Jumanne 28 Julai 2026 - 01:06
Ayatullah A'rafi asisitiza kuwa, Iran itaendelea kuiunga mkono Palestina

Hawza/ Ayatullah A'rafi katika hotuba yake kwenye kikao cha ufunguzi wa Kongamano la Tano la Kimataifa la “Nidaa al-Aqsa” lililofanyika Karbala, alisisitiza kuendelea kwa uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kadhia ya Palestina.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah A'rafi katika hotuba yake kwenye kikao cha ufunguzi wa Kongamano la Tano la Kimataifa la “Nidaa al-Aqsa” lililofanyika Karbala, alisisitiza kuendelea kwa uungaji mkono wa Iran kwa kadhia ya Palestina na akatoa wito wa kuunganishwa kwa safu za Waislamu, kupambana na mchakato wa kuhalalisha uhusiano na Israel, pamoja na kukatiza aina yoyote ya mahusiano na utawala huo.

Siku ya Jumamosi, shughuli za Kongamano la Tano la Kimataifa la “Nidaa al-Aqsa” zilianza rasmi kwa kikao cha ufunguzi katika mji mtukufu wa Karbala. Katika kongamano hilo, wajumbe mbalimbali na shakhsia kutoka nchi za Kiarabu na kimataifa walikusanyika kwa lengo la kujadili nafasi ya vyombo vya habari na simulizi sahihi katika kuisaidia kadhia ya Palestina, pamoja na kupata msukumo kutoka katika misingi ya Mapinduzi ya Imam Hussein (as) ili kukabiliana na upotoshaji na kueneza kuielewesha jamii.

Ayatullah Alireza A'rafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, alisema katika hotuba yake kuwa; baadhi ya nchi za eneo hili zimesimama upande wa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, huku akisisitiza kwamba misimamo ya nchi hizo inahudumia maslahi ya wavamizi.

Aliongeza kuwa; Iran itaendelea kuiunga mkono kadhia ya Palestina ili kukabiliana na miradi ya uadui dhidi ya eneo hili, na akatoa wito wa kuunganishwa kwa safu za Waislamu, kuondokana na tofauti za kimadhehebu na kikabila, pamoja na kuandaliwa kwa hati ya pamoja kuhusu Palestina ambayo itajumuisha mpango wa vitendo ulio wazi.

Mkurugenzi wa Hawza pia alitoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuitambua “haki ya kufanya mapambano ya kujihami” na “Mhimili wa Muqawama”, pamoja na kuthibitisha haki ya wananchi wa Palestina ya kupiga kura ya maoni ya jumla ili kuamua mustakabali wao. Aidha, alisisitiza kupingwa kwa “Muamala wa Karne” na kufanya juhudi za kuufelisha kwa kutumia njia zote zinazowezekana.

Ayatullah A'rafi pia alitoa wito wa kukatizwa kwa aina zote za mahusiano ya kiuchumi, kibiashara na kitamaduni na utawala wa Kizayuni, kususiwa kikamilifu bidhaa zake katika ulimwengu wa Kiislamu, kuvunjwa kwa mahusiano ya kisiasa na kufungwa kwa balozi za utawala huo katika nchi husika. Vilevile alisisitiza kuzingatia mapambano dhidi ya uvamizi na kutoa misaada ya kifedha kwa harakati za Muqawama nchini Palestina na Lebanon.

Hassan Rashid Jawad Al-Abayiji, msimamizi wa Ataba Tukufu ya Imam Hussein (as), pia alisisitiza katika mkutano huo kwamba; kufanyika kwa kongamano hili kumejengwa juu ya misingi ya Imam Hussein (as) ya kufanya mageuzi, kuamrisha mema, kukataza maovu na kupambana na dhulma. Alisema kwamba kadhia ya Palestina ni mwendelezo wa harakati hiyo na ni ujumbe wa milele wa kupambana na dhulma na kuwatetea wanaodhulumiwa.

Abdul Latif Al-Haj, Mratibu Mkuu wa Kampeni ya Kimataifa ya Kurejea Palestina, pia alieleza kuwa kilio cha Wapalestina kinaendana na wito wa Imam Hussein (as) katika kupambana na dhulma.

Alitoa wito wa kujengwa kwa simulizi la kweli linalotegemea ukweli, nyaraka na ushahidi wa moja kwa moja kutoka uwanjani ili kukabiliana na kampeni za upotoshaji na vyombo vya habari vyenye mwelekeo maalumu.

Al-Haj aliongeza kuwa; vilio vya wanawake, watoto na wanaume wa Ghaza vimepata mwitikio mkubwa katika maandamano ya mitaani, vyuo vikuu na viwanja mbalimbali vinavyodai kusimamishwa kwa mauaji ya kimbari, kuwafikisha wahusika mbele ya sheria na kuikomboa Palestina—ardhi na watu wake.

Sayyid Abdul Qadir Al-Hassani Al-Alusi, Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni la Ribat Muhammadi, alizungumzia suala la kupotoshwa kwa simulizi la kihistoria la Umma wa Kiislamu na kusisitiza kwamba; jukumu la kupambana na upotoshaji huo ni sehemu ya “vita ya kuutetea ukweli”, ambavyo vilianza tangu tukio la Karbala.

Akisisitiza kuwa Msikiti wa Al-Aqsa ndiyo kiini cha mapambano kati ya haki na batili, alionya kwamba; kuhalalisha uhusiano wa baadhi ya serikali na “adui mvamizi na mkoloni” ni usaliti mkubwa dhidi ya kadhia ya Palestina.

Adnan Mansour, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Lebanon, alisema katika hotuba yake kwamba; Palestina, kwa ardhi yake yote, katika historia, wakati wa sasa na siku zijazo, inaendelea kuuita Umma wa Kiarabu, Umma wa Kiislamu na watu wote huru duniani. Alisisitiza kwamba: “Kadiri uvamizi unavyoendelea, hakutakuwa na amani katika eneo hili,” na kwamba kushindwa kwa Umoja wa Mataifa kutekeleza maazimio yake tangu mwaka 1948 kumewasukuma wananchi wa Palestina kuelekea kwenye Muqawama wa kisheria kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Mansour alitoa wito wa kuunganishwa kwa juhudi za wanasiasa, wanafikra, wanahabari, wasomi wa vyuo vikuu na wanaharakati ili kukabiliana na kampeni za uharibifu na upotoshaji zinazoongozwa na taasisi zinazohusishwa na makundi ya ushawishi yanayoiunga mkono Israel.

Vilevile, Sheikh Amer Al-Bayati alitoa hotuba kwa niaba ya Mufti wa Iraq, Sheikh Mahdi Al-Sumayda'i. Katika hotuba yake alisisitiza kupinga kuhalalishwa kwa uhusiano na Israel na kutokukubali kuachia hata upana wa shibri moja ya ardhi ya Palestina. Aidha, alisisitiza kwamba msimamo wa wananchi wa Palestina unapaswa kubaki imara na kwamba njia ya kujitolea na kujitoa mhanga iendelee hadi ushindi utakapopatikana.

Aliongeza kuwa; mji wa Quds umewahi kukombolewa mara nyingi katika historia, na kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, ukombozi wake uko karibu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha