Jumapili 11 Oktoba 2026 - 16:50
Wanazuoni wa Bahrain Watoa Tamko Kali Kupinga Maamuzi ya Hivi Karibuni ya Utawala wa Al Khalifa Kuhusu Masuala ya Kisheria na Kiislamu

Hawza/ Wanazuoni wa Bahrain wametoa tamko la kuunga mkono taarifa ya Ayatullah Sheikh Isa Qassim, kiongozi wa harakati ya Kiislamu nchini Bahrain, kuhusu maamuzi ya hivi karibuni yaliyofanywa na utawala wa Al Khalifa nchini humo.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, wanazuoni wa Bahrain wametoa tamko la kuunga mkono taarifa ya Ayatullah Sheikh Isa Qassim, kiongozi wa harakati ya Kiislamu nchini Bahrain, kuhusu maamuzi mbalimbali ya hivi karibuni yaliyopitishwa na utawala wa Al Khalifa nchini humo.

Ifuatayo ni matini kamili ya tamko hilo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

﴿إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّهِ ۚ أَمَرَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ﴾

“Hukumu haimilikiwi na yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu. Ameamuru kwamba msimuabudu yeyote isipokuwa Yeye. Hiyo ndiyo dini iliyonyooka, lakini watu wengi hawajui.”

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, ambaye ni Wake uumbaji na mamlaka ya kuendesha mambo yote. Rehema na amani zimshukie Mtume Wake aliyetumwa, Muhammad (s.a.w.w.), pamoja na kizazi chake kitakatifu na kilichotakaswa.

Ama baada ya hayo:
Tunasimama kuunga mkono tamko lililotolewa na Ayatullah Sheikh Isa Ahmad Qassim mnamo tarehe 22 Rabiul Thani, mwaka 1448 Hijria, kuhusu maamuzi kadhaa yaliyofanywa nchini Bahrain.

Tumelitambua tamko hilo kuwa ni neno la haki lililotokana na utambuzi wa kina wa mwanazuoni wa fiqhi na muumini. Aidha, tamko hilo linaeleza kile ambacho dini ya haki inakihukumu, badala ya kile kinachoamriwa na hesabu za kisiasa na maslahi ya kidunia.

Kwa msingi huo, tunatangaza uungaji mkono wetu kamili kwa yote yaliyomo katika tamko hilo, na tunasimama nyuma yake katika safu moja yenye umoja.

Tawhidi si tamko linalotamkwa kwa ndimi pekee huku ukweli wake ukikosa athari katika maisha halisi. Bali, ni ahadi iliyopo kati ya waja na Mola wao, ambayo inahitaji kwamba hakuna mtu anayepaswa kutiiwa kwa namna inayopingana na amri ya Mwenyezi Mungu, wala hakuna sheria inayopaswa kutangulizwa mbele ya Sheria Yake.

Mtu yeyote anayekiri Umola na Uungu wa Mwenyezi Mungu, kwa hakika anakiri pia haki Yake ya kuweka sheria. Na yeyote anayeshindana Naye katika haki hiyo, kwa hakika anashindana Naye katika jambo ambalo ni maalumu Kwake pekee.

﴿أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ﴾

“Fahamuni! Uumbaji na mamlaka ya kuendesha mambo yote ni Vyake pekee.”

Kwa hiyo, uamuzi wowote uliowekwa na mwanadamu unaokinzana na mojawapo ya hukumu za Mwenyezi Mungu, unakataliwa katika mizani ya imani. Uamuzi huo haupati uhalali kwa sababu tu umetolewa na mwenye mamlaka, wala hauwezi kuifunga dhamiri ya muumini kwa kumlazimisha kufanya jambo linalopingana na amri ya Mola wake.

Msimamo huu si uadui wa kisiasa, wala haulengi kupata faida yoyote ya kidunia. Bali, ni uaminifu kwa neno ambalo mbingu na ardhi vimesimama juu yake; neno ambalo halitavunjwa wala halitavunjika kamwe.

﴿وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّهِ حُكْمًا لِقَوْمٍ يُوقِنُونَ﴾

“Na ni nani aliye bora zaidi kuliko Mwenyezi Mungu katika kutoa hukumu kwa watu wenye yakini?”

Kwa msingi huo, tunawaomba waumini wote kulisimamisha neno la Tawhidi, Laa ilaaha illa Allah (Hakuna mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu), kuwa kaulimbiu ya pamoja inayoonesha msimamo wao wa umoja dhidi ya maamuzi haya. Hii ni kwa sababu neno hilo ni jibu lisiloacha nafasi ya jibu jingine baada yake.

Vilevile, tunatoa wito wa kulisambaza neno hili tukufu kupitia mitandao yote ya kijamii na kila mimbari inayopatikana, kwa kutumia njia zote zinazokubalika kisheria na kwa namna ya amani yenye ufahamu na utambuzi, ili kueleza kutokubaliana na maamuzi hayo na kuyapinga.

Tunaitaka mamlaka tawala nchini Bahrain kuyapitia upya maamuzi hayo na kuyabatilisha, kwa sababu Muislamu hatakiwi kutanguliza matakwa ya kiumbe mbele ya matakwa ya Muumba wake. Hili ni jambo lisilowezekana na ambalo hakuna muumini anayeweza kulitekeleza.

Katika Hadithi Qudsi imeelezwa:

«كلمة لا إله إلا الله حصني، فمن دخل حصني أمن من عذابي»

“Neno la Laa ilaaha illa Allah ni ngome Yangu, basi, yeyote atakayeingia katika ngome Yangu atakuwa salama kutokana na adhabu Yangu.”

Basi, na ngome hii iwe mahali petu pa kujikinga, na neno hili liwe bendera yetu.

﴿وَاللَّهُ غَالِبٌ عَلَى أَمْرِهِ وَهُوَ حَسْبُنَا وَنِعْمَ الْوَكِيلُ﴾

“Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kushinda katika jambo Lake, naye anatutosha na ni Mbora wa kutegemewa.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha