Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Shirika la Habari la ON4, ripoti mpya zinaonyesha kwamba; makumi ya mashirika ya hisani yaliyosajiliwa nchini Uingereza yamehamisha mamilioni ya pauni za misaada ya kifedha kwa taasisi na miradi inayohusishwa na makazi ya walowezi wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Suala hili limezua ukosoaji mkali kutoka kwa baadhi ya wabunge wa Uingereza na wito wa kufanyika uchunguzi pamoja na kufutwa kwa leseni za mashirika hayo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya Uingereza, Melanie Ward, mbunge wa Chama cha Labour katika Bunge la Uingereza, alitahadharisha kwamba; ikiwa misaada hiyo imejumuishwa katika mfumo wa misamaha ya kodi ya mashirika ya hisani (Gift Aid), basi walipa kodi wa Uingereza kwa vitendo wamechangia takribani pauni milioni 5.6 kwa shughuli zinazohusiana na makazi haramu ya walowezi wa Israel, alielezea hali hiyo kuwa “ya kusikitisha”.
Wakati huohuo, Yvette Cooper alitangaza kwamba; Tume ya Kusimamia Mashirika ya Hisani ya Uingereza imepewa jukumu la kuchunguza uhusiano wa mashirika ya hisani ya Uingereza na makazi ya walowezi wa Israel.
Melanie Ward, ambaye hapo awali alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Medical Aid for Palestinians, katika barua yake kwa taasisi ya usimamizi wa mashirika ya hisani, alitaka kufanyike uchunguzi kuhusu shughuli za mashirika hayo na yaondolewe kutoka katika orodha ya mashirika ya hisani yaliyosajiliwa.
Katika barua hiyo alisisitiza kwamba; upanuzi na kuendelea kuwepo kwa makazi ya walowezi wa Israel katika ardhi za Palestina kunatambuliwa na jumuiya ya kimataifa kuwa moja ya vikwazo vikubwa vya kufikiwa kwa amani. Kwa mujibu wake, msaada wowote wa kifedha kwa shughuli zinazosaidia kulinda au kupanua makazi hayo ni sawa na kuunga mkono misimamo mikali na unapingana na maslahi ya umma wa Uingereza pamoja na misingi ya sheria za kimataifa.
Tuhuma za Kufadhili Makundi ya Misimamo Mikali
Miongoni mwa taasisi zilizotajwa ni Kasner Charitable Trust na shirika la hisani la UK Toremet. Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa mwaka uliopita, UK Toremet ilifanya kazi kama mpatanishi wa kifedha, na taasisi hizi mbili kwa pamoja zilitoa takribani pauni milioni 5.7 kwa shule ya dini ya Bnei Akiva Yeshiva iliyoko katika makazi ya walowezi ya Susiya katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Aidha, watafiti baada ya kuchunguza nyaraka za Kiingereza na Kiebrania walitangaza kwamba; taasisi ya Kasner pia ilitoa msaada wa kifedha kwa shule ya dini katika mji wa Hebron.
Ripoti pia zinaonyesha kwamba UK Toremet mwaka 2022 ilitoa pauni 38,479 kwa kundi la walowezi wenye misimamo mikali la Regavim, kundi ambalo linaunga mkono ubomoaji wa nyumba za Wapalestina na ambalo limewekewa vikwazo na European Union.
Vilevile, imeelezwa kwamba; kupitia jukwaa la Jgive, ambalo hushughulikia malipo ya kifedha ya UK Toremet, kulikuwepo uwezekano wa kutoa misaada kwa makundi mengine ya walowezi, ikiwemo Shivat Zion Lerigvy Admata, kundi ambalo Uingereza imetangaza kuwa inapanga kuliwekea vikwazo.
Utetezi wa Mashirika ya Hisani
Msemaji wa UK Toremet, akijibu tuhuma hizo, alisema kwamba; taasisi ya usimamizi wa mashirika ya hisani ya Uingereza hapo awali ilithibitisha kuwa shughuli za shirika hilo ni halali kisheria.
Pia alieleza kwamba malipo yote yaliyofanywa kupitia Jgive yaliidhinishwa tu baada ya uchunguzi unaohitajika kufanyika, na yalielekezwa kwenye miradi iliyokuwa inaendana na malengo ya shughuli za hisani.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, kundi la Shivat Zion Lerigvy Admata halimo katika orodha ya walengwa waliothibitishwa na taasisi hiyo. Aidha, msaada wa kifedha uliotolewa kwa Regavim ulihusiana na mradi uliotekelezwa ndani ya mipaka ya Israel ya kabla ya mwaka 1967.
Aliongeza kwamba, shirika la Regavim pia kwa sasa halipo tena katika orodha ya walengwa walioidhinishwa na UK Toremet.
Maoni yako