Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Muhammad Al-Farah, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah, katika ujumbe aliouchapisha kwenye ukurasa wake binafsi katika jukwaa la «X», alieleza kwamba; wananchi wa Yemen hawakuchagua vita wala hawakuvifuata, bali walilazimishwa kutokana na mashambulizi na mzingiro waliowekewa.
Alisisitiza kwamba; Wayaemen walijikuta mbele ya machaguo mawili: ima kujisalimisha mbele ya kifo kinachosababishwa na njaa na mzingiro, au kupigana kwa ajili ya uhuru, mamlaka ya kitaifa na heshima yao.
Al-Farah alisema: “Mashambulizi ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen yalianza mwaka 2015 (1394 kwa kalenda ya Shamsi), katika mazingira ya udhaifu na mgawanyiko wa ndani. Saudi Arabia ilitumia hali hiyo kuanzisha vita vikubwa vya uchokozi dhidi ya wananchi wa Yemen, wakati makundi ya kisiasa nchini Yemen yalikuwa yakifanya mazungumzo kwa lengo la kufikia makubaliano na yalikuwa yameanza kuchukua hatua kuelekea kuanzishwa kwa amani na ushirikiano.”
Aliongeza kuwa; kutangazwa vita kutoka Washington lilikuwa tukio la kihistoria na la hatima lililofichua asili ya uamuzi wa Saudi Arabia pamoja na uungaji mkono wa Marekani uliokuwa ukiambatana nao. Alisema mashambulizi hayo tangu mwanzo yalikuwa ya kiwango kikubwa, yakihusisha nyanja zote za maisha nchini Yemen, huku miundombinu ya kiraia, maeneo ya makazi na hata makaburi yakiwa hayajaachwa salama.
Mwanachama huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah alisisitiza kwamba vita vya uchokozi viliendelea kwa miaka mingi, sambamba na mashambulizi makali ya anga, kuwatumia wanajeshi wa ndani kupigana katika maeneo mbalimbali ya mapambano na kuweka mzingiro mpana uliolenga chakula, dawa, mafuta, matibabu na mahitaji ya msingi ya wananchi, jambo lililozidisha mateso ya watu wa Yemen.
Kwa upande mwingine, alisisitiza kwamba; wananchi wa Yemen, licha ya kuwa na uwezo mdogo ukilinganishwa na ukubwa wa vikosi vilivyoshiriki katika vita hivyo, walikabiliana na mashambulizi na waliweza kusimama imara na kuwasababishia maadui hasara mfululizo. Wayaemen, licha ya kujitolea kwao na kutoa kafara kubwa, hawakukubali kusalimu amri wala kunyenyekea.
Aidha, alisema Sana’a ilipokea kwa mtazamo chanya miito ya amani, lakini upande wa pili haukuwa ukitafuta amani ya kweli; badala yake, ulikuwa ukijaribu kulazimisha kujisalimisha na kutumia kujishughulisha kwa Yemen katika kuiunga mkono Palestina na wananchi wa Ghaza pamoja na Muqawama nchini Lebanon, ili kutekeleza mipango ya kijeshi na kiusalama na kuongeza shinikizo za kiuchumi na vyombo vya habari.
Aliongeza kwamba Riyadh, sambamba na hilo, ilifanya juhudi za kuongeza maradufu shinikizo za kiuchumi na kuanzisha kampeni za vyombo vya habari zilizolenga safu ya ndani, huku ikikwepa kutekeleza ahadi zinazohusiana na amani na kuwasukuma upande wa Yemen kuelekea katika uwanja wa kisiasa, wakati maamuzi ya kijeshi na kisiasa yakiendelea kuwa mikononi mwa pande za nje.
Alifafanua kwamba; hali ilifikia viwango vya hatari, kiasi kwamba ujumbe wa Yemen uliokuwa Tehran kwa ajili ya kutoa pole ulizuiwa kurejea nchini, huku uwanja wa ndege wa Sana’a ukishambuliwa kwa mabomu na ndege ya abiria iliyokuwa imebeba mamia ya abiria kuwekwa katika hatari.
Al-Farah alivitaja vitendo hivyo kuwa ni ukiukaji wa mamlaka ya Yemen na kusisitiza kwamba vinaonesha kuendelea kwa sera ya uadui dhidi ya Yemen.
Mjumbe huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah alisema kupita kwa miaka hakujabadilisha kiini cha mlingano huo, kwa sababu wananchi wa Yemen bado wako mbele ya chaguo la kutetea mamlaka yao, uhuru na heshima yao au kukubali mzingiro unaoendelea na mashambulizi yasiyokoma.
Alisema Sana’a ilikuwa imetoa tahadhari mara kadhaa kwa upande wa Saudi Arabia, ikiwemo onyo lililotolewa katika “Ijumaa ya Onyo”, lakini tahadhari hizo hazokujibiwa.
Alieleza kwamba; harakati za vikosi vya Yemen vilivyo na silaha, katika mfumo wa juhudi za kuondoa mzingiro na kusitisha mashambulizi, zinaendana na malengo na madai halali yanayolingana na sheria, mikataba na desturi za kimataifa. Alisisitiza kuwa Yemen haikuelekea kwenye makabiliano kwa sababu ya kupenda vita, bali ilifanya hivyo kutokana na kuendelea mashambulizi na mzingiro.
Al-Farah aliishutumu Saudi Arabia kwa kuwatumia wanamgambo na vikosi vya mamluki vinavyoiunga mkono ndani ya Yemen na kuwaleta katika makabiliano. Alisema wanamgambo hao waliingia vitani kwa niaba ya adui wa Saudi Arabia na kushiriki katika operesheni za kijeshi dhidi ya wananchi wa Yemen kwa malipo ya msaada na fedha walizokuwa wakipokea.
Alibainisha kwamba; mapambano ya ardhini yalishuhudia mabadiliko makubwa ya kijeshi katika maeneo kadhaa ya mapambano, kabla ya Jeshi la Anga la Saudi Arabia kurejea katika kufanya mashambulizi kwa kutumia ndege za kivita za aina mbalimbali na kulenga mikoa na maeneo kadhaa nchini Yemen.
Mjumb huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah alirejelea mashambulizi yaliyolenga maeneo ya Al-Barah, Hays na Kituo cha Marekebisho na Malezi cha Al-Hazm katika mkoa wa Al-Jawf, na kuongeza kwamba kuendelea mashambulizi hakukuwalazimisha wananchi wa Yemen kurudi nyuma, bali kulisababisha kuongezeka kwa majibu ya kijeshi.
Alisema Vikosi vya Yemen vilivyo na silaha vilifanya operesheni ya kulenga vituo vya mafuta vya Saudi Arabia kama sehemu ya kutoa onyo, lakini upande wa Saudi Arabia haukuuchukulia ujumbe huo kuwa tahadhari makubwa.
Al-Farah alisema operesheni za makombora na anga za Yemen zinaendelea kupanuka kwa upande wa eneo linalofikiwa na pia kuongezeka kwa nguvu zake. Alisema Vikosi vya Yemen vilivyo na silaha vina uwezo wa kijeshi unaoviwezesha kuendelea kukabiliana na ukaliaji na utawala wa mabavu hadi kufikia uhuru na mamlaka kamili.
Alisema Saudi Arabia ina chaguo lililo wazi mbele yake: kusitisha mashambulizi, kumaliza mzingiro na kutoingilia mambo ya Yemen, au kuendelea katika njia ya kuchochea mvutano.
Alionya kwamba; kuendelea na uzoefu wa kijeshi hakutaifikisha Riyadh kwenye matokeo inayoyatafuta, na kwamba Saudi Arabia, baada ya miaka ya mashambulizi na mzingiro, inakabiliwa na hali tofauti na ile iliyokuwepo mwanzoni mwa mashambulizi.
Alisema muungano ambao Riyadh iliwaongoza katika miaka iliyopita haukuweza kufikia malengo yake, na kwamba kuendelea kwa makabiliano katika mazingira ya sasa kutakuwa kugumu zaidi kwake.
Mjumbe huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah aliendelea kusema kwamba juhudi za utawala wa Saudi Arabia kutafuta msaada kutoka Marekani na utawala wa Kizayuni hazitabadilisha mlingano huo, kwa sababu Yemen katika makabiliano yake inamtegemea Mwenyezi Mungu pamoja na uwezo wake wa ndani.
Alisisitiza kwamba kuendelea kwa shinikizo la kijeshi hakutawafanya wananchi wa Yemen kuachana na mamlaka yao au kukubali kutawaliwa na nguvu za kigeni.
Al-Farah alisisitiza tena kwamba; Yemen imechagua njia ya uhuru, heshima na kukataa utegemezi, na kwamba kuendelea kwa mashambulizi na mzingiro hakutabadilisha chaguo hilo.
Aidha, alitoa wito kwa upande wa Saudi Arabia kuzipitia upya hesabu zake badala ya kuendelea na njia ya kijeshi ambayo, kwa mujibu wake, imethibitisha kushindwa kwake katika miaka iliyopita, na akaitaka kusitisha mashambulizi na kumaliza mzingiro.
Maoni yako