Kwa mujibu wa Kitengo cha trajama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Abdul Mahdi Karbalai, mwakilishi wa Ayatullah Mkuu Sistani na msimamizi wa Kisheria wa Haram Tukufu ya Imam Hussein (as), alisema hayo katika hotuba yake mwishoni mwa hafla ya kuwapongeza na kuwashukuru wale waliowahudumia kwa juhudi kubwa wageni wa ziarah. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Hassan Rashid Jawad al-Abayiji, Mkurugenzi wa Haram ya Imam Hussein (as), wajumbe wa Bodi ya Uongozi, wakuu wa idara mbalimbali pamoja na idadi kubwa ya wafanyakazi wa Haram Tukufu ya Imam Hussein (as).
Alisisitiza kwamba; kumhudumia Imam Hussein (as) hakuishii katika kutekeleza majukumu ya kazi pekee, bali hukamilika kwa kushikamana kwa vitendo na njia ya Ahlul-Bayt (as), kutekeleza wajibu wa Kisheria na kuacha mambo yaliyoharamishwa. Pia alieleza kuwa hadhi ya kweli mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu hupimwa kwa uchamungu na utiifu, si kwa cheo cha kikazi au cha kiutawala.
Mwakilishi wa Ayatullah Sistani alisema kwamba; majlisi ambazo ndani yake hutajwa Mtume Mtukufu Muhammad (saww) na Ahlul-Bayt wake (as) zimejaa baraka nyingi, akirejelea riwaya zinazoeleza kuwamepo kwa Malaika katika majlisi hizo na namna zinavyonukia kwa kutajwa fadhila za Ahlul-Bayt (as), aliongeza kuwa; hata baada ya kumalizika kwa majlisi, athari ya utajo huo hubaki katika sehemu hiyo.
Akifafanua kwamba kushikamana na Ahlul-Bayt (as) ni mwendelezo wa kushikamana na Qur'ani Tukufu, alirejelea Hadithi ya Thaqalayn na kubainisha kuwa uongofu haupatikani kwa mapenzi pekee, bali kwa kufuata njia yao na kushikamana na mafundisho yao. Aidha, alisisitiza kwamba ardhi haitabaki tupu bila Hujjah wa Mwenyezi Mungu Mtukufu hadi Siku ya Kiyama.
Msimamizi wa Kisharia wa Haram ya Imam Hussein (as) aliongeza: Baada ya mafanikio yaliyopatikana katika siku kumi za mwanzo za mwezi mtukufu wa Muharram mwaka 1448 Hijria, tunatoa shukrani na pongezi zetu kwanza kwa Mkurugenzi wa Haram Tukufu ya Imam Hussein (as), Ustadh Hassan Rashid Jawad al-Abayiji, wajumbe wa Bodi ya Uongozi, viongozi wa idara na vitengo pamoja na wafanyakazi wote walioshiriki katika kufanikisha ziara hii. Tunathamini juhudi zao kubwa katika kuwahudumia mazuwari, ambazo ziliwezesha kutolewa kwa huduma za kipekee katika siku za ziara hii yenye baraka.
Sheikh Karbalai alisisitiza kwamba; heshima ya kuhusishwa na huduma kwa Imam Hussein (as) lazima iambatane na maarifa na kushikamana na mafundisho ya dini. Aliwataka wahudumu wote kuendelea kuhudhuria kozi za Fiqhi na mihadhara ya kielimu inayoongeza uelewa wao kuhusu hukumu za dini na njia ya Ahlul-Bayt (as), kwa sababu wao, zaidi ya wengine, wanastahili kuyadhihirisha maadili hayo katika mwenendo wao wa kila siku.
Aliendelea kusema: Kupandishwa ngazi katika majukumu ya kiutawala kunahusiana na utendaji wa kazi, lakini ubora mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu hupatikana kwa utiifu na uchamungu. Alieleza matumaini yake kwamba wafanyakazi wote wa Haram Tukufu ya Imam Hussein (as) wawe mfano bora wa Muumini aliyejitolea, na waendelee kutekeleza jukumu lao la kumhudumia Imam Hussein (as) kwa namna iliyo bora zaidi.
Mwishoni, Sheikh Karbalai alisema: Heshima hii tunayowapa leo kwa juhudi zenu, kukesha kwenu usiku na taabu mlizobeba katika kipindi hiki cha ziara, ni kutokana na mafanikio yenu katika kutekeleza majukumu mliyokabidhiwa. Hata hivyo, heshima na daraja la kweli katika nafasi mbalimbali hupatikana tu kwa kushikamana na kutekeleza wajibu wa Kisheria na kuacha yaliyoharamishwa. Kwa hiyo, tunawaomba muwe kioo kinachoakisi tabia na mwenendo wa Muumini mcha Mungu. Mwenyezi Mungu awajaalie mafanikio ya kutoa huduma bora zaidi katika ziara zijazo na awathibitishe katika heshima ya kumhudumia Imam Hussein (as).
Maoni yako