Jumatatu 27 Julai 2026 - 09:30
Viongozi wa Bahrain hawazingatii sheria zozote za kimataifa

Hawza/ Chama cha Haki za Binadamu cha Bahrain kimesisitiza kuendelea kwa kile kilichokitaja kuwa ni sera ya makusudi ya mamlaka ya nchi hiyo ya kuwavunjia heshima maulamaa wa Kishia waliokamatwa, pamoja na kutoheshimu Katiba ya nchi.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Chama cha Haki za Binadamu cha Bahrain, katika taarifa iliyochapishwa kupitia tovuti yake, kimesisitiza kuendelea kwa kile kilichokitaja kuwa ni sera ya makusudi ya mamlaka ya Bahrain ya kuwavunjia heshima maulamaa wa Kishia waliokamatwa, kutoheshimu Katiba ya nchi na mikataba ya kimataifa iliyosainiwa na Bahrain, pamoja na kutumia mbinu za vitisho, mateso na ukiukaji wa wazi wa heshima ya utu wa binadamu.

Chama hicho kilisema kuwa; mamlaka za Bahrain, kwa kutumia vibaya mazingira ya kisiasa yanayohusiana na vita vinavyoendelea katika eneo pamoja na sera ya "kutoadhibiwa" ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitumika nchini humo, zinawadhalilisha kwa makusudi maulamaa wa Kishia waliokamatwa. Kwa mujibu wa taarifa zilizopokelewa, maulamaa ishirini waliokamatwa wamekataa kukutana na mawakili wao wakipinga hatua za kiholela na matumizi ya minyororo ya chuma mikononi na miguuni mwao. Taarifa hiyo ilisema kuwa hali hii inaonesha kuongezeka kwa ukiukaji wa dhamana za kesi ya haki, inayokanyaga utu wa binadamu na kukiuka haki zilizohakikishwa katika mikataba ya kimataifa na Katiba ya Bahrain.

Chama hicho kilirudia kulaani vikali ukiukaji mkubwa wa haki na heshima ya binadamu, ikiwemo haki ya kujitetea, kanuni ya kudhaniwa kuwa mtu hana hatia hadi ithibitike vinginevyo, uhuru wa mhimili wa mahakama, na haki ya kutofanyiwa mateso au vitendo vya udhalilishaji.

Chama cha Haki za Binadamu cha Bahrain kilisisitiza tena kuwa; mamlaka za Bahrain haziheshimu sheria zinazohusu haki za wafungwa zilizomo katika Kanuni za Kiwango cha Umoja wa Mataifa za Kuwatendea Wafungwa, pamoja na mikataba ya kimataifa, hususan Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa. 

Chama cha Haki za Binadamu cha Bahrain kilionya kuhusu hatari ya mwenendo unaochukuliwa na mamlaka za nchi hiyo, na kuitaka jumuiya ya kimataifa kufanya shinikizo na kuingilia kati haraka ili kulinda heshima na kuhakikisha usalama wa maulamaa hao. Pia kilitoa wito wa kufunguliwa uchunguzi huru wa kimataifa na wa haraka ili kuhakikisha uwajibikaji na kukomesha hali ya kuendelea kutoadhibiwa nchini humo.

Aidha, chama hicho kilitaka kuachiwa huru mara moja na bila masharti maulamaa wa Kishia waliokamatwa. Pia kilimwomba Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Mwandishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mateso, Mwandishi Maalumu kuhusu uhuru wa dini na imani, Mwandishi Maalumu kuhusu uhuru wa majaji na mawakili, pamoja na Kikundi Kazi kuhusu ukamataji wa kiholela, kufuatilia suala hilo. Chama hicho pia kilitaka kuandikiwa serikali ya Bahrain ili kutoa taarifa sahihi kuhusu hali ya waliokamatwa na dhamana za kisheria walizonazo, pamoja na kusisitiza umuhimu wa kufanya ziara za ukaguzi wa moja kwa moja na kutathmini kiwango ambacho hatua zilizochukuliwa zinazingatia wajibu wa Bahrain chini ya sheria za kimataifa.

Mwishoni, Chama cha Haki za Binadamu cha Bahrain kilisisitiza kuwa; mamlaka za Bahrain zinabeba jukumu kamili la usalama wa maulamaa waliokamatwa na madhara yoyote ya kimwili au kisaikolojia ambayo yanaweza kuwapata kutokana na kukamatwa kwao kiholela. Aidha, kilimtaja hasa mtawala wa Bahrain Hamad Isa Al Khalifa na Waziri Mkuu Salman Hamad Al Khalifa kuwa wanawajibika kwa hali hiyo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha