mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mkutano wa pili wa kimataifa wa viongozi wa dini umefanyika katika jiji la Saint Petersburg nchini Urusi. Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa dini, wanazuoni na watu mashuhuri kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Urusi na nchi mbalimbali. Kuhifadhi maadili ya Kiislamu na kidini, utu wa mwanadamu na uadilifu, umoja baina ya dini, mgogoro wa kimaadili duniani na masuala muhimu ya kimataifa, yakiwemo mauaji na uhalifu unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni huko Palestina na Gaza, ilikuwa miongoni mwa mada muhimu zilizojadiliwa katika mkutano huo.
Katika mkutano huo, Dkt. Kazem Jalali, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Urusi, na Hujjatul-Islamu wal-Muslimin Hamid Shahriyari, Katibu Mkuu wa Baraza la Kimataifa la Kuleta Ukaribu kati ya Madhehebu ya Kiislamu, walitoa hotuba na kueleza mitazamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu masuala muhimu ya dunia.
Hamid Shahriyari: Utu wa mwanadamu na uadilifu ni miongoni mwa misingi ya mfumo wa Kiislamu
Hujjatul-Islamu wal-Muslimin Hamid Shahriyari, Katibu Mkuu wa Baraza la Kimataifa la Kuleta Ukaribu baina ya Madhehebu ya Kiislamu, katika hotuba yake, huku akizungumzia migogoro ya sasa duniani, alisema: “Katika mazingira haya ya migogoro, ni muhimu kuzingatia maadili mawili ya msingi ya Uislamu, yaani utu na uadilifu.”
Aliongeza: “Utu ni thamani ya kibinadamu ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu amewajaalia wanadamu wote, na si jambo linalohusishwa na dini, madhehebu au itikadi maalumu. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’ani Tukufu:
«وَلَقَدْ کَرَّمْنَا بَنِی آدَمَ»
‘Na kwa hakika tumewatukuza wanadam.’”
Hujjatul-Islamu wal-Muslimin Shahriyari alifafanua kwamba uadilifu ni kuheshimu na kutekeleza haki za wengine, na kusema: “Uadilifu ni miongoni mwa maadili ya juu kabisa na yanayokubalika katika jamii, wakati dhuluma maana yake ni kuzikanyaga haki za wengine kupitia uchokozi na uadui.”
Kuheshimu haki za msingi za mwanadamu ni wajibu wa kila mtu
Katibu Mkuu wa Baraza la Kimataifa la Kuleta Ukaribu baina ya Madhehebu ya Kiislamu, huku akizungumzia haki za binadamu, alisema: “Kila mwanadamu ana haki zisizopingika, kama vile haki ya kuishi, kupata chakula na maji, kuishi katika ardhi yake na kuwa na uhuru, na kuheshimu haki hizi ni wajibu wa kila mtu.”
Alisisitiza: “Kumuua mwanadamu asiye na hatia, kumzingira na kumnyima chakula, maji, makazi na haki ya kuishi katika nchi yake, si jambo linaloruhusiwa kwa mtu yeyote. Hii ni misingi ya kibinadamu ambayo Qur’ani Tukufu imeisisitiza na Waislamu wana wajibu wa kuizingatia misingi hii bila kujali dini, madhehebu au mtazamo wa upande mwingine.”
Ukiukaji wa haki za Wapalestina ni mfano wa wazi wa mgogoro wa kimaadili duniani
Hujjatul-Islamu wal-Muslimin Shahriyari, akizungumzia changamoto kubwa zinazozikabili thamani za kimaadili duniani, alisema: “Leo hii haki hizo za msingi zinanyimwa taifa la Palestina.”
Aliongeza: “Haki ya kuishi ni miongoni mwa haki za msingi zaidi za mwanadamu, lakini watu wa Palestina kwa miongo kadhaa wamekuwa wakikabiliwa na dhuluma, ukandamizaji, kulazimishwa kuhama makazi na kunyimwa haki zao.”
Mzungumzaji huyo katika mkutano alisema: “Kwa uungaji mkono wa Marekani, mfumo wa utawala wa kidhalimu duniani na utawala wa Kizayuni unaokalia kwa mabavu, sehemu ya ardhi ya Palestina ilichukuliwa, na watu wa Palestina wakafukuzwa kutoka katika nchi yao; nyumba zao ziliharibiwa na mali na raslimali zao zikaporwa, na hivyo kunyimwa haki zao za msingi za kibinadamu.”
Alisema: “Mchakato wa kulazimishwa kuwahamisha Wapalestina umeendelea kwa vizazi kadhaa, na leo mamilioni ya Wapalestina huko Ghaza wanaishi katika mazingira magumu sana, huku maelfu ya raia, hususan wanawake na watoto, wakiwa walengwa wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni.”
Uhalifu wa utawala wa Kizayuni huko Ghaza na Lebanon ni mfano wa mauaji ya kimbari na usafishaji wa kikabila
Katibu Mkuu wa Baraza la Kimataifa la Kuleta Ukaribu baina ya Madhehebu ya Kiislamu alielezea vitendo vya utawala wa Kizayuni huko Gaza, Lebanon na nchi nyingine za Kiislamu kuwa ni mauaji ya kimbari, usafishaji wa kikabila na mauaji ya halaiki, na kusema: “Uhalifu huu unaweka wazi viwango viwili vya mfumo wa dunia unaodai kutetea haki za binadamu.”
Aliongeza: “Ikiwa kuwaua watu wasio na hatia ni jambo baya, basi linapaswa kuwa baya kila mahali; na ikiwa kuwafukuza watu kutoka katika ardhi yao ni jambo lisilofaa, basi linapaswa kuwa lisilofaa kila mahali. Lakini kwa masikitiko, utawala wa Kizayuni unawasilisha mauaji ya watoto na wanawake kama ‘vita ya haki’, na utetezi wa haki za binadamu kama ‘ugaidi’.”
Kazem Jalali: Tunapaswa kusimama dhidi ya dhuluma na ukosefu wa uadilifu
Dkt. Kazem Jalali, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Urusi, katika hotuba yake, huku akizungumzia nafasi ya kihistoria ya Saint Petersburg na roho ya upinzani katika jiji hilo, alisema: “Mimi ni mwakilishi wa nchi ambayo imepambana na uchokozi wa Marekani na Israel na katika mapambano hayo pia imepata ushindi.”
Akizungumzia kudhoofika kwa maadili ya kidini na kimapokeo katika dunia ya leo, alisema: “Leo tunapaswa kujiuliza: Je, tunazingatia tu vipengele vya nje vya dini, au tumeuelewa ujumbe wa kweli na wa msingi wa dini?”
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliongeza: “Tunapaswa kujiuliza ikiwa mauaji ya makumi ya maelfu ya watu huko Palestina na kuuwawa wanawake na watoto huko Ghaza kumewaamsha wanazuoni na wasomi? Vilevile, je, kuuwawa watoto huko Minab na mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani hakujatufanya tutambue ukweli na kiini cha dini?”
Alisema: “Sote tunazungumza kuhusu kupinga misimamo ya itikadi kali ya kidini, lakini ikiwa wanazuoni hawatazungumza kuhusu kupambana na dhuluma na madola ya kishetani, je, jambo hili halitatoa mazingira ya kuenea misimamo ya itikadi kali?”
Jalalii, akizungumzia malengo ya Uzayuni, alisema: “Uzayuni umeweka mipango kwa ajili ya Waislamu, Wakristo na hata Wayahudi wa kweli, na kwa kutumia nyenzo za kisasa na zilizoendelea, umelenga maadili ya kidini na kibinadamu, maadili mema na uadilifu.”
Aliongeza: “Marekani leo, ikiwa na mtazamo wa Kifirauni, imesimama dhidi ya wafuasi wa dini zote za Mwenyezi Mungu, wakati Mitume wa Mwenyezi Mungu daima wamesimama dhidi ya dhuluma. Kwa hiyo, nasi tunapaswa kusimama dhidi ya dhuluma na ukosefu wa uadilifu; dhuluma ambayo leo moja ya mifano yake iliyo wazi zaidi ni Marekani.”
Viongozi wa dini nchini Urusi wasisitiza kuhifadhi maadili ya kidini na kimaadili
Mwanzoni mwa mkutano huo, Alexander Beglov, Gavana wa Saint Petersburg, huku akiwakaribisha wageni, alielezea furaha yake kutokana na umoja na mshikamano uliopo baina ya wafuasi wa dini na madhehebu mbalimbali katika jiji hilo.
Alisema: “Ndani ya Urusi, kwa ajili ya kuwawezesha vijana kukuza vipaji vyao, sera, sheria na programu mbalimbali zimeandaliwa kwa kuzingatia maadili ya kidini na kiroho, na mkutano huu ni fursa nzuri ya kuzisogeza karibu zaidi dini na madhehebu mbalimbali na kuimarisha umoja miongoni mwa watu.”
Askofu wa Kiorthodoksi wa Saint Petersburg pia alisema katika mkutano huo: “Misingi ya kimaadili katika jamii inazidi kupuuzwa; kwa hiyo, kuimarisha maadili ya kidini na kimaadili kunapaswa kuwa miongoni mwa majukumu yetu ya msingi.”
Aliongeza: “Imani inamualika mwanadamu katika kutafakari, na sisi tunawajibika mbele ya vizazi vijavyo. Saint Petersburg kwa karne nyingi imekuwa uwanja wa kuishi pamoja, umoja na mshikamano wa wafuasi wa dini na madhehebu mbalimbali.”
Alber Garkanov, Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu wa Urusi, katika hotuba yake pia alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi maadili ya kidini na kimapokeo, na kusema: “Maadili haya yanaweza kuiongoza jamii na utamaduni kuelekea katika wokovu.”
Akikosoa mtazamo wa kimaada wa ustaarabu wa Magharibi, kwa kusema: “Leo hii si wanazuoni pekee, bali waabudu wote wa Mungu duniani wanapaswa kuungana ili waweze kupata ushindi dhidi ya uyakinifu uliopindukia.”
Garkanov aliongeza: “Leo kuna mapambano muhimu yanayoendelea kwa ajili ya kuhifadhi hali ya kiroho, na tunapaswa kupinga athari za Kimagharibi na za kimaada na kuhifadhi maadili yetu ya kidini, kibinadamu na kiroho.”
Katika mkutano huu wa kimataifa, viongozi wa dini pia walisisitiza kwamba kukabiliana na migogoro ya dunia na changamoto za kimaadili za sasa kunawezekana kupitia tu kuimarisha maadili ya kidini na kibinadamu, uadilifu, utu, kuheshimiana na umoja baina ya dini na madhehebu.
Aidha, kumaliza janga la kibinadamu huko Palestina na Ghaza pamoja na kuunga mkono haki za msingi za taifa linalodhulumiwa la Palestina kulielezwa kuwa ni wajibu wa jamii ya kimataifa.
Maoni yako