Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujatul-Islam wal-Muslimin Mohsen Qara’ati alisema hayo katika hafla ya ufunguzi wa masomo ya Taasisi ya Elimu ya Juu ya Hawzah ya Imam Mahdi (as) — Kituo Maalumu cha Mahdawiyya na Swala — iliyofanyika Jumanne jioni katika ukumbi wa kuswalia wa taasisi hiyo mjini Qom Iran. Akisisitiza umuhimu wa kuzingatia majukumu ya msingi ya Hawza na jukumu la wanafunzi wa Hawzah katika nyanja za elimu na uhubiri, alisema: Kama ambavyo watu wengi duniani hushiriki katika mojawapo ya nyanja tatu za uzalishaji, usambazaji au matumizi, ndivyo pia ilivyo katika masomo ya Hawzah; yanaweza kumwelekeza mwanadamu katika kuzalisha elimu, kusambaza maarifa ya dini, au kutumia na kutekeleza elimu za Kiislamu.
Mkuu wa Baraza la Kusimamisha Swala nchini Iran alisema kwamba masomo ya Hawzah katika kiwango chake cha juu yanaweza kuwa msingi wa uzalishaji wa elimu. Alieleza kuwa katika hatua moja, masomo ya Hawzah humfikisha mtu katika uwezo wa ijtihadi, fiqhi, utafiti na uandishi wa kazi za kielimu, na katika hali hiyo mwanafunzi wa Hawzah huwa katika nafasi ya mzalishaji wa elimu.
Kueneza maarifa ya Ahlul-Bayt (as); jukumu muhimu la wanafunzi wa Hawzah katika uhubiri
Hujatul-Islam wal-Muslimin Qara’ati aliongeza kusema: Ikiwa mwanafunzi wa Hawzah hatafikia hatua ya ijtihadi na uzalishaji wa kazi za kielimu, bado njia ya masomo ya Hawzah inaweza kuwa msingi wenye thamani wa kunufaika na kazi za kielimu zilizozalishwa na wanazuoni wakubwa, pamoja na kuhamisha na kusambaza maarifa ya Qur’ani Tukufu na Ahlul-Bayt wa Mtume Mtukufu (saww). Uhamishaji huu wa maarifa unaweza kufanyika kupitia maandishi, hutuba, kuhama kwa ajili ya kueneza dini na uhubiri; na katika hatua hii, mwanafunzi wa Hawzah hubeba jukumu la msambazaji wa elimu na maarifa ya dini.
Mwalimu huyo wa Hawzah, akitoa hoja kwa kutumia kauli ya Imam Ridhaa (as) kuhusu umuhimu wa kuwatambulisha watu maarifa ya Ahlul-Bayt (as), alisisitiza: Imam Ridhaa (as) amesema:
«فَإِنَّ النَّاسَ لَوْ عَلِمُوا مَحَاسِنَ کَلَامِنَا لَاتَّبَعُونَا»
“Kwa hakika, lau watu wangejua uzuri wa maneno yetu, wangetufuata.”
Kufahamu elimu za Kiislamu kunapaswa kupelekea matendo na mwenendo wa kidini
Mwalimu Qara’ati aliendelea kwa kuitaja hatua ya tatu kuwa ni matumizi ya kivitendo ya elimu za Kiislamu, akasema: Kufahamu elimu za Kiislamu, kwa uchache, kunapaswa kuwa msingi na mazingira ya mtu mwenyewe kuzifanyia kazi. Kwa hiyo, elimu hufikia matokeo yanayokusudiwa pale inapojitokeza pia katika maisha na mwenendo wa mwanadamu, mafanikio ya kweli ni kwa yule anayeweza kutekeleza hatua zote tatu kwa pamoja; yaani kuzalisha elimu kupitia utafiti na ijtihadi, kuchukua hatua katika njia ya kusambaza na kueneza maarifa ya Mwenyezi Mungu kupitia kalamu na mazungumzo, na pia kuwa wa kwanza katika kuyatekeleza kwa vitendo.
Mkuu wa Baraza la Kusimamisha Swala, akirejea riwaya kuhusu nafasi ya mwanazuoni mwenye kunufaisha, alisema:
«عَالِمٌ نَاطِقٌ یَنْتَفِعُ بِعِلْمِهِ»
“Mwanazuoni anapaswa kuzungumza na kuifanya elimu yake iwe na manufaa na athari.”
Kwa msingi huo, matokeo yanayotarajiwa kutoka katika Hawza yanapaswa pia kufafanuliwa katika mkondo huo; yaani elimu na maarifa yanayopelekea katika kuzalisha, kueneza na kuyafanyia kazi.
Tafaquh katika dini na uhubiri; neema ya Mwenyezi Mungu na mwendelezo wa ujumbe wa Mitume
Hujatul-Islam wal-Muslimin Qara’ati, akisisitiza umuhimu wa kutambua nafasi na umuhimu wa njia ya masomo ya Hawzah, alisema: Ikiwa mwanadamu atatambua kwamba tafaquh katika dini na kuhubiri maarifa ya Mwenyezi Mungu ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni kazi inayoendeleza ujumbe wa Mitume, atatembea katika njia hii kwa mapenzi na hamu kubwa zaidi.
Mfasiri wa Qur’ani aliongeza: Mtu anayetambua nafasi halisi ya njia hii hapaswi kuathiriwa na dhana potofu, propaganda mbaya na ulinganisho usio sahihi, kisha kubadilisha njia yake. Mwanafunzi wa Hawzah anapaswa kufahamu kwamba njia ya elimu, uhubiri na kuitumikia dini ni njia yenye thamani na yenye nafasi mbele ya Mwenyezi Mungu, na kwamba hapaswi kuiacha kwa sababu ya mitazamo isiyo sahihi au ulinganisho usio wa kweli.
Katika njia ya kuhubiri dini, mtu hapaswi kumwogopa yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu
Hujatul-Islam wal-Muslimin Qara’ati aliendelea kusisitiza umuhimu wa kusimama imara katika njia ya kuhubiri dini na kutekeleza majukumu ya Hawzah, akasema: Mafanikio ya kweli ni kwa yule ambaye katika njia hii hamwogopi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, na anatekeleza wajibu wake kwa ujasiri na ikhlasi.
Mkuu wa Baraza la Kusimamisha Swala, kuthibitisha kauli hiyo, alirejea Aya ya 39 ya Surat al-Ahzab, akasema: Mwenyezi Mungu anasema kuhusu sifa za waja Wake:
«الَّذینَ یُبَلِّغُونَ رِسالاتِ اللَّهِ وَ یَخْشَوْنَهُ وَ لا یَخْشَوْنَ أَحَداً»
“Wale wanaofikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu, wanamwogopa Yeye na hawamwogopi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu.”
Maoni yako