Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu chombo cha habari cha Mir'at al-Bahrain, kesi ya maulamaa 41 wa dini iliyoanza tangu mwezi Mei uliopita (Ordibehesht) ilianzishwa kwa taarifa na kampeni kubwa za kiusalama zilizotiwa chumvi, zilizotoa tuhuma zinazovuka mipaka ya nchi, kisha ikaendelea kwa ukimya mzito.
Baada ya yote hayo, sura halisi ya tukio imeanza kujitokeza, Maulamaa hao wa dini wamefungwa katika maeneo yasiyojulikana, wamezuiwa kufikiwa na dawa, nguo na mahitaji yao binafsi, mawakili wao wametishwia, na wao wenyewe wamezuiwa kuwasiliana na ndugu zao au kutembelewa.
Taswira halisi ni tofauti kabisa na simulizi rasmi, tunakabiliwa na amri ya kuzuiliwa kwa muda mrefu unaofikia miezi sita katika kesi inayowalenga maulamaa wa Kishia; watu wanaojulikana katika nyanja za hotuba za dini, uongozi wa kijamii na shughuli za wazi za kidini.
Hapa si simulizi la kugunduliwa kwa kundi la watu wenye silaha linalofanya kazi kwa siri, bali ni simulizi la kuigeuza jamii nzima ya kidini kuwa jukwaa la tuhuma, ambapo vipengele vya mashtaka ni khums, uwakilishi wa Kisheria, majlisi za dini, mahusiano baina ya maulamaa, na hata fedha za wake zao pamoja na vibubu vya watoto.
Namna ambavyo vyombo husika vimewashughulikia mawakili imefichua sehemu muhimu ya uhalisia wa kesi hii. Mawakili wengi walioteuliwa kuwatetea hawakuitwa kabisa kuhudhuria vikao vya mahojiano katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali; vikao vilivyofanyika wiki kadhaa baada ya maulamaa hao kushikiliwa na idara ya ujasusi.
Wale wachache walioweza kuhudhuria ni wale walioweza kujibu haraka kile kilichofanana na simu ya ghafla, kwani suala lote lilitegemea mlio mmoja wa simu kama uthibitisho kwamba wakili amealikwa. Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya mawakili kupinga utaratibu huo, lakini Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ikawajibu kwa kuwatishia kuwafikisha mbele ya Baraza la Nidhamu.
Hivyo ndivyo haki ilivyo katika mazingira ya sasa ya mamlaka: wakili anazuiwa kuhudhuria, mfungwa haruhusiwi kukutana na wakili wake, na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, ambayo ilipaswa kulinda uadilifu wa uchunguzi, inageuzwa kuwa sehemu ya vitisho.
Mawakili wale walioweza kuhudhuria mahojiano walitoka wakiwa na mshangao mkubwa; ushahidi unaowasilishwa dhidi ya maulamaa hao ni dhaifu kiasi cha kuaibisha.
Kilichompata Sheikh Jaafar Ashour kinatosha kuelewa mantiki ya vyombo vya usalama. Nchini Bahrain anajulikana kwa shughuli zake za kijamii, juhudi za kuimarisha familia na kuwaongoza wanandoa vijana, hata hivyo, matokeo ya mahojiano yanaonyesha kwamba alikamatwa kwa sababu katika hafla moja alimpongeza Sheikh Hani al-Bannaa kutokana na shughuli zake. Je, kumsifu mtu sasa ni ushahidi wa kuwa mwanachama wa kile kinachodaiwa kuwa shirika haramu?
Maswali yaliyoulizwa katika mahojiano pia yalifichua kina cha mgogoro wa kisheria. Baadhi ya maulamaa waliokamatwa waliulizwa ni wapi huswali, kisha wakaulizwa kuhusu tofauti kati ya Wilayah ya Imam Ali (as) na Wilayat al-Faqih.
Haya si maswali ya uchunguzi wa jinai kama inavyodaiwa, bali ni maswali ya kuchunguza na kuhukumu imani za kidini. Mamlaka hapa haitafuti kitendo cha jinai kinachotambulika kisheria, bali inajaribu kuivunja imani ya jamii nzima ili baadaye iitumie ksma kosa la jinai.
Leo, kila kitu kinachofanyika katika mazingira ya kidini ya Kishia kinaweza kugeuzwa kuwa ushahidi wa uhalifu: majlisi, hotuba, khums, marjaiya, mahusiano ya kijamii au misaada ya kifedha.
Hata mali zilizochukuliwa kutoka katika nyumba za maulamaa zilitaifishwa bila kutenganisha kati ya fedha zinazomilikiwa na waliokamatwa na zile zinazomilikiwa na familia zao. Hata vibubu vya watoto wao na vifaa vya kielektroniki vilivyokuwa vinatumika kwa masomo havikusamehewa; vyote viliwekwa chini ya shtaka moja.
Jambo linalowatia wasiwasi wachunguzi ni kwamba hatua za kimahakama hazikuanza kwa ushahidi, bali zilianza kwa hotuba ya Waziri wa Mambo ya Ndani. Mazingira ya kesi hii hayafanani na uchunguzi wa kimahakama, bali yanafanana zaidi na uamuzi wa kisiasa unaotafuta baadaye msingi wa kisheria. Waziri wa Mambo ya Ndani alitoa simulizi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inajenga simulizi hilo, na majaji baadaye watajaribu kuligeuza kuwa hukumu zilizopangwa tayari ili kukidhi kiu ya kuadhibu au kulipiza kisasi.
Hata hivyo, jambo linalozitia hofu familia za maulamaa hao waliotekwa nyara ni kutokujulikana mahali walikowekwa na mazingira wanayoishi. Je, wanashikiliwa katika Idara ya Upelelezi wa Jinai? Au katika majengo ya Idara ya Usalama wa Taifa? Au wamehamishiwa katika Jengo Na. 15 la Gereza Kuu la Jaw, jengo ambalo hivi karibuni limehusishwa na kifo cha mfungwa aliyefariki baada ya kuteswa?
Mwenendo wa kesi hii ya maulamaa unaiweka sheria ya Bahrain katika mtihani mkubwa kuhusu maana yake halisi. Tunakabiliwa na mfumo ambao hautafuti ukweli, bali unalazimisha simulizi lake kwa nguvu.
Kwa mujibu wa yanayofichuliwa nyuma ya pazia, kesi hii haiwakilishi operesheni ya shirika la usalama pekee, bali ni kielelezo cha juhudi za kudhibiti mazingira ya dini ya Kishia, ni ujumbe mkali kwa kila mwanazuoni na mhubiri kwamba dini ambayo haiendani na mtazamo wa mamlaka inaweza wakati wowote watakapopenda kuvikwa joho la usaliti.
Maoni yako