Jumatano 22 Julai 2026 - 09:00
Ukiukwaji wa Haki za Raia nchini Bahrain Imekuwa Sera Iliyopangwa Dhidi ya Mashia na Wanazuoni

Hawza/ Sheikh Adel Al-Shaala amesema kuwa; ukiukwaji wa mara kwa mara wa haki za raia wa Kishia unaoshuhudiwa leo nchini Bahrain haujaishia tena katika vikwazo vya kisiasa au kiusalama, bali umegeuka kuwa ukiukwaji wa moja kwa moja wa matukufu ya kidini na ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul Islam wal-Muslimin Sheikh Adel Al-Shaala, mwanazuoni wa Kishia kutoka Bahrain, alisema katika hotuba yake kwamba; ukiukwaji wa haki za raia wa Kishia unaoshuhudiwa nchini Bahrain leo hauko tena katika kiwango cha vikwazo vya kisiasa au kiusalama pekee, bali umefikia hatua ya kukiuka moja kwa moja matukufu ya kidini na ya kibinadamu.

Alisema kuwa mamlaka tawala zinaendeleza sera inayolenga utambulisho wa wafuasi wa Ahlul-Bayt (as), matukufu yao na taasisi zao za kidini, sambamba na kuongezeka kwa hatua ambazo hazijawahi kushuhudiwa dhidi ya kundi kubwa zaidi la wananchi wa nchi hiyo, yaani Mashia.

Sheikh Al-Shaala alisema: "Utawala wa Bahrain umeonesha wazi dhamira yake ya kuiangamiza dini na mafundisho ya Ahlul-Bayt (as)."

Akizungumzia vielelezo vya sera hiyo, alisema miongoni mwa hatua zake kuu ni kuidhibiti mihimili ya mahakama na kuibana kwa kiwango kikubwa Mahakama ya Jaafaria huku mashauri mengine yakipelekwa katika mfumo wa mahakama ambao kwa mujibu wake, "hayana uhusiano wowote na Uislamu wala sheria."

Mwanazuoni huyo wa Bahrain aliongeza kuwa; miongoni mwa mifano mingine ya wazi ya kulengwa Mashia ni kudhibitiwa wakfu za wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) na kunyakuliwa kinyume cha sheria mali na ardhi zao. Aidha, alisema makumi ya misikiti, ambayo baadhi yake ilijengwa hata kabla ya kuingia kwa familia tawala nchini Bahrain, imebomolewa kabisa.

Pia alieleza kuwa; wakati Mashia wanazuiwa kujenga misikiti katika maeneo yao, vibali vinatolewa kwa madhehebu mengine kujenga misikiti katikati ya maeneo yenye wakazi wengi wa Kishia, jambo hili linaashiria sera iliyopangwa ya ubaguzi wa kimadhehebu na inayochochea chuki.

Sheikh Al-Shaala alisema kuwa; mamlaka tawala zimevuka mipaka ya kuzilenga taasisi za kidini pekee, na sasa zimeelekeza hatua zake dhidi ya alama na viongozi wa kidini wa Mashia kwa kuwakamata makumi ya wanazuoni, wakiwemo mafaqihi wanaohesabiwa kuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri katika jamii hiyo.

Alisisitiza kuwa; utawala wa Bahrain hauoneshi kuthamini kundi kubwa zaidi la wananchi wa nchi hiyo, wakati ukiendelea kumchukulia mkuu wa serikali kuwa "mtu asiyeweza kuguswa wala kuwajibishwa," kwa upande mwingine unawatendea wanazuoni wakuu wa Kishia kwa matusi, kuwakamata na kuwavunjia heshima.

Sheikh Al-Shaala aliongeza kuwa; taarifa zilizochapishwa kuhusu mateso, matusi na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanazuoni wa Kishia walioko gerezani, pamoja na kuwasingizia "uongo na uzushi," ni ushahidi mwingine wa ukubwa wa ukiukwaji wa haki unaofanywa dhidi yao.

Alihoji: "Ikiwa hali ya viongozi na wanazuoni wakubwa wa madhehebu haya ndiyo hii, je, itakuwaje hali ya raia wa kawaida na maskini anayekamatwa, kupigwa, kudhalilishwa na kuteswa hadi kufikia ukingoni mwa kifo?"

Alisisitiza kuwa; katika Uislamu, heshima ya mwanadamu inajumuisha uhai wake, mali yake, heshima yake, utu wake na faragha yake. Hata hivyo, alisema heshima hizi zote leo zinavunjwa kwa mfumo uliopangwa, iwe kupitia uvamizi wa nyumba za watu, kuzitia hofu familia zao, kuzuia ibada na nembo za dini, au kwa kuwalenga wanazuoni na wafungwa.

Mwishoni mwa hotuba yake, Sheikh Al-Shaala alisisitiza kuwa; mwenendo wa utawala wa Bahrain unaonesha wazi kwamba "sheria inayotawala ni sheria ya msituni," ambapo raia huhesabiwa kuwa na hatia kabla ya kuthibitishwa kuwa ana kosa, alisema hali hiyo inapingana na misingi ya msingi kabisa ya sheria na kanuni ya Kiislamu, na akatoa wito wa kusitishwa kwa sera hizo, kuheshimiwa utu wa wananchi na kulindwa matukufu ya kidini na ya kibinadamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha