Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Akitoa mawaidha yake, Maulana Hemed Jalala, alisema kuwa: Mazishi ya Sayyid Ali Khamenei hayakuwa tukio la kawaida, bali lilikuwa somo kubwa lililoonesha namna jamii inavyoweza kujengwa kwa misingi ya umoja, uadilifu, uzalendo na kuheshimiana. Alieleza kuwa kila Muumini anapaswa kutafakari ujumbe uliobebwa na tukio hilo na kuugeuza kuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku.
Funzo la Kwanza: Umuhimu wa umoja wa Mashia
Maulana Hemed alieleza kuwa; funzo la kwanza ni umuhimu wa kuimarisha umoja wa Mashia. Alisema nguvu ya jamii yoyote hupatikana pale wanajamii wake wanapokuwa na mshikamano, kusaidiana na kusimama pamoja katika nyakati za furaha na za mitihani. Alisisitiza kuwa tofauti ndogo za mitazamo hazipaswi kuwa sababu ya migawanyiko, bali kila mmoja anapaswa kutanguliza maslahi ya Uislamu na umoja wa Waumini.
Funzo la Pili: Umoja wa Waislamu bila kujali tofauti za madhehebu
Akifafanua funzo la pili, Maulana alisema kuwa; tukio hilo limeonesha umuhimu wa Waislamu kushikamana licha ya kuwepo kwa tofauti za kimadhehebu. Alieleza kuwa kinachowaunganisha Waislamu ni kikubwa zaidi kuliko kinachoweza kuwatenganisha, hivyo akatoa wito wa kuendeleza upendo, kuheshimiana na kushirikiana katika mambo yanayolenga kuimarisha dini, amani na maendeleo ya jamii.
Funzo la Tatu: Umoja wa watu wa dini mbalimbali katika kuthamini utu wa binadamu
Maulana Hemed alibainisha kuwa; funzo la tatu ni umuhimu wa watu wa dini mbalimbali kuishi kwa amani, kuheshimiana na kushirikiana katika mambo yenye manufaa kwa jamii. Alisema kuwa tofauti za dini hazipaswi kuwa chanzo cha chuki au migogoro, bali zinapaswa kuwa fursa ya kujenga maelewano, kuthamini utu wa kila mwanadamu na kushirikiana katika kulinda haki, amani na mshikamano wa kitaifa.
Funzo la Nne: Uzalendo na kuipenda nchi
Funzo la nne, kwa mujibu wa Maulana Hemed Jalala, ni umuhimu wa uzalendo. Aliwahimiza waumini kuipenda Tanzania kwa dhati, kuitumikia kwa uaminifu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Alisisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kulinda amani, umoja na ustawi wa taifa, kwani maendeleo ya nchi yanategemea mchango wa wananchi wake.
Funzo la Tano: Kuwaheshimu na kuwapenda viongozi wanaolitumikia taifa kwa uadilifu
Akizungumzia funzo la tano, Maulana alisema kuwa; jamii inapaswa kuwaheshimu na kuwaunga mkono viongozi wanaojitolea kulitumikia taifa na wananchi kwa uadilifu, uaminifu na kujituma. Alieleza kuwa viongozi wa aina hiyo wanastahili kuthaminiwa na kuombewa dua ili waendelee kusimamia haki, kuimarisha maadili na kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.
Akihitimisha mawaidha yake, Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, aliwataka waumini wote kuyafanyia kazi mafunzo hayo badala ya kuishia kuyasikiliza pekee. Alisema kuwa jamii itafanikiwa kuwa na amani ya kudumu, mshikamano wa kweli na maendeleo endelevu pale ambapo kila mmoja atatekeleza wajibu wake kwa kumcha Mwenyezi Mungu, kuwapenda wenzake na kutanguliza maslahi ya taifa mbele ya maslahi binafsi.
Majlisi hiyo ilimalizika kwa dua na nasaha mbalimbali zilizowahimiza waumini kuendelea kushikamana na mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s.), kuimarisha umoja wao na kuwa nguzo ya amani na maendeleo katika jamii.



Maoni yako