Jumamosi 17 Oktoba 2026 - 15:09
Jamii Ina Wajibu wa Kuzingatia Malezi Bora ya Watoto/ Mitandao ya Kijamii Itumike Vizuri

Hawza/ Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Mashia Tanzania (TIC) na Imam Mkuu wa Msikiti wa Ghadir, uliopo Kigogo Post, jijini Dar es Salaam, ameitaka jamii kutoa kipaumbele katika malezi bora ya watoto, huku akisisitiza kuwa mtoto mwema ni neema kubwa kwa wazazi wake, si katika maisha ya dunia pekee, bali hata baada ya kufariki kwao.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, akizungumza katika khutuba ya Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa jana katika Msikiti wa Ghadir, Sheikh Jalala, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Hawza ya Imam Swadiq (a.s.), ameeleza umuhimu wa wazazi kutimiza wajibu wao katika kuwalea watoto kwa misingi ya maadili mema, mafundisho ya dini na heshima kwa wazazi, hususan katika kipindi hiki ambacho jamii inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimaadili.

Sheikh Jalala alianza khutuba yake kwa kusoma aya ya 59 ya Suratul Maryam, inayozungumzia hali ya baadhi ya vizazi vilivyokuja baada ya watu wema, vikapuuza Swala na kufuata matamanio yao. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’ani Tukufu:

﴿فَخَلَفَ مِنۢ بَعۡدِهِمۡ خَلۡفٌ أَضَاعُوا۟ ٱلصَّلَوٰةَ وَٱتَّبَعُوا۟ ٱلشَّهَوَ ٰ⁠تِۖ فَسَوۡفَ یَلۡقَوۡنَ غَیًّا ﴾

“Lakini wakaja baada yao watu wabaya walioacha Swala na wakafuata matamanio yao, basi watakutana na adhabu ya upotovu.”

(Suratul Maryam: 59)

Akifafanua aya hiyo, Sheikh Jalala alisema kuwa; hali inayozungumziwa katika aya hiyo inafanana na changamoto zinazoikabili jamii ya leo, ambapo baadhi ya watu wanapuuza misingi ya dini na maadili, hali inayoweza kuathiri mwenendo wa watoto na kizazi kijacho.

Alisisitiza kuwa; kipindi cha sasa kinahitaji wazazi na walezi kuongeza juhudi katika kuwalea watoto wao, hasa kutokana na kuongezeka mmomonyoko wa maadili na changamoto zinazowakabili vijana katika mazingira yao ya kila siku.

Aliongeza kuwa; kuna juhudi na ushawishi mbalimbali unaoweza kutumiwa kuathiri malezi ya watoto, hivyo wazazi wanapaswa kuwa macho na kuhakikisha kuwa watoto wao wanakulia katika mazingira yanayowajenga kiimani, kiakhlaki na kitabia.

Mtoto mwema ni neema kubwa kwa wazazi

Katika sehemu nyingine ya khutuba yake, Sheikh Jalala alieleza nafasi na fadhila za mtoto mwema katika maisha ya wazazi, huju akibainisha kuwa mtoto mwenye maadili mema ni miongoni mwa neema kubwa ambazo Mwenyezi Mungu humjaalia mwanadamu.

Katika kuthibitisha hilo, alinukuu riwaya kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) inayosema:

«مِنْ سَعَادَةِ الرَّجُلِ الْوَلَدُ الصَّالِحُ»

“Miongoni mwa mambo yanayomletea mwanadamu furaha ni kuwa na mtoto mwema.”

(Bihar al-Anwar, Juzuu ya 104, uk. 98, riwaya ya 67.)

Akifafanua riwaya hiyo, Sheikh Jalala alieleza kuwa; mtoto mwema ni chanzo cha furaha na baraka kwa wazazi wake, kwani wema wake huonekana kupitia tabia, mwenendo na namna anavyowatendea watu, hususan wazazi wake.

