Jumatatu 27 Julai 2026 - 15:14
Kuwatetea Wapiganaji Jihadi wa Lebanon ni Sera ya Kimkakati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Hawza/ Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika kujibu barua ya Katibu Mkuu na wapiganaji wa Hizbullah, amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuzingatia msimamo wa Kiongozi Mkuu na Shahidi wa Mapinduzi, Imam Sayyid Ali Khamenei (r.a), imeifanya kutetea Mujahidina hawa madhulumiwa lakini wenye nguvu (wapiganaji wa Hizbullah) kuwa sera yake ya kimkakati. Aidha, imeweka kulinda ukamilifu wa ardhi ya Lebanon na kukomeshwa kikamilifu na bila masharti uvamizi wa utawala wa Kizayuni kuwa sharti la kwanza la makubaliano ya kumaliza vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Marekani mvamizi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Mtukufu Ayatullah Sayyid Mujtaba Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametoa ujumbe katika kujibu barua ya Katibu Mkuu na wapiganaji wa Hizbullah.

Ifuatayo ni matini kamili ya ujumbe huo:

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قَاتِلُوا الَّذِينَ يَلُونَكُم مِّنَ الْكُفَّارِ وَلْيَجِدُوا فِيكُمْ غِلْظَةً...

Mtukufu Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Naim Qassim (Mwenyezi Mungu aendeleze heshima yake), Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, pamoja na makamanda wote na wapiganaji waliojitolea kwa nafsi zao, wenye subira na imara wa Hizbullah.

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Barua yenu, enyi ndugu zangu na wanangu, wapiganaji waumini na mashujaa wa Hizbullah tukufu, iliyobeba ujumbe wa ustahimilivu na uimara kwa ajili ya kuliinua Neno la Mwenyezi Mungu, kuamini ahadi za Qur'ani Tukufu na malengo yenye kuleta heshima ya Imam Khomeini pamoja na Kiongozi Shahidi Ayatullah Mkuu Sayyid Ali Khamenei (Mwenyezi Mungu awarehemu wote wawili), inastahiki kuthaminiwa na kuheshimiwa.

Leo hii, ambapo mataifa ya dunia yamechoshwa na dhulma na uonevu wa serikali ya Marekani pamoja na Wazayuni wahalifu wanaoharibu mimea na kuangamiza vizazi vya wanadamu, hakuna njia nyingine iliyobaki isipokuwa Jihadi na Muqawama. Kusimama imara katika njia hii kutawapatia wanaopigana jihadi kwenye njia ya haki nusura iliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu.

...وَكَانَ حَقًّا عَلَيْنَا نَصْرُ الْمُؤْمِنِينَ

Sasa ambapo Hizbullah ya Lebanon, ikiwa ni kinara wa makundi ya Jihadi mbele ya mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na utawala wa Kizayuni na wanao waunga mkono, imesimama imara kama jabali lisilotikisika, uimara huu umekuwa ujumbe wenye kuhamasisha mataifa huru ya dunia katika kujikomboa dhidi ya dhulma na uonevu wa ubeberu wa kimataifa pamoja na vibaraka wake. Bila shaka, sehemu kubwa ya mafanikio haya makubwa inatokana na subira, heshima, kujitolea na ushirikiano wa wananchi wa Lebanon, hususan wa eneo la kusini mwa nchi hiyo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia, kwa kuzingatia msimamo wa Kiongozi Mkuu na Shahidi wa Mapinduzi, Imam Sayyid Ali Khamenei (r.a), imeifanya kuwatetea Mujahidina hawa madhulumiwa lakini wenye nguvu kuwa sera yake ya kimkakati. Aidha, imeweka kulinda ukamilifu wa ardhi ya Lebanon na kukomeshwa kikamilifu na bila masharti uvamizi wa utawala wa Kizayuni kuwa sharti la kwanza la makubaliano ya kumaliza vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Marekani mvamizi.

Rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mashahidi, majeruhi, familia zao zenye subira, pamoja na wahamiaji katika njia ya Mwenyezi Mungu waliovumilia na kubeba kwa moyo wa uthabiti mitihani na masaibu.

Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya roho tukufu ya Kiongozi wa Mashahidi wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrallah, na juu ya makamanda wote waliotangulia wa Muqawama pamoja na wenzake mashahidi (Mwenyezi Mungu awarehemu wote), ambao waliugeuza mche wa Muqawama wa Kiislamu kuwa mti mkubwa wenye mizizi iliyothabiti na matawi yake yaliyofika mbinguni. Wapiganaji hao ambao kwa Jihadi na Muqawama wao wameiletea Lebanon heshima na utukufu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Mwisho, ninatumaini kwamba kwa baraka za dua njema za Bwana wetu (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake tukufu), aina zote za uangalizi na fadhila za Mwenyezi Mungu zitawashukia wale wote wenye kupigana jihadi, mashahidi, waliojeruhiwa ndani ya Muqawama, wahamiaji na familia zao zenye subira.

وَنُرِيدُ أَن نَّمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الْأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Sayyid Mujtaba Hosseini Khamenei

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha