Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa hawza nchini Iran, katika barua aliyomwandikia Sheikh Yusuf Murad, Mufti Mkuu na Kiongozi wa Kidini wa Waislamu wa Romania, alisisitiza umuhimu wa mshikamano, kuimarishana na kujiepusha na aina yoyote ya mgawanyiko katika ulimwengu wa Kiislamu. Barua hiyo, ambayo iliwasilishwa na Hujjat al-Islam wal-Muslimin Muhammad Sadiq Amin al-Din, Mkuu wa Ofisi ya Dini na Madhehebu ya hawza, wakati wa ziara yake katika mji wa Constanța nchini Romania, imetajwa kuwa mwanzo wa ushirikiano mpana wa kielimu na kiutamaduni baina ya hawza ya Iran na jamii ya Waislamu wa Romania.
Katika barua hiyo, ambayo imeandikwa kwa kurejelea Aya za Qur’ani Tukufu na Sira ya Mtume (saww), imesisitizwa haja ya kimkakati ya umoja wa Umma wa Kiislamu, na kuelezwa wazi kwamba kuleta ukaribu baina ya madhehebu ya Kiislamu hakumaanishi kupuuza tofauti za kifiqhi na kiitikadi, bali kunamaanisha kusisitiza mambo ya pamoja na kushirikiana katika changamoto kubwa zinazoikabili dunia ya Kiislamu, zikiwemo uvamizi wa kiutamaduni, kudhoofishwa kwa taasisi ya familia na misimamo mikali. Aidha, alipongeza nafasi muhimu ya Mufti wa Romania katika kuendeleza ukaribu baina ya Waislamu na kuishi pamoja kwa amani.
Mkuu wa hawza nchini Iran, katika sehemu nyingine ya barua hiyo, alibainisha utayari kamili wa hawza ya Iran kushirikiana na Dar al-Ifta ya Romania katika nyanja tatu: elimu na utafiti; utamaduni na jamii; pamoja na masuala ya kiroho na maadili. Kubadilishana walimu na watafiti katika taaluma za fiqhi linganishi, elimu ya itikadi ya Kiislamu na historia ya Uislamu, kuandaa mikutano ya kimataifa yenye kuzingatia umoja wa Kiislamu, vijana na utambulisho wa kidini, pamoja na kuzingatia urithi wa pamoja wa kiirfani na kimaadili, ni miongoni mwa maeneo ya ushirikiano yaliyopendekezwa. Katika barua hiyo, msisitizo maalumu umetolewa kuhusu kufufua tafiti za Qur’ani na tafsiri linganishi kama mhimili wa pamoja wa Waislamu wote.
Mwisho wa barua hiyo, kwa kurejelea fatwa za Marajii wakuu wa Kishia kuhusu uharamu wa kuwatukana au kuwadhalilisha watakatifu wa Ahl al-Sunnah, imesisitizwa umuhimu wa kujiepusha na kutukanana kuhusu matukufu na vitakatifu vya kila upande, na kusisitiza uchamungu kuwa ndio kipimo cha ubora mbele ya Mwenyezi Mungu.
Mkuu wa hawza, katika barua hiyo, ameutaja ushirikiano mpana na jamii ya Waislamu wa Romania kuwa ni hatua yenye ufanisi katika kulinda urithi wa Uislamu halisi wa Muhammad (saww) na kukabiliana na misimamo mikali na uzushi, huku akimuombea Mufti Mkuu pamoja na ndugu wote wkiiislamu wa Romania mafanikio na heshima kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Maoni yako