Jumapili 7 Juni 2026 - 12:20
Imam Khomeini (r.a), alikuwa nembo ya mwamko na mapambano dhidi ya ubeberu

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi katika ujumbe wake amesema: Imam Khomeini (r.a) kupitia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwasilisha mfano wenye mafanikio wa serikali ya kidini na akawaonesha walimwengu njia ya heshima, uhuru na kusimama imara dhidi ya ubeberu.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia wa Pakistan, katika ujumbe wake wa kuadhimisha kumbukumbu ya miaka thelathini na saba tangia kuaga dunia mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza: Imam Khomeini (r.a) hakulikomboa tu taifa la Iran kutoka kwenye makucha ya mfumo fisadi na wa kidikteta wa kifalme, bali pia alisimama kama taa yenye kung'aa katikati ya giza la dunia ya kisasa na kuonesha njia ya uhuru, kujitegemea na heshima kwa mataifa ya Kiislamu na wanyonge duniani.

Katika ujumbe huu imeelezwa: Imam Khomeini (r.a) alikuwa mmoja wa watu mashuhuri zaidi wa kielimu na kimapinduzi katika ulimwengu wa Kiislamu ambaye kwa kutumia elimu, uelewa, mtazamo wa kina wa kidini na uwepo wa vitendo katika medani, aliweza kuwaongoza Waislamu katika njia sahihi, yeye kupitia uongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwasilisha kwa walimwengu taswira halisi, hai na bora ya Uislamu na akaonesha mfano wa vitendo wa serikali inayojengwa juu ya maadili ya Kiislamu; mfano ambao athari na baraka zake bado zinaonekana katika ulimwengu mzima wa Kiislamu.

Ameongeza: Leo tunaadhