Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Maulana Sheikh Hemed Jalala alitoa wito huo jana wakati akihutubia waumini katika Msikiti wa Ghadeer uliopo Kigogo Post, jijini Dar es Salaam, katika moja ya majlisi za maombolezo ya mwezi mtukufu wa Muharram.
Katika hotuba yake, Sheikh Jalala aliwaelekeza vijana kuwa makini na taarifa wanazokutana nazo kwenye mitandao ya kijamii, huku akisisitiza umuhimu wa kupima mambo kwa mizani ya akili, elimu na mwongozo wa Qur’ani Tukufu.
Mkurugenzi huyo wa Hawza ya Imam Sw'adiq (as) alisema: “Katika mitandao ya kijamii kumejaa mambo mengi; yapo yanayofaa na yapo yasiyofaa, pale palipo na haki, ni wajibu wetu kuifuata, na pale palipo na batili, tunapaswa kuikataa na kuepukana nayo,”.
Sheikh Jalala alibainisha kuwa: Qur’ani Tukufu imewataka wanadamu mara nyingi kutumia akili zao katika kutafakari na kufanya maamuzi sahihi, aliashiria aya mbalimbali za Qur’ani tukufu zinazosisitiza umuhimu wa kufikiri, kuchunguza na kuchagua njia ya haki, zikiwemo aya kama vile: Suratul Kahf (18:29), Fussilat (41:40), At-Tawbah (9:105), Al-Muddathir (74:37), Abasa (80:12), Al-Muzzammil (73:19), An-Naba’ (78:39) na Al-An‘am (6:148).
Aidha, aliwataka vijana kuepuka kufuata mitazamo kwa upofu au kusikiliza propaganda dhidi ya madhehebu mbalimbali bila kufanya utafiti wa kina katika madhehebu husika.
Katika kulisisitiza hilo alisema: “Msikubali kuambiwa tu kwamba hawa ni Mashia, hivyo msisome vitabu vyao. Ikiwa mnataka kuijua haki, someni vitabu vya Kishia vyenyewe, si vitabu vya maadui wa Uashia vinavyouzungumzia Ushia, baada ya kufanya utafiti na kufahamu yaliyomo, ndipo mtoe hukumu au mjibu kwa hoja”.
Vilevile, Sheikh Jalala aliwahamasisha vijana kutembelea misikiti na vituo vya elimu vya mashia kwa lengo la kujifunza na kujionea ukweli wenyewe, badala ya kutegemea taarifa za kusimuliwa au zinazotolewa na watu wenye misimamo ya chuki dhidi ya Ushia.
Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho matumizi ya mitandao ya kijamii yanaendelea kuongezeka kwa kasi, hali inayofanya umuhimu wa kutumia akili, elimu na uchunguzi wa kina kuwa jambo la msingi katika kuijenga jamii yenye ufahamu sahihi na uwezo wa kutofautisha kati ya haki na batili.
Maoni yako