu kuhusu kulengwa kwa watoto huko Ghaza na yale yaliyotokea huko.”

Finstra pia alisema kwamba; madaktari wote waliorejea kutoka Ghaza walihisi kuwa walipaswa kuueleza ulimwengu yale waliyojionea. Alifafanua: “Wao huenda Ghaza kama madaktari kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa, lakini wanapoona kwa macho yao hali ya kutisha iliyopo huko, wanafikia hitimisho kwamba, kuwa daktari pekee haitoshi; wao pia ni mashahidi wa matukio hayo na wanapaswa kuyafikisha kwa walimwengu.”

Finstra alisema kwamba; wakati mwingine walizungumza na madaktari kwa saa nyingi, na kwa ajili ya kuthibitisha simulizi hizo waliwaomba wawasilishe nyaraka na ushahidi, matokeo yake, picha, video, taswira za kitabibu, kumbukumbu za matibabu na hati mbalimbali zilikusanywa.

Pia alirejelea nafasi ya daktari wa Marekani, Dk. Feroze Sidhwa, ambaye alikuwa miongoni mwa vyanzo muhimu vya ripoti hiyo, kwa mujibu wa Finstra, Sidhwa alituma dodoso kwa zaidi ya madaktari 60 wa Marekani waliokuwa wamefanya kazi Ghaza na kuwauliza kuhusu matukio kama vile njaa, watoto waliojeruhiwa kwa risasi, na hali nyingine za kibinadamu walizozishuhudia.

Finstra alisema kuwa; mbinu hiyo ilikuwa njia yenye ufanisi ya kufichua mfumo au muundo maalumu wa matukio, lakini gazeti la  The New York Times liliwasilisha suala hilo si kama ripoti ya habari, bali katika mfumo wa makala ya maoni, jambo ambalo kwa mtazamo wao lilikuwa la kushangaza.

Finstra, akizungumzia hali ya mgawanyiko mkubwa inayotawala mijadala kuhusu Ghaza duniani kote na pia nchini Uholanzi, alisema kwamba; walipokuwa wakifanyia kazi mada hiyo walijua tangu mwanzo kuwa wangekabiliwa na ukosoaji na uchunguzi mkali.

Aliongeza kusema: “Tulihakiki vyanzo vyetu vyote kwa umakini mkubwa kadiri ilivyowezekana, tulichunguza picha na nyaraka tulizotumiwa, na pia tulitumia msaada wa wataalamu. Sisi si wataalamu wa tiba ya uchunguzi wa kisayansi wa maiti, na hatuwezi kutoa hukumu kuhusu undani wa jeraha au namna risasi ilivyopiga kwa kutegemea tu picha ya kitabibu.”

Kwa mujibu wake, kwa ajili ya kuchambua picha za kitabibu na kuchunguza mifumo iliyokuwapo, walisaidiwa na wataalamu wawili wa tiba ya uchunguzi kutoka Uholanzi na Ubelgiji, pamoja na wataalamu wa jeshi la Uholanzi.

Finstra alisisitiza kwamba; licha ya uchunguzi huo mpana, ripoti yao inayozungumzia kulengwa kwa makusudi kwa watoto huko Ghaza bado inakabiliwa na ukosoaji na miitikio mbalimbali.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha