Alhamisi 26 Novemba 2026 - 15:30
Utawala wa Saudi Arabia katika njia ya kuelekea kuanguka; gharama kubwa za kuichezea dini

Hawza/ Utawala ambao kwa miaka mingi umejiegemeza katika nafasi ya kidini ya miji mitakatifu ya Makka na Madina, na kujitambulisha kuwa kinara wa Uislamu, kwa sasa umenaswa katika mkanganyiko mkubwa kati ya madai yake ya kidini na mwenendo wake katika nyanja za kiutamaduni, kijamii na kisiasa; mkanganyiko ambao sasa unatishia misingi ya uhalali wa utawala na uhai wa familia ya kifalme ya Aal Saud.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, utawala wa Saudi Arabia unajitambulisha kuwa mtetezi wa Uislamu na mlinzi wa maeneo matakatifu ya Kiislamu, ilhali kwa mujibu wa wakosoaji, sera zake za kuingilia mambo ya nchi nyingine, ukandamizaji wa ndani na matumizi ya dini kama chombo cha kisiasa vimeufikisha utawala huo katika kukabiliwa na migogoro mikubwa ya ndani na nje ya nchi; migogoro ambayo inaweza kuhatarisha mustakabali wa familia inayotawala.

Mizozo ya kihistoria baina ya Saudi Arabia na Yemen imeendelea tangu zamani hadi sasa. Katika miaka ya mwanzo ya kuanzishwa utawala wa Saudi Arabia, jitihada za kuitawala Rasi ya Arabia zilisababisha mapigano na Yemen kuhusu eneo la Asir. Wakati wa vita hivyo, majeshi ya Saudi Arabia yalilikalia kwa mabavu eneo la Hodeidah, na Imam Yahya alilazimika kujiondoa katika eneo la Asir. Hatimaye, kwa kusainiwa  Mkataba wa Taif mwaka 1934, maeneo ya Jizan, Najran na Asir yalikabidhiwa kwa utawala wa Saudi Arabia kwa kipindi cha miaka 30.

Uingiliaji huo haukuishia hapo. Utawala wa Saudi Arabia uliingilia migogoro ya ndani ya Yemen katika miaka ya 1948 na 1955 kwa lengo la kuiunga mkono familia ya Hamiduddin. Baada ya kutokea Mapinduzi ya Septemba mwaka 1962, utawala huo uliendelea kuiunga mkono familia hiyo kifedha na kijeshi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kambi za mafunzo katika miji ya Najran na Jizan, kwa lengo la kukabiliana na harakati za kimapinduzi nchini Yemen.

Miongoni mwa hoja kuu zinazotolewa katika kuukosoa utawala wa Saudi Arabia ni matumizi ya dini kama chombo cha kuhifadhi madaraka na kudhibiti jamii. Tangu kuanzishwa kwake, utawala huo umeifanya dini kuwa nguzo kuu ya muundo wake wa kisiasa. Kwa kujiegemeza katika uwepo wa miji miwili mitakatifu ya Makka na Madina, umekuwa ukijitambulisha daima kuwa mlinzi wa Uislamu katika ulimwengu wa Kiarabu na nchi za Kiislamu. Hata hivyo, wakosoaji wanaamini kuwa ufisadi katika muundo wa madaraka na sera za pande mbili za utawala huo vimeweka pengo lililo wazi baina ya madai yake ya kidini na matendo yake halisi.

Mkanganyiko huu unazidi kudhihirika pale ambapo, kwa upande mmoja, utawala wa Saudi Arabia unasisitiza utambulisho wake wa Kiislamu, lakini kwa upande mwingine unafungua milango ya nchi kwa programu za utalii na burudani ambazo zinachukuliwa kuwa zinakinzana na misingi ya kidini ambayo utawala huo unadai kuisimamia. Kwa mujibu wa mwandishi, sera hizi zinazokinzana zimeifanya jamii ikabiliwe na migawanyiko mikubwa zaidi ya kimawazo na kijamii.

Katika nyanja ya ndani, familia inayotawala pia inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Kwa upande mmoja, makundi ya Kiislamu yanataka kufanyika mabadiliko makubwa zaidi ya kisiasa, na kwa upande mwingine, makundi ya kitaifa pamoja na wapinzani wa utawala wanataka kukomesha ukiritimba wa madaraka unaofanywa na familia ya kifalme. Katika mazingira kama haya, ukandamizaji wa wapinzani, kuwekewa vikwazo uhuru wa kujieleza na matumizi ya nguvu dhidi ya wakosoaji vimeongeza wigo wa kutoridhika miongoni mwa wananchi.

Katika muktadha huu, utegemezi wa utawala wa Saudi Arabia kwa nchi za Magharibi, hususan Marekani na utawala wa Kizayuni, pia ni miongoni mwa hoja nyingine zinazoukabili kwa ukosoaji. Mwelekeo huu, sambamba na uingiliaji wake katika masuala ya kikanda na migogoro ya kidiplomasia na nchi mbalimbali, umeifanya nafasi ya Saudi Arabia ikabiliwe na changamoto.

Hata uwezekano wa kuongezeka kwa migogoro ya ndani na kutokea kwa makabiliano baina ya majeshi na familia inayotawala, pamoja na kuondolewa kwake madarakani na kulazimishwa kwenda uhamishoni, umetajwa kuwa miongoni mwa matukio yanayoweza kutokea.

Katika hitimisho la uchambuzi huu, imesisitizwa kuwa; utawala wa Saudi Arabia, kutokana na vita vyake vya uharibifu dhidi ya Yemen, ukandamizaji wa ndani, matumizi ya kisiasa ya dini na kuunga mkono sera za nchi za Magharibi, unakabiliwa na mkusanyiko wa migogoro mbalimbali iliyojikusanya kwa muda mrefu. Kuendelea na mwelekeo huu kunaweza kuigharimu familia inayotawala gharama kubwa. Kwa mtazamo huu, mustakabali wa utawala wa Saudi Arabia unategemea zaidi kubadili sera zake za ndani na za kikanda, pamoja na kukomesha mwenendo wake wa kidikteta.

Chanzo: September26 – Yemen.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha