Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, ikinukuu tovuti ya “Mir’at al-Bahrain”, ripoti za hivi karibuni kutoka Bahrain zinaonesha kwamba hatua za kisheria na kiusalama dhidi ya wanazuoni wa dini, wahubiri na taasisi za kidini zimevuka hatua ya kushughulikia kesi za mtu mmoja mmoja, na zimegeuka kuwa mfumo unaotia wasiwasi wa sera za kimfumo dhidi ya dhehebu moja. Kuchunguza kwa kina vipengele vya kesi hizi ambazo wakati mwingine huchukua hadi masaa 13, kunazusha swali la msingi: Je, mfumo wa mahakama wa Bahrain unawashtaki watu binafsi, au unalenga kuzuia utambulisho wa kidini na kuondoa vielelezo vya kidini vya sehemu kubwa ya jamii yake?
Zeinab Ali, mwandishi wa Bahrain, aliandika katika makala yake: “Msishangae ikiwa kesi ya wanazuoni wa dini itachukua zaidi ya nusu ya siku, yaani masaa 13; hasa pale ambapo kesi hiyo—kama mmoja wa wanasheria wa Bahrain alivyoielezea—haionekani kuwa ni kesi dhidi ya watu binafsi, bali inaonekana zaidi kuwa ni kesi dhidi ya dhehebu moja na tabaka fulani au sehemu ya jamii kwa ujumla, ambayo wanataka kuzuia uwepo wake na kupunguza vielelezo vyake katika maisha ya umma.”
Aliongeza kusema: “Ikiwa tutaziangalia hatua mbalimbali ambazo mamlaka za Bahrain zimechukua katika kipindi kilichopita, basi kauli hii, kwa maoni yangu, si ya kutia chumvi katika kuelezea hali hiyo; kwa sababu suala hilo halijaishia tena katika kuwakamata watu binafsi au kuwafungulia kesi katika masuala maalumu, bali limewafikia makhatibu, wasomaji wa maombolezo, yaani waimbaji wa maombolezo ya Ahlulbayt, maimamu wa misikiti, pamoja na viongozi wa Husseiniyyah. Aidha, limeenea hadi kwenye sherehe za kidini, mali za wakfu na vielelezo vya kidini vinavyohusiana na madhehebu ya Shia.
“Hatua hizi hazikutokea kwa ghafla; bali dalili za mwelekeo huu zilianza kujitokeza kwa uwazi zaidi kuanzia mwishoni mwa Septemba 2024 (mwanzoni mwa Mehr 1403), kisha wigo wa ufuatiliaji na msimamo mkali ukaendelea kupanuka, na kuyahusisha makundi, taasisi na taratibu mbalimbali za kidini.
“Chini ya siku moja baada ya kutangazwa kwa shahada ya Sayyid Hassan Nasrullah mwishoni mwa Septemba 2024 (mwanzoni mwa Mehr 1403), serikali ilianza kuchukua hatua na kutoa vitisho vilivyolihusisha kundi la makhatibu, waimbaji wa maombolezo, maimamu wa misikiti na viongozi wa Husseiniyyah.
“Baadaye, katika kipindi kilichofuata, waliendelea kukamatwa mmoja baada ya mwingine na kuwahusisha raia wengi; kabla ya hali hiyo kuingia katika hatua pana zaidi tarehe 9 Mei iliyopita (19 Ordibehesht 1404), ambapo amri ya kukamatwa kwa zaidi ya viongozi 40 wa dini ilitolewa, wakiwemo wanazuoni wakubwa, wahubiri na walimu wa Hawza.”
Jambo la kuzingatiwa katika kesi hizi ni kwamba, majina ya mashtaka na tuhuma zilizowasilishwa katika baadhi ya kesi hayaonekani kuhusiana na vitendo maalumu, bali yanaonekana zaidi kuhusishwa na hotuba za kidini, au imani na sherehe za kidini. Hapa ndipo linapojitokeza swali muhimu zaidi: Je, watu hawa wanawajibishwa kwa sababu ya vitendo walivyofanya, au uhusiano wao wa kidini na shughuli zao zinazohusiana na itikadi ndio umegeuka kuwa sababu kuu ya kufuatiliwa na kushtakiwa?
Suala hili haliishii katika ukamataji na kesi za mahakamani; kwa sababu taasisi za kisheria zimezungumzia tabia za kudhalilisha wanazuoni wa dini ndani ya mazingira ya mahakama. Aidha, zimesimuliwa taarifa kuhusu kusainishwa kwa matamko chini ya shinikizo, ambalo lilifikia hadi vitisho vya ubakaji.
Haya ni matendo yenye hatari kubwa sana, na iwapo ukweli wake utathibitishwa, basi suala hili halitakuwa tena ni tofauti tu kuhusu taratibu za kisheria, bali litafungua mlango mpana wa kuuliza kuhusu kiwango cha kuheshimiwa dhamana za kesi ya haki na haki za washtakiwa. Hivyo, uchunguzi huru na wa wazi kuhusu yote yaliyodaiwa katika suala hili unahitajika.
Kwa upande mwingine, mjadala na mvutano huu umeenea pia hadi kwenye wakfu na mali za kidini, kwani hatua na maamuzi yalichukuliwa ambayo yameibua wasiwasi mkubwa kuhusu mustakabali wa mali za wakfu zinazomilikiwa na Husseiniyyah.
Hatua hizi zilichukuliwa wakati mmoja na vikwazo vingine vilivyohusisha vielelezo na sherehe za kidini; miongoni mazo ni kupigwa marufuku maandamano ya maombolezo ya Imam Hussein, kuzimwa vipaza sauti vya nje vya Husseinia, pamoja na kuwakataza wafuasi wa madhehebu haya kusafiri kwa ajili ya kuzuru maeneo matakatifu nchini Iraq na Iran, na vitisho na maonyo yaliyotolewa baadaye kuhusiana na suala hilo.
Inawezekana kwamba kila moja ya hatua hizi, ikiwa itaangaliwa peke yake, inaweza kuonekana kuwa na sababu inayoweza kutetewa na serikali; iwe kwa mtazamo wa kiusalama au wa kisheria.
Lakini tatizo huanza pale hatua zote zinapowekwa katika muktadha au mfumo mmoja: ukamataji, kesi za mahakamani, shinikizo dhidi ya wahutubu na wasomaji wa maombolezo, vikwazo dhidi ya Huseinia na maandamano, hatua zinazohusu mali za wakfu, na msimamo mkali dhidi ya jumla ya sherehe za kidini.
Hapo ndipo inakuwa halali kuuliza swali linalokwenda zaidi ya suala la kumfuatilia au kumkamata mwanazuoni huyu au mhutubu yule: Je, tunakabiliwa na hatua chache za kiusalama na kisheria, au kuna mchakato wa mfululizo unaolenga utambulisho wa kidini na taratibu za kidini zenye mizizi ndani ya jamii ya Bahrain?
Sehemu yenye hatari zaidi katika hali hii si kukamatwa mwanazuoni fulani, mhutubu fulani au msomaji wa maombolezo fulani; bali ni pale ambapo kitendo chenyewe cha kidini kinapogeuzwa kuwa chanzo cha mashaka, sherehe za kidini zinawekwa chini ya vikwazo, na wanazuoni wa dini wanajikuta katika mduara wa kufuatiliwa kwa sababu ya hotuba zao au uhusiano wao wa kidini, huku hatua hizo zikienea hadi kwenye kumbi, Husseiniyyah na mali za wakfu zinazohusiana nazo.
Kutetea haki hizi hakumaanishi kuomba upendeleo kwa ajili ya dhehebu moja dhidi ya dhehebu jengine, bali kunamaanisha kutetea haki ya msingi ya kila raia ya kutekeleza kwa uhuru na usalama imani na sherehe zake za kidini.
Serikali inayowaheshimu raia wake haiifanyi itikadi yenyewe kuwa sababu ya adhabu, wala haifanyi utekelezaji wa sherehe za kidini kuwa kosa, na wala haishughulikii sehemu halisi ya jamii yake kana kwamba ni tatizo ambalo inapaswa kuliondoa.
Kwa sababu hiyo, suala la leo halihusiani tena na mtu mmoja au kesi moja pekee. Wakati mwanazuoni, mhutubu, msomaji wa maombolezo, mhubiri, kumbi, Husseiniyyah, matembezi na sherehe za kidini zote zinapowekwa katika mduara wa kulengwa au kuwekwa chini ya vikwazo, swali linakuwa la dharura zaidi: Je, kinachohitajika ni kuwawajibisha watu binafsi kwa misingi ya vitendo maalumu, kupitia kesi za haki na zilizo wazi, au kuna mchakato mpana zaidi ambao lengo lake ni kudhoofisha uwepo wa dhehebu moja kwa ujumla na kupunguza vielelezo vyake katika maisha ya umma?
Ikiwa suala ni lile la kwanza, basi kesi ya haki na iliyo wazi ndiyo mwamuzi wa mwisho, na ushahidi ndio unaoamua uwajibikaji.
Lakini ikiwa matukio yatathibitisha kuwepo kwa ubaguzi wa kimfumo kwa misingi ya uhusiano wa kidini, au kulengwa kwa taratibu na sherehe za kidini zenye amani, basi suala hili linakuwa kubwa zaidi kuliko kesi za kawaida za kisheria.
Hapo ndipo linapokuwa “suala la haki na uhuru”, pamoja na haki halisi ya kutekeleza imani na sherehe za kidini bila kuwepo hofu, vitisho au udhalilishaji.
Maoni yako