Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Yasin Mousawi, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad na mmoja wa walimu mashuhuri wa Hawza ya Najaf Ashraf, katika khutba zake za Swala ya Ijumaa za tarehe 22 Khordad 1405 H.Sh., alizungumzia masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kikanda, na kusisitiza kwamba: “Mgogoro wa kina zaidi unaoikabili Iraq leo hauishii katika maelezo ya matatizo ya huduma za jamii na uchumi pekee, bali ni kukosekana kwa mtazamo wa kisiasa unaojengwa juu ya msingi wa nchi kujitegemea, ambao unaweza kulinda uhuru wa maamuzi ya nchi.”
Alionya kuhusu juhudi zinazofanywa ili kuhalalisha na kueneza utamaduni wa utegemezi, pamoja na kuwapandikiza wananchi fikra kwamba mustakabali wa serikali na maamuzi ya Iraq unategemea matakwa ya madola ya kigeni.
Alisema: “Baadhi ya vyombo vya habari vinajaribu kuonesha uundwaji wa serikali za Iraq kana kwamba unafanyika moja kwa moja kwa kufuata maagizo ya serikali ya Marekani, jambo la msingi si maelezo ya namna viongozi wanavyochaguliwa, bali ni kukataa kwa dhati aina yoyote ya kujisalimisha mbele ya mashinikizo na maagizo ya kigeni, kutoka upande wowote ule.”
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad aliongeza kuwa: “Wananchi wa Iraq wanapaswa kutambua kwamba wana haki ya kuishi katika nchi yenye mamlaka kamili ya kitaifa, na kwamba kiongozi wa Iraq anapaswa kuwa huru katika maamuzi yake, si kuwa mtekelezaji wa matakwa ya Marekani, utawala wa Kizayuni au nchi nyingine yoyote.”
Alisisitiza kwamba: “Utamaduni wa uhuru wa kitaifa unapaswa kupewa kipaumbele hata kabla ya madai ya huduma za kijamii na mahitaji ya maisha, kwa sababu kupoteza mamlaka ya kitaifa maana yake ni kupoteza uwezo wa kuamua mustakabali wa nchi.”
Ayatullah Mousawi alibainisha: “Wananchi wa Iraq wanapaswa kulitanguliza suala la Nchi kujitegemea kuliko jambo lolote jingine, na kabla ya kudai kuboreshwa kwa huduma au haki za maisha bora, wanapaswa kutetea haki yao ya kushiriki kwa dhati katika uongozi wa nchi; kwa sababu raia wa Iraq hapaswi kuwa mtu wa kutekeleza tu maamuzi yanayolazimishwa kutoka nje ya nchi.”
Alieleza kwamba; kuimarisha uelewa huu kwa umma ndiyo dhamana kuu ya kujenga taifa lenye nguvu na uwezo wa kutetea maslahi ya wananchi wake.
Kurejelea Uzoefu wa Iran katika Kulinda Uhuru Wake
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad aliendelea na hotuba yake kwa kurejelea uzoefu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: “Kutaja uzoefu huu hakumaanishi utegemezi wa kisiasa, bali ni kutumia uzoefu wa taifa ambalo limeweza kuhifadhi uhuru wake mbele ya mashinikizo mbalimbali.”
Aliongeza: “Wananchi wa Iran, licha ya matatizo ya kiuchumi na madai ya kuboreshwa kwa maisha, walipohisi kwamba mamlaka na uhuru wa nchi yao uko katika hatari, waliinuka kwa pamoja kutoka makundi mbalimbali ya jamii ili kuitetea nchi yao na mfumo wao wa utawala, na wakalitanguliza suala la uhuru wa kitaifa kuliko masuala mengine ya pembeni.”
Ayatullah Mousawi alisema: “Ni uelewa huu uliowafanya wananchi wa Iran kusimama imara mbele ya aina yoyote ya uvamizi au tishio dhidi ya uhuru wa nchi yao. Taifa la Iraq pia linahitaji kurejea katika aina hii ya ufahamu wa kitaifa.”
Aidha, akirejelea uwezo wa kihistoria wa wananchi wa Iraq, alisema: “Watu wa Iraq wana historia ndefu ya uelewa na ushujaa.”
Katika muktadha huo, alitaja kauli ya shahidi Sayyid Muhammad Baqir al-Hakim kuhusu mtazamo wa Imam Khomeini (r.a), ambapo Imam Khomeini kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alikuwa na imani kwamba; taifa la Iraq lina uwezo wa kuanzisha mfumo huru wa utawala chini ya uongozi wa Marjaiyya ya dini.
Maoni yako