Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah al-Udhma Ja’far Subhani, jioni ya leo, katika hotuba yake kwenye kongamano la kimataifa la kumbukumbu ya miaka mia tangu kuasisiwa upya Hawza ya Qom, lililofanyika katika Madrasa ya Imam Kadhim (a.s.), kwa kurejelea hadithi isemayo:
«العالم بزمانه لا تهجم علیه اللوابس»
Mwenye elimu katika zama zake, shubha hazimshambulii
Alisema: Hadithi hii inabainisha sifa mashuhuri ya maulamaa na mujtahidina wanaoutambua vyema wakati wao, na Ayatollah al-Udhma Haj Sheikh Abdulkarim Ha’iri Yazdi alikuwa mfano kamili wa hadithi hii tukufu.
Akiangazia historia ya Hawza, aliongeza kuwa: Hawza ya kwanza ya hadithi na fiqhi ilianzishwa mjini Madina baada ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w.), na hadi tukio la Fakh, Madina ilikuwa kituo cha kulea maulamaa wakubwa kama vile Abdullah bin Abbas, Ubay bin Ka‘b na Abdullah bin Mas‘ud. Kwa kuingia kwa Banu Marwan, hali hii ilipungua, lakini katika zama za Imam Baqir (a.s.) na Imam Swadiq (a.s.) ilifufuliwa tena, na wanafunzi wao wakaendeleza njia hiyo.
Ayatollah Subhani vilevile alisema: Hawza ya pili iliundwa katika Msikiti wa Kufa, mahali ambapo wanafunzi wa Imam Baqir (a.s.) na Imam Swadiq (a.s.) walifundisha fiqhi na hadithi. Baadaye, kufuatia kuhamishwa kwa lazima kwa Imam Ridha (a.s.) kwenda Khorasan, Hawza ya tatu ya Kishia iliwekwa msingi katika eneo hilo, ambayo ilitekeleza jukumu muhimu sana katika kueneza mafundisho ya Kiislamu.
Akaelezea kuwa Hawza ya Qom kuwa ni mwendelezo wa njia hii yenye nuru, na akasema: Tangia kuwasili kwa Banu Ash‘ari mjini Qom, mji huu ukawa moja ya vituo muhimu zaidi vya elimu na fiqhi ya Kishia. Viongozi wakuu wengi kama vile Muhammad bin Ahmad bin Yahya Ash‘ari na Ahmad bin Abi Abdillah Barqi walikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa wa kipindi hicho.
Ayatollah Subhani, kwa kuashiria kipindi cha kudhoofika kwa Hawza ya Qom katika karne ya saba Hijria kutokana na uvamizi wa Wamongolia, alizungumzia mazingira ya kufufuliwa tena kwa Hawza hii katika enzi ya Safawi, na kufikia kilele chake katika karne ya kumi na moja kwa kuwepo kwa nyuso mashuhuri kama vile Sheikh Bahai, Mulla Sadra, Faydh Kashani na Fayadh Lahiji.
Akaelezea karne ya kumi na tatu kuwa ni enzi ya kung'ara kwa Mirza-ye Qummi mjini Qom, na kuhusu karne ya kumi na nne alisema: Katika karne hii, Marehemu Haj Sheikh Abdulkarim Ha’iri, kwa uelewa wa kina wa mahitaji ya zama, aliweka msingi wa awamu mbili za Hawza ya kielimu huko Arak, na hatimaye kwa mwaliko wa maulamaa wa Qom, akaasisi tena Hawza ya mji huu.
Kiongozi huyo mkubwa pia aliongeza kuwa: Haj Sheikh, kwa kujiepusha na mirengo ya kisiasa katika harakati ya Mashrutiya, alionyesha wazi kwamba wasiwasi wake pekee ulikuwa ni kulinda Hawza na kulea maulamaa wa dini. Alikuwa anaamini kuwa katika hali ya misukosuko ya kisiasa, ni lazima ngome ya dini na uongozi wa kisheria ilindwe kwa kulea maulamaa na walinganizi wa dini.
Ayatollah Subhani, katika hitimisho la hotuba yake, kwa kurejelea athari za kielimu za Marehemu Haj Sheikh, vikiwemo vitabu vyake vya Swalat na Usul, alisema: Marehemu Ayatollah al-Udhma Borujerdi alikuwa akimwona Haj Sheikh kuwa ni mwanachuoni aliyekuwa akihamisha maarifa makubwa kwa maneno mafupi. Pia, Ayatollah Sayyid Muhsin Jabal ‘Amili katika kitabu chake A’yan al-Shi‘ah alisisitiza sifa za zuhudi, umakini na uelewa wa zama wa Haj Sheikh – sifa zote hizi ni funzo kubwa kwetu.
Maoni yako