Jumatatu 27 Julai 2026 - 06:30
Vyama vya Mapinduzi vya Bahrain yvatoa wito wa mshikamano na Maulamaa waliofungwa magerezani

Hawza/ Wawakilishi wa vyama vya mapinduzi vya Bahrain wamesisitiza yaliyopo katika taarifa ya Ayatullah Sheikh Issa Qassim, ambayo imeelezea hali ya Bahrain kuwa ni "tishio la uwepo" dhidi ya raia wa Kishia nchini humo.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, wawakilishi wa vyama vya mapinduzi vya Bahrain wamesisitiza yaliyomo katika taarifa ya Ayatullah Sheikh Issa Qassim, ambayo imeelezea hali ya Bahrain kuwa ni "tishio la uwepo" dhidi ya raia wa Kishia nchini humo.

Vyama vya upinzani vimechapisha muhtasari wa mkutano wao wa pili wa mara kwa mara, ambapo vilizungumzia kile walichokieleza kuwa ni kutendwa kwa jinai zisizo na mfano na utawala dhidi ya wananchi halisi wa nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani viongozi wakuu wa kidini na kuendesha vita vya kuangamiza madhehebu ya Shia nchini Bahrain. Katika taarifa hiyo ilisisitizwa kuwa kampeni za ugaidi wa dola na vita vya usafishaji vinavyolenga misikiti, Husseiniyya, wakfu za Kiislamu, maulamaa na maeneo ya ziara za kidini, vinafanyika moja kwa moja kwa amri ya mtawala Hamad, na kutekelezwa na Waziri wake wa Mambo ya Ndani, Rashid Al Khalifa.

Vyama hivyo vilisisitiza kuwa; uaminifu kwa taifa na dini unahitaji kutokubali dhulma na kukataa kulegeza msimamo mbele ya ukiukaji wa mamlaka ya nchi. Pia vilisisitiza umuhimu wa kupinga sera ya kuwalenga wananchi kwa misingi ya madhehebu yao, kuwa na uelewa kamili wa michezo ya kisiasa ya wenye madaraka, kusimama imara dhidi ya kuhatarishwa kwa nchi na mali zake, pamoja na kushikamana na umoja wa kitaifa na kuulinda dhidi ya mikakati ya nje na kuingizwa katika miungano na mipango ya kivamizi.

Aidha, vyama vya mapinduzi vilitangaza ushiriki wao wa dhati katika maadhimisho ya shahada ya Imam Hasan al-Mujtaba (as) tarehe saba ya mwezi wa Safar. Pia vilisisitiza kutokuzingatia sheria walizozitaja kuwa za kidhalimu ambazo zinanyima haki na uhuru wa umma, hususan sheria zilizowekwa katika mfumo wa vita vya usafishaji vinavyoongozwa na Hamad, kwa lengo la kuhalalisha kuzuia na kuadhibu nembo za kidini, kueneza hofu miongoni mwa wananchi na kuzuia ushiriki wao mkubwa katika hafla za kidini, ambazo ni sehemu ya utambulisho wa asili wa Bahrain na wananchi wake.

Vyama hivyo viliwataka wananchi kuitangaza siku ya Ijumaa kuwa "Ijumaa ya Kuwanusuru Maulamaa", siku ya kuonesha mshikamano na maulamaa waliotekwa na kufungwa. Viliwataka wananchi wakusanyike misikitini na kumuomba Mwenyezi Mungu awaachilie huru maulamaa waliowekwa katika magereza ya utawala huo, awaangamize madhalimu na watesi, na aikomboe jamii dhidi ya dhulma na mateso. Pia vilitoa wito wa kupatikana kwa usalama na amani kwa watu wa Bahrain na mataifa yote ya Kiarabu na Kiislamu kupitia kuondoka kwa wavamizi na madola ya kibeberu katika ardhi zao.

Mwishoni, vyama vya mapinduzi viliwataka wananchi kushiriki siku ya Ijumaa katika maandamano na mikusanyiko ya kampeni ya "Ijumaa ya Kuwanusuru Maulamaa" katika maeneo yote ya nchi, ili kuonesha upinzani wao dhidi ya kile walichokiita vita vya usafishaji na mauaji ya kimbari vinavyoongozwa na Hamad, hususan kuhusu kuwafikisha mahakamani maulamaa wakuu, jambo ambalo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, linalenga kuvunja kwa makusudi heshima na hadhi yao ya kidini na kitaifa na kuwaweka katika aina mbaya zaidi za mateso ya kimwili na kisaikolojia.

Katika maandamano hayo, washiriki wanatarajiwa kupaza sauti kaulimbiu zinazoeleza kwamba wananchi wa Bahrain hawatakubali kamwe kusalimu amri wala kurudi nyuma, na wataendelea kuwa waaminifu kwa taifa lao, utambulisho wao, nembo zao za kidini na maulamaa wao.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha