Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Baqir Jabr al-Zubaidi, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani wa Iraq, amesisitiza kuwa wapiganaji kutoka makundi ya kigaidi ya Syria wamehamishiwa nchini Yemen, na akaashiria kuwepo kwa daraja la angani kwa ajili ya kuwahamisha wapiganaji hao ili kushiriki katika mapigano dhidi ya Harakati ya Ansarullah.
Al-Zubaidi alisema katika chapisho moja kwamba: “Daraja la angani limewahamisha magaidi kutoka Syria kwenda Yemen ili kukabiliana na Ansarullah. Hatua hii imechukuliwa baada ya kushindwa kwa operesheni za kijeshi za Ghuba katika kukabiliana na kundi hili.”
Aliongeza kuwa hatua hiyo imeambatana na kampeni kubwa ya vyombo vya habari ya kuzungumzia kuhusu kuikomboa Yemen.
Aliongeza kusema: “Kuingia kwa Abu Muhammad al-Jolani, kiongozi wa Tahrir al-Sham, katika vita hivi ni hatua iliyoshindwa, lakini kwake ni jambo muhimu, kwa sababu ni jaribio la kuwashughulisha Wasyria na migogoro ya nje ili kuwafanya wasitambue migogoro yao ya ndani.” Alieleza kuwa hatua hiyo pia huenda ikalenga kuwaondoa baadhi ya makamanda ambao wanahesabiwa kuwa tishio kwa nafasi yake.
Al-Zubaidi alizungumzia kiwango cha Uturuki kukubaliana na hatua hii, pamoja na iwapo hatua hiyo ni sehemu ya makubaliano ya Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan, akisema: “Huenda maslahi ya Ankara yakawa yanaelekea katika kuimarisha kila upande unaokabiliana na utawala wa Israel, na miongoni mwa pande hizo, Ansarullah iko mstari wa mbele.”
Alisisitiza kuwa huenda al-Jolani amelazimika kuingia katika makabiliano haya kutokana na shinikizo linalohusiana na ufadhili wa Ghuba kwa Syria, aliongeza kusema: “Uamuzi wa Syria kwa sasa umehusishwa na pande kadhaa za kikanda na kimataifa.”
Al-Zubaidi alionya: “Kuendelea na njia hii kunaweza kusababisha kufunguliwa kwa medani mpya za mapigano, na kumuingiza al-Jolani katika vita ni hatua ndani ya mradi mpana zaidi, ambao kupitia huo amehamishwa kutoka kuwa mtu anayetafutwa hadi katika nafasi ya uongozi wa mamlaka nchini Syria.”
Hapo awali, chanzo kimoja cha Syria kililiambia Shirika la Habari la Al-Maalouma kwamba; kuna harakati na mikutano ya siri inayohusiana na uratibu wa kuwahamisha wapiganaji wa Syria kwenda Yemen. Chanzo hicho kilieleza kuwa operesheni hiyo inafanywa kimakundi na kwa mipango inayoongozwa na Marekani, Uturuki na Saudi Arabia.
Maoni yako