Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, hafla hiyo ilifanyika siku ya Jumamosi, tarehe 3 Safar 1448 Hijria, kwa ushiriki mkubwa wa waombolezaji wa Imam Hussein (as) katika eneo la Birnin Kudu, lililopo Jimbo la Jigawa kaskazini mwa Nigeria.
Matembezi hayo yalianza kupitia njia kuu mbili. Njia ya kwanza ilianzia katika kituo cha mkusanyiko cha Babaldo, ambapo waombolezaji kutoka miji na vijiji vya Sara, Samamiya, Tsangarawa, Kiyako, Babaldo, Bodinga na maeneo ya jirani walishiriki, wakielekea hadi mji wa Birnin Kudu.
Njia ya pili ilianzia katika kituo cha mkusanyiko cha Tsamia, kwa ushiriki wa waombolezaji kutoka Birnin Kudu, Igi, Yalwan Damai, Kafin Gana, Kangire na maeneo yanayozunguka.
Washiriki, ambao walifikia mamia ya watu, walivaa mavazi meusi na kubeba bendera pamoja na picha za viongozi mashuhuri wa Muqawama, akiwemo Imam Khomeini (ra), Ayatullah Imam Sayyid Ali Khamenei, Ayatullah Sayyid Mujtaba Hosseini Khamenei (Mwenyezi Mungu azidumishe baraka zake), Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mashahidi wengine wa Muqawama. Walitoa tenzi za maombolezo na kuimba nauha wakihuisha kumbukumbu ya mashahidi wa Karbala na masaibu yaliyowapata Ahlul-Bayt (as) baada ya tukio la Ashura.
Hafla hiyo ilimalizika katika mazingira ya utulivu na nidhamu, huku baadhi ya wakazi wa miji na vijiji vilivyokuwa kandokando ya njia za maandamano wakijitokeza kuwakaribisha waombolezaji wa Imam Hussein (as) na kuonesha mshikamano wao pamoja nao.
Matembezi ya Birnin Kudu ndiyo hafla ya kwanza ya Arubaini ya Imam Hussein (as) kwa mwaka 1448 Hijria nchini Nigeria. Inatarajiwa kuwa katika siku zijazo maeneo mbalimbali ya nchi hiyo yataandaa maandamano mengine kama hayo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, kilele cha maandamano ya Arubaini ya mwaka huu kitafanyika katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.
Maoni yako