Alhamisi 17 Septemba 2026 - 02:00
Ghaza ni mtihani mkubwa kwa wanaodai kutetea demokrasia duniani

Hawza/ Hujatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sa'jid Ali Naqvi, katika ujumbe wake wa kuikosoa jumuiya ya kimataifa kwa kunyamazia jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza, amesisitiza kwamba: Siku ya Kimataifa ya Demokrasia itakuwa na maana na uhalali wa kweli pale ambapo haki za mataifa, uhuru wa kujieleza na matakwa ya wananchi vitaheshimiwa kwa vitendo, na demokrasia haitageuzwa kuwa chombo cha kutimiza maslahi ya madola yenye nguvu duniani.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan, katika ujumbe wake kwa mnasaba wa tarehe 15 Septemba, ambayo ni “Siku ya Kimataifa ya Demokrasia”, amesisitiza kwamba; lengo la kuifanya siku hii kuwa ya kimataifa ni kuiunga mkono demokrasia katika ngazi ya kimataifa na kufanya juhudi za kuimarisha na kueneza mifumo ya kidemokrasia katika nchi mbalimbali; hata hivyo, utendaji wa jumuiya ya kimataifa kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu, hususan katika eneo la Asia Magharibi, unahitaji kufanyiwa mapitio makubwa.

Akirejelea jinai na majanga ya kibinadamu huko Ghaza pamoja na kuendelea kwa mashambulizi na ukiukaji wa haki za wananchi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, amesema: Leo, wakati Siku ya Kimataifa ya Demokrasia inaadhimishwa katika maeneo mbalimbali duniani, mbele ya macho ya Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa, wananchi wa Ghaza wako chini ya mashambulizi na shinikizo kali zaidi, huku katika Ukingo wa Magharibi ukiukaji wa haki na dhuluma dhidi ya wananchi ukiendelea; na katika Asia Kusini pia, matukio mengi ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu yanakabiliwa na kupuuzwa.

Mwanazuoni huyo wa Pakistan ameongeza: Siku ya Kimataifa ya Demokrasia iliwekwa kwa lengo la kuiunga mkono misingi ya demokrasia katika uwanja wa kimataifa na kuchukua hatua zinazohitajika kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya kidemokrasia katika nchi mbalimbali, na imekuwa ikipewa umuhimu tangu mwaka 2008; lakini sasa inapaswa kuchunguzwa ni kwa kiwango gani malengo haya yametekelezwa kwa vitendo na jumuiya ya kimataifa imekuwa ikizingatia kwa kiwango gani misingi halisi ya demokrasia.

Akikosoa utendaji wa madola yenye nguvu duniani, amesisitiza: Uzoefu umeonesha kwamba katika matukio mengi, kwa ajili ya kulinda maslahi ya kisiasa na kiuchumi, badala ya kuiunga mkono demokrasia, serikali za kidikteta zimekuwa zikiungwa mkono. Katika baadhi ya nchi pia, misingi kama utawala wa sheria na katiba, nafasi na kipaumbele cha bunge, pamoja na kuheshimiwa kwa kura za wananchi, havitekelezwi kwa kiwango kinachopaswa, wakati kwa jina la demokrasia maslahi maalumu yamekuwa yakilindwa, masuala mengi ya msingi, ikiwemo haki za msingi za binadamu na uhuru wa kujieleza, bado yanakabiliwa na changamoto kubwa.

Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia Pakistan ameendelea kusema: Kuundwa mazingira ya hofu na vitisho katika maeneo mbalimbali duniani, kukanyagwa  haki za msingi za wananchi na kuwekwa vikwazo dhidi ya vyombo vya habari, hakulingani na misingi na roho ya demokrasia. Tabia ya kihalifu ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza, huku wanaodai kuiunga mkono demokrasia wakiwa kimya mbele yake, ni pigo lililo wazi kwa uhalali wa kauli mbiu za kutetea demokrasia; na ukimya wa madola yenye nguvu duniani mbele ya jinai hizi pia unatia wasiwasi mkubwa.

Mwisho, akirejelea maana halisi ya demokrasia, amesema: Demokrasia katika maana yake ya kweli ni “utawala wa watu, kwa watu na kwa ajili ya watu”. Ikiwa msingi huu utatekelezwa kwa uhalisia na vitendo, lengo lake kuu litakuwa kuwatumikia wananchi na kuheshimu kura na matakwa yao. Katika mfumo wa kidemokrasia, mitazamo na maoni ya matabaka yote ya jamii yanapaswa kuzingatiwa; na Uislamu pia, kwa kusisitiza mashauriano na kunufaika na mitazamo mbalimbali, unasisitiza umuhimu wa ushiriki na maoni ya wananchi katika kusimamia mambo ya jamii.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha