Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza Arafi alitoa kauli hiyo alipokutana na Dkt. Mehdi Amiri Isfahani, Naibu wa Masuala ya Kijamii na Kuzuia Uhalifu katika Mamlaka ya Mahakama.
Katika mkutano huo, Ayatullah Arafi alianza kwa kutoa salamu za rambirambi kufuatia kumbukumbu ya siku za kuuawa kishahidi Bibi Fatimah Zahraa (sa), kisha akatoa shukrani kwa ripoti iliyowasilishwa kuhusu shughuli zilizotekelezwa na vitengo mbalimbali vya mfumo wa mahakama.
Alieleza kuwa Hawza ni taasisi yenye jukumu la kudai uwajibikaji pamoja na kutoa majibu na kuwajibika kwa jamii. Aidha, alisema kuna fursa ya kupanua ushirikiano kati ya Hawza na Mamlaka ya Mahakama katika nyanja za elimu, mafunzo ya majaji, tafiti, ulinganiaji wa dini na uzalishaji wa misingi ya kitaaluma na kifiqhi kwa ajili ya mfumo mpya wa utawala wa mahakama, kupitia Ofisi ya Fiqhi ya Kisasa ya Hawza za kielimu.
Kusisitiza matumizi ya fursa ya mpango wa kuimarisha vitongoji kwa kuzingatia misikiti
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, aliutaja mpango wa kuimarisha vitongoji kwa kuzingatia misikiti kuwa miongoni mwa fursa muhimu za kupunguza madhara ya kijamii na kuzuia uhalifu. Aliongeza kuwa Mamlaka ya Mahakama inaweza kuwasiliana na Makao Makuu ya Kitaifa ya Msikiti pamoja na sekretarieti yake ili kufanikisha jambo hilo.
Mjumbe wa Baraza la Walinzi, katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake, alisisitiza pia kuwa Mpango wa Saba wa Maendeleo una fursa nzuri ya kuimarisha mkabala wa kuzuia matatizo kabla hayajatokea. Hivyo, fursa hiyo inapaswa kutambuliwa ipasavyo na kutumiwa katika masuala ya kijamii na kuzuia uhalifu.
Umuhimu wa kubuni dhana, kuunda istilahi na kuanzisha mtazamo mpya wa utawala wa mahakama
Miongoni mwa mapendekezo mengine ya Ayatullah Arafi kwa Naibu wa Masuala ya Kijamii na Kuzuia Uhalifu katika Mamlaka ya Mahakama ni umuhimu wa kubuni dhana, kuunda lugha na istilahi maalumu, pamoja na kuanzisha mtazamo mpya wa utawala wa masuala ya mahakama. Kuhusiana na jambo hilo, alisema kuwa hatua hii inahitaji msingi imara wa kitaaluma na kifiqhi, na kwamba Hawza inaweza kusaidia katika kubuni dhana na misingi hiyo.
Aidha, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, alisisitiza umuhimu wa kupanua mafunzo maalumu ya masuala ya mahakama na kutumia uwezo uliopo katika Fiqhi ya Kisasa pamoja na Fiqhi ya Akili Unde (Artificial Intelligence).
Pia alikumbusha kuwa Mamlaka ya Mahakama inapaswa kushirikiana na taasisi za kijamii kwa mfumo wa mnyororo wa ushirikiano na kwa mtazamo unaozingatia muunganiko wa taasisi hizo kama mfumo mmoja.
Mapendekezo na hoja 10 za kimkakati
Katika kuendeleza mazungumzo yake, Ayatullah Arafi aliwasilisha mapendekezo na hoja kumi za kimkakati zinazolenga kuimarisha na kuboresha utawala wa mahakama, kuzuia uhalifu, kupunguza madhara ya kijamii na kupanua ushirikiano kati ya Hawza na Mamlaka ya Mahakama, kama ifuatavyo:
1. Umuhimu wa tafiti na uchunguzi
- Mipango na hatua zote zinazochukuliwa zinapaswa kutegemea tafiti za msingi na tafiti zinazolenga matumizi ya vitendo.
- Upimaji wa maoni ya wananchi na uchambuzi sahihi wa takwimu za kijamii una umuhimu mkubwa.
- Kufanya maamuzi bila kuwa na ufahamu wa kina na bila kufanya tafiti ni sawa na kutembea katika njia isiyo sahihi, kwa mujibu wa mafundisho yaliyopokelewa katika riwaya.
2. Kutambua sababu na mizizi ya matatizo ya kijamii
- Ili kutatua matatizo ya kijamii, ni lazima kutambua sababu zake halisi na kuzipanga kulingana na vipaumbele vyake.
- Kuhusu suala la kuhama kwa wasomi na wataalamu wenye vipaji, tafiti zinaonesha kuwa sababu kuu zimepangwa kwa mtiririko ufuatao: hadhi na heshima katika jamii, hali ya maisha na kipato, masuala ya kiutamaduni na hatimaye masuala ya kisiasa.
- Kuzitambua sababu halisi za matatizo hubadilisha namna ya kukabiliana na matukio hayo.
3. Matumizi ya teknolojia
- Teknolojia mpya zinaweza kuwa tishio na wakati huohuo kuwa fursa.
- Kuna umuhimu wa kubadilisha tisho linavyotokana na teknolojia kuwa fursa za kuzuia matatizo kabla hayajatokea.
4. Ushirikiano wa kimfumo na taasisi za kijamii
- Mamlaka ya Mahakama inapaswa kushirikiana na taasisi za kijamii kwa mfumo wa mnyororo wa ushirikiano na kwa mtazamo unaozingatia muunganiko wa taasisi hizo kama mfumo mmoja.
- Taasisi muhimu katika ushirikiano huo ni:
- Hawza na wanazuoni wa dini.
- Vyuo vikuu.
- Elimu na malezi.
- Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
- Familia.
- Hawza inapaswa kuwa taasisi inayodai uwajibikaji na wakati huohuo inayowajibika kutoa majibu.
- Kuna umuhimu wa kutoa taarifa kwa mtandao mpana wa wanahawza, wahubiri na wanaharakati wa masuala ya ulinganiaji wa dini.
- Pia alielekeza kwenye matumizi ya fursa zilizopo kama vile Mradi wa Amin, shule za Amin na mitandao ya ulinganiaji wa dini.
5. Kuzingatia rasilimali watu katika Mamlaka ya Mahakama
- Ubora wa uelewa wa masuala ya kijamii, mtazamo wa kuzuia matatizo kabla hayajatokea, pamoja na haiba na mwenendo wa wakuu wa mahakama na waendesha mashtaka vina athari kubwa.
- Mtazamo na falsafa ya Naibu wa Masuala ya Kijamii vinapaswa kujengeka na kuwa sehemu ya utamaduni wa rasilimali watu katika Mamlaka ya Mahakama. Jambo hili linahitaji mpango mpana, mafunzo, ujenzi wa mtazamo wa pamoja na uvumilivu katika kukabiliana na upinzani unaoweza kujitokeza ndani ya taasisi.
6. Kutumia fursa zilizopo katika Mpango wa Saba wa Maendeleo
- Mpango wa Saba wa Maendeleo una fursa nzuri ya kuimarisha mkabala wa kuzuia matatizo kabla hayajatokea. Fursa hii inapaswa kutambuliwa ipasavyo na kutumiwa katika masuala ya kijamii na kuzuia uhalifu.
7. Kuimarisha vitongoji na kuweka misikiti kuwa kitovu cha shughuli
- Mpango wa kuimarisha vitongoji kwa kuzingatia misikiti unaendelea kutekelezwa na Serikali. Mamlaka ya Mahakama inaweza kuwasiliana na Makao Makuu ya Kitaifa ya Msikiti pamoja na sekretarieti yake ili kujadili na kufanikisha mpango huo.
- Mtandao wa vitongoji na misikiti unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza madhara ya kijamii na kuzuia uhalifu.
8. Suala la magereza
- Gereza linaweza kuwa na athari mbili: linaweza kuzuia uhalifu, lakini pia linaweza kuwa mazingira yanayochochea na kueneza tabia za uhalifu.
- Kuna umuhimu wa kuandaa mkakati mpana wa kupunguza athari hasi zinazotokana na magereza.
- Pia ni muhimu kuzingatia njia na suluhisho zinazokubalika kwa mujibu wa Sharia na sheria, ambazo zinaweza pia kukubaliwa na Baraza la Walinzi.
9. Ushirikiano wa Hawza na Mamlaka ya Mahakama katika elimu, tafiti na ulinganiaji wa dini
- Kuna fursa ya kushirikiana katika nyanja za elimu, tafiti na ulinganiaji wa dini.
- Kuna umuhimu wa kufafanua na kuweka bayana ujuzi maalumu wa masuala ya sheria na mahakama ambao wanafunzi wa Hawza wanapaswa kuupata.
- Ni muhimu kutumia uwezo uliopo katika Fiqhi ya Kisasa, ikiwemo mijadala ya Fiqhi ya Akili Unde.
- Kutoa mafunzo kwa majaji na kuimarisha ujuzi wao wa masuala ya mahakama ni miongoni mwa maeneo muhimu ya ushirikiano.
10. Kubuni dhana na kuzalisha istilahi za utawala wa mahakama
- Kuna haja ya kubuni dhana, kuunda lugha na istilahi maalumu, pamoja na kuanzisha mtazamo mpya wa utawala wa masuala ya mahakama.
- Hatua hii inahitaji msingi imara wa kitaaluma na kifiqhi. Hawza inaweza kutoa mchango katika kubuni dhana na misingi hiyo.
Mapendekezo 10 ya utekelezaji
Katika kuendeleza mazungumzo yake, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran alisisitiza umuhimu wa kupanua ushirikiano kati ya Hawza na Mamlaka ya Mahakama. Aidha, aliwasilisha mapendekezo ya kiutendaji kwa ajili ya kutekeleza na kufuatilia mikakati hiyo kumi, kama ifuatavyo:
1. Kuandaa hati ya pamoja ya ushirikiano kati ya Hawza na Mamlaka ya Mahakama, chini ya makubaliano ya ushirikiano yaliyopo, huku maeneo ya ushirikiano yakifafanuliwa kwa usahihi.
2. Kuratibu na Ofisi ya Fiqhi ya Kisasa kwa ajili ya kuzalisha misingi ya kitaaluma na kifiqhi ya utawala mpya wa mahakama.
3. Kuwasiliana na Kituo cha Mawasiliano cha Hawza na Mfumo wa Kiislamu kwa ajili ya kufuatilia maeneo ya ushirikiano.
4. Kuwasiliana na kitengo cha ulinganiaji wa dini cha Hawza.
5. Kuandaa mpango mpana wa rasilimali watu katika Mamlaka ya Mahakama kwa kuzingatia mtazamo wa kijamii na kuzuia uhalifu.
6. Kuratibu na Makao Makuu ya Kitaifa ya Msikiti na kuchunguza mpango wa kuimarisha vitongoji kwa kuzingatia vitongoji na misikiti.
7. Kufanya uchunguzi mpana kuhusu suala la magereza na kuwasilisha suluhisho zinazokubalika kwa mujibu wa Sharia na sheria.
8. Kuimarisha tafiti, uchunguzi na upimaji wa maoni ya wananchi katika Naibu wa Masuala ya Kijamii na Kuzuia Uhalifu.
9. Kupanua mafunzo maalumu ya masuala ya mahakama na kutumia uwezo uliopo katika Fiqhi ya Kisasa pamoja na Fiqhi ya Akili Unde.
10. Kuendesha mikutano ya mara kwa mara kati ya Hawza na Mamlaka ya Mahakama, pamoja na kuwasilisha ripoti za maendeleo ya utekelezaji.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Dkt. Mehdi Amiri Isfahani, Naibu wa Masuala ya Kijamii na Kuzuia Uhalifu katika Mamlaka ya Mahakama, alitoa salamu za rambirambi kufuatia siku za huzuni za kuuawa kishahidi Bibi Fatimah Zahraa (sa).
Pia alisisitiza umuhimu wa nchi kuvuka changamoto zake za kihistoria kwa mafanikio, heshima na nguvu. Baada ya hapo, aliwasilisha ripoti kuhusu mipango na shughuli zinazotekelezwa na naibu huyo.
Maoni yako