Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ujumbe wake, huju akidhihirisha heshima zake kwa Mara'jii Wakuu, wasomi, viongozi wa makabila na vijana wenye hamasa pamoja na wananchi wa Iraq kutokana na tukio lenye maana kubwa la kusindikiza mwili wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwenye Ataba Takatifu, ameeleza kuwa; mazishi hayo ya mamilioni ya watu na yasiyo na mfano ya Mbeba Bendera wa Muqawama yalikuwa ni dhihirisho kamili la mshikamano, undugu na msimamo mmoja kati ya mataifa mawili ya Iraq na Iran, aidha amesisitiza kuwa: Uwepo wa makumi ya mamilioni ya watu nchini Iran na Iraq kwa ajili ya mazishi na kumuaga Imam Mujahid Shahidi, Mwenyezi Mungu auinue daraja lake tukufu, umefungua ukurasa mpya wa mwamko na ushiriki wa wananchi katika kubadilisha mizani iliyotengenezwa na madola yenye kiburi.
Matini ya ujumbe wa Ayatullah Sayyid Mujtaba Khamenei ni kama ifuatavyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Tunawasilisha salamu, maamkizi, heshima na shukrani zetu nyingi kwa Mara'jii Wakuu, wanazuoni waheshimiwa, walimu na wanazuoni wa Hawza na vyuo vikuu, wanafikra na wasomi mashuhuri, viongozi wa makabila, masheikh wa koo, viongozi wa makundi mbalimbali, wananchi wema na wenye mapenzi, pamoja na vijana wenye hamasa na heshima wa kwenye ardhi iliyodhulumiwa ya Iraq.
Wananchi waumini wa Iraq, ambao wamebarikiwa kwa neema kubwa ya kuwa majirani na wenyeji wa Ahlul-Bayt (as) ndani ya Ataba Takatifu, wakiwa na historia angavu ya ustaarabu na wakinufaika na hazina ya kiroho na uongofu ya Hawza tukufu na kongwe ya Najaf Ashraf, pamoja na utendaji wao wa jihadi katika safu ya Muqawama, walimuandalia mapokezi Kiongozi Mkuu Shahidi, Mwenyezi Mungu auinue daraja yake tukufu, kwa namna iliyofanana na taifa la Iran, na hivyo wakaunda tukio kubwa, lenye maana na lililojaa majonzi na hisia za dhati.
Iraq, tangu siku ambayo nyayo zenye baraka za bwana wetu Amirul Muuminin (as) zilipokanyaga ardhi yake, imekuwa ardhi yenye baraka. Muda si mrefu baadaye, watu wake kwa fahari kubwa walivaa shingoni mwao mkufu wa mapenzi na uongozi (Wilayah) wa mtukufu huyo na wa wanawe watoharifu (as). Enzi za utawala wa madhalimu na watawala waovu juu ya ardhi hii hazikuweza kamwe kuondoa lulu safi ya Wilayah na mapenzi kwa Ahlul-Bayt watoharifu kutoka katika nyoyo za watu hawa, ndio maana baada ya kuanguka kwa utawala wa Baath, tukio kubwa la matembezi ya Arubaini lilitokea, na kwa kuwa lilitoka ndani kabisa ya nyoyo za watu hawa waumini, liliendelea kukua siku baada ya siku. Na kwa sababu hiyo hiyo, walipoona kuwa mwana aliedhulumiwa na shahidi wa Amirul Muuminin na Sayyidush Shuhadaa (as), baada ya miaka mingi ya kutokuwepo kwa dhahiri katika Ataba Takatifu, safari hii anakuja kuzunguka makaburi matukufu ukiwa ni mwili unaofanana na wa Hussein, mama yake na ndugu yake, walimkaribisha kwa moyo wao wote na wakakuheshimu kwa hali ya juu kufika kwake.
Kwa upande mwingine, mazishi haya ya mamilioni ya watu na yasiyo na mfano ya Mbeba Bendera wa Muqawama yalionesha kwa ukamilifu mshikamano, undugu na umoja wa msimamo kati ya mataifa mawili ya Iraq na Iran. Bila shaka viongozi wenye kiburi duniani walitazama kwa nyoyo zilizojaa hofu picha za mandhari za mkusanyiko huu mkubwa nchini Iraq, na wakaona jinsi uwekezaji wao mkubwa walioufanya kwa lengo la kuharibu uhusiano wa mataifa haya mawili ulivyogeuka kuwa bure na usio na athari yoyote. Uwepo huu wa makumi ya mamilioni ya watu nchini Iran na Iraq kwa ajili ya mazishi na kumuaga Imam Muja'hid Shahidi, Mwenyezi Mungu auinue daraja lake tukufu, umefungua ukurasa mpya wa mwamko na ushiriki katika kubadilisha mizania iliyotengenezwa na madola yenye kiburi.
Sasa Shetani Mkuu, Marekani mhalifu, imeelewa kwamba kuendelea kuwepo kwake katika eneo hili kwa urahisi na kwa mtazamo wa kutawala ni ndoto isiyowezekana.
Hivi karibuni, mikono iliyo wazi ya taifa tukufu la Iraq pamoja na makabila na koo zake zenye ukarimu na mapenzi itawakaribisha tena mamilioni ya mazuwari wenye shauku ya Ziara ya Arubaini, wakiwemo wale wengi watakaozuru kwa niaba ya Bwana Shahidi wa Iran. Kumbukumbu ya mazishi haya ya kifahari itaungana na kumbukumbu ya shujaa huyo ambaye huenda kwa miaka mingi alikuwa akitamani kupata fursa ya kufika katika Ataba Takatifu, hapo ndipo kaulimbiu yenye ukweli mkubwa isemayo: "حب الحسين يجمعنا" (Mapenzi ya Hussein yanatuunganisha) itaonekana wazi mbele ya watu wote, na Inshaallah, dua ya Bwana wetu (aj) kwa ajili ya usalama, baraka na maendeleo ya taifa la Iraq itapatikana; kwa fadhila na ukarimu Wake Mwenyezi Mungu.
Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei
2 Safar al-Mudhaffar 1448 H
26 Tir 1405 Sh
Maoni yako