Alisisitiza kuwa; malezi bora yanapaswa kumjenga mtoto katika hali ambayo atatambua wajibu wake kwa wazazi, kuwaheshimu na kuwahudumia, badala ya kusubiri mpaka waeleze mahitaji na matatizo yao.

Katika kueleza zaidi umuhimu wa kuwafanyia wema wazazi, Sheikh Jalala alisoma aya ya 23 ya Suratul Israa, ambayo inasisitiza kumuabudu Mwenyezi Mungu na kuwatendewa wema kwa wazazi wawili.

Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعۡبُدُوا۟ إِلَّا إِيَّاهُ وَبِٱلْوَٰلِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴾

“Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote isipokuwa Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee akiwa kwako, au wote wawili, basi usiwaambie hata ‘Ah!’ Wala usiwakemee, na sema nao kwa maneno ya heshima.”

(Suratul Israa: 23)

Akifafanua aya hiyo, Mkurugenzibwa hawza ya Imaam Swa'adiq alisema kuwa; mtoto mwema ni yule anayejitahidi kutambua mahitaji ya wazazi wake na kuwahudumia kwa moyo wa upendo na huruma, bila kusubiri mpaka wazazi hao waeleze matatizo yao au kuomba msaada. Alieleza kuwa kuwafanyia wema wazazi si jambo linalopaswa kufanywa kwa maneno pekee, bali inapaswa kudhihirika katika matendo, ikiwemo kuwahudumia, kuwajali, kuwaheshimu na kuhakikisha wanapata mahitaji yao kadiri ya uwezo wa mtoto.

Malezi bora huacha alama hata baada ya kifo

Katika kuzungumzia mafanikio ya malezi, Sheikh Jalala alieleza kuwa: Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alifanikiwa katika malezi ya kizazi chake, kama ambavyo Bibi Fatimah Zahraa (s.a.) na Imam Ali (a.s.) walivyofanikiwa katika malezi yao.

Alisisitiza kuwa malezi bora hayapimwi kwa mafanikio ya mtoto katika maisha ya dunia pekee, bali pia kwa athari njema anazoendelea kuziacha katika jamii na kwa wazazi wake, hata baada ya wao kufariki.

Katika kufafanua jambo hilo, alinukuu riwaya ifuatayo:

«لَيْسَ يَتْبَعُ اَلرَّجُلَ بَعْدَ مَوْتِهِ مِنَ اَلْأَجْرِ إِلَّا ثَلَاثُ خِصَالٍ صَدَقَةٌ أَجْرَاهَا فِي حَيَاتِهِ فَهِيَ تَجْرِي بَعْدَ مَوْتِهِ إِلَى يَوْمِ اَلْقِيَامَةِ صَدَقَةٌ مَوْقُوفَةٌ لَا تُورَثُ أَوْ سُنَّةُ هُدًى سَنَّهَا فَكَانَ يَعْمَلُ بِهَا وَعَمِلَ مِنْ بَعْدِهِ غَيْرُهُ أَوْ وَلَدٌ صَالِحٌ يَسْتَغْفِرُ لَهُ»

“Hakuna malipo ya thawabu yanayoendelea kumfuata mwanadamu baada ya kifo chake isipokuwa mambo matatu: Sadaka aliyoitoa na kuifanya iendelee kutumika katika uhai wake, ambayo huendelea kuleta thawabu baada ya kifo chake mpaka Siku ya Kiyama; sadaka ya kudumu ambayo hairithiwi; au mwenendo mwema aliouanzisha na kuufanyia kazi, kisha wengine wakaufuata baada yake; au mtoto mwema anayemuombea msamaha.”

(Al-Kafi, Juzuu ya 7, uk. 56.)

Akifafanua riwaya hiyo, Sheikh Jalala alieleza kuwa mtoto mwema anaweza kuwa sababu ya kuendelea kumpatia mzazi wake thawabu hata baada ya kufariki kwake, kupitia dua, kuomba msamaha na kufanya matendo mema kwa nia ya kumfikishia thawabu.

Kisa cha Nabii Isa (a.s.) na mtoto aliyekuwa sababu ya kusamehewa kwa mzazi wake

Ili kufafanua zaidi athari za matendo mema ya mtoto kwa mzazi wake aliyefariki, Sheikh Jalala alisimulia kisa cha Nabii Isa (a.s.), ambaye siku moja alipita karibu na kaburi na kusikia kuwa mtu aliyezikwa humo alikuwa akiadhabiwa. Baada ya kupita mwaka mmoja, Nabii Isa (a.s.) alipita tena katika kaburi hilo, lakini safari hii hakusikia sauti ya adhabu kama alivyokuwa amesikia hapo awali. Jambo hilo lilimfanya amuulize Mwenyezi Mungu kuhusu sababu iliyosababisha adhabu ya mtu huyo kukoma.

Kwa mujibu wa kisa hicho, Mwenyezi Mungu alimteremshia wahyi Nabii Isa (a.s.) na kumweleza kuwa marehemu huyo alikuwa ameacha mtoto mwema, mtoto huyo alijenga barabara na kuwasaidia yatima, kisha akaomba thawabu za matendo hayo mema zimfikie mzazi wake aliyefariki. Kwa sababu ya matendo hayo mema na dua ya mtoto wake, Mwenyezi Mungu alimsamehe marehemu huyo, na hivyo adhabu aliyokuwa akipata ikakoma.

Kupitia kisa hicho, Sheikh Jalala alisisitiza kuwa malezi bora yanaweza kuzaa matunda yenye athari kubwa kwa wazazi na jamii kwa ujumla. Aidha, kisa hicho kinaweka wazi umuhimu wa kuwalea watoto wanaotambua thamani ya matendo mema, kuwasaidia wenye mahitaji na kuwaombea wazazi wao dua.

Wazazi watakiwa kuwa makini na malezi katika zama za mitandao ya kijamii

Katika sehemu ya mwisho ya khutuba yake, Sheikh Jalala alirejea umuhimu wa malezi bora na kuonya kuhusu changamoto za kimaadili zinazoweza kuathiri watoto katika kipindi cha sasa.

Akizungumzia suala la ushoga na usagaji, alieleza wasiwasi wake kuhusu ushawishi wa maudhui na mitazamo inayohusiana na mapenzi ya jinsia moja, akiwataka wazazi kuimarisha malezi ya watoto wao kwa mujibu wa mafundisho ya dini na maadili wanayoyaamini.

Katika muktadha huo, alidai kuwa baadhi ya ushawishi kutoka nchi za Magharibi unaweza kuchangia kuathiri maadili ya vijana barani Afrika, hivyo akasisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuwa makini na mazingira yanayowazunguka watoto wao.

Vilevile, Sheikh Jalala alieleza kuwa jukumu la malezi haliishii katika kuwapatia watoto chakula, mavazi, elimu na mahitaji mengine ya kimwili, bali linahusisha pia kuwafuatilia, kuwashauri, kuwaongoza na kuwajengea uwezo wa kutambua mambo yanayoweza kuwaathiri katika maisha yao.

Alionya kuwa kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii kunahitaji wazazi kuwa na uelewa na uangalizi zaidi, kwa kuwa wakati mwingine wanaweza wasifahamu aina ya maudhui ambayo watoto wao wanakutana nayo kupitia majukwaa kama Instagram, WhatsApp, Facebook na mitandao mingine.

Alisisitiza kuwa; wazazi wanapaswa kuchukua hatua za makusudi katika kuwafuatilia watoto wao, kuwajengea mawasiliano ya karibu na kuwaelimisha kuhusu namna ya kutumia teknolojia kwa uwajibikaji, huku wakihakikisha kuwa watoto wanapata malezi yanayowawezesha kutofautisha mema na mabaya.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha