Jumamosi 1 Agosti 2026 - 17:43
Kuweka sharti la kupata kibali cha serikali ya Bahrain ili kuwazuru Maimamu (as) ni miongoni mwa makatazo makubwa kabisa

Hawza/ Sheikh Adel Al-Shaala, mwanazuoni wa Kishia wa Bahrain, amesisitiza kwamba; ibada ya kuwazuru Maimamu Maasumina (as) si kama hukumu nyingine za kisheria, bali ni miongoni mwa alama na nembo kubwa za dini.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Adel Al-Shaala, mwanazuoni wa Kishia wa Bahrain, katika hotuba yake alisema: Ibada ya kuwazuru Maimamu Maasumina (as) si kama hukumu nyingine za kisheria, bali ni nembo kubwa ya dini ambayo kwa ajili ya kuilinda huenda ikahitajika kujitoa muhanga na kujitolea. Alibainisha kuwa; vizuizi na vikwazo vinavyowekwa katika njia hii vinawawekea waumini wajibu wa kisheria wa kuilinda ibada hii na kuzuia isigeuzwe kuwa jambo linalodhibitiwa na maamuzi ya mamlaka tawala.

Sheikh Al-Shaala alieleza kuwa; kadiri kiwango cha madhara na ugumu anaoupata zuwari wa Maimamu (as) kinavyoongezeka, ndivyo malipo na thawabu za ziara hiyo zinavyoongezeka pia, jambo ambalo limethibitishwa katika riwaya mbalimbali.

Alisema kuwa madhara hayo yanaweza kujumuisha kupoteza mali, kama vile mtu anayelipa gharama za safari huku akijua kuna uwezekano wa kuzuiwa kufika au kurejea, au anayebeba gharama hizo kwa nia ya kuvunja sera ya kuzuia safari. Pia yanaweza kujumuisha madhara ya kisaikolojia wakati wa kupita katika baadhi ya nchi zinazowafanyia uadui wafuasi wa Ahlul-Bayt (as), hatari ya kukamatwa, kunyimwa uhuru na hata uwezekano wa kupoteza maisha.

Sheikh Al-Shaala alikosoa kile alichokiita juhudi za serikali kuingilia masuala ya dini, akisema kuwa serikali inatumia hali ya sasa ya nchi, ambayo kwa mujibu wake ni matokeo ya muungano na Uzayuni, ili kupanua mamlaka yake juu ya mambo yote yanayohusiana na masuala ya kidini.

Katika muktadha huo alirejelea kubadilishwa kwa jina la "Idara ya Wakfu wa Jaafari" kuwa "Usimamizi wa Masuala ya Jaafari", akisema kuwa ni taasisi ya serikali inayotekeleza maagizo ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa lengo la kudhibiti masuala ya Mashia, itikadi zao na ibada zao.

Mwanazuoni huyo wa Kishia wa Bahrain aliendelea kuzungumzia vizuizi vya safari na kusema kuwa; kuna mkanganyiko mkubwa, alisema kwamba wakati raia wageni na wakazi wanaruhusiwa kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani hata Palestina inayokaliwa kwa mabavu, raia halisi wa Bahrain mfuasi wa Ahlul-Bayt (as) hukumbana na vizuizi anapotaka kusafiri kwa ajili ya kuwazuru Maimamu (as), na daima huwa katika hatari ya kuhojiwa, kushtakiwa, kutukanwa au kunyimwa uhuru.

Alisema kuwa; hatua za sasa za kuzuia safari hazitadumu milele, lakini kwa tathmini yake ni hatua ya kimkakati inayolenga kuuweka ibada ya kuwazuru Maimamu (as) chini ya udhibiti kamili wa serikali na kudhibiti kila kipengele chake. Alisema kuwa njia hii ndiyo ambayo hapo awali Ayatullah Sheikh Isa Qassim alikuwa ameitahadharisha.

Sheikh Al-Shaala alinukuu kauli ya Ayatullah Sheikh Isa Qassim iliyosema kwamba: Kusimamisha ziara ya Maimamu Watoharifu kwa kuifanya itegemee kibali cha kiutawala, kama inavyosisitizwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain, ni miongoni mwa makatazo makubwa kabisa.

Alisisitiza kuwa; msimamo huu umetolewa na "faqihi mwenye utambuzi na basira", na kwamba wanaume na wanawake waumini wanapaswa kujiepusha na kuupinga.

Mwanazuoni huyo alieleza kuwa, ingawa mafaqihi wanatofautiana kuhusu hukumu ya kifiqhi ya kuzuru Maimamu (as), kuanzia kuiona kuwa ni sunna yenye msisitizo mkubwa hadi kuiona kuwa ni wajibu katika hali mbalimbali, wote wanakubaliana kwamba ziara ni hukumu ya kisheria, na hakuna taasisi ya serikali yenye mamlaka ya kuifanya iwe ibada inayotegemea kibali cha kiutawala.

Sheikh Al-Shaala alisisitiza kuwa; jukumu liko juu ya wafuasi wote wa Ahlul-Bayt (as) kuhakikisha kuwa hawairuhusu serikali "kunyakua hukumu ya kisheria" na kuhamisha mamlaka ya kuamua kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenda kwa mamlaka ya serikali, kiasi kwamba serikali ndiyo iamue ni nani anaruhusiwa na ni nani anayekatazwa.

Alisema kuwa kuweka sharti la kibali cha serikali kwa ajili ya kuzuru Maimamu (as) ni "ujasiri mkubwa sana dhidi ya mamlaka ya Mwenyezi Mungu", na kwamba kuweka mazingira ya kuiwezesha serikali kutumia mamlaka hayo ni kuisaidia kutenda kile alichokiita "miongoni mwa makatazo makubwa kabisa."

Mwanazuoni huyo wa Kishia wa Bahrain pia alitahadharisha dhidi ya namna zote, za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, za kuimarisha mtazamo huo, iwe kwa kudharau hukumu ya kisheria au kwa kutoa vibali na ruhusa kwa watu binafsi au misafara, jambo ambalo linaimarisha msingi wa kwamba ibada ya ziara inapaswa kutegemea kibali cha serikali.

Mwishoni, Sheikh Al-Shaala alisisitiza kuwa; suala hili si jambo binafsi linalowahusu waandaaji wa misafara, wafanyakazi au watu fulani, bali linahusiana na mustakabali wa wafuasi wote wa Ahlul-Bayt (as) nchini Bahrain. Alionya kuwa haifai kuacha hukumu ya kisheria kwa sababu ya maslahi ya muda au hofu, kwani athari zake zitagusa mustakabali wa jamii nzima.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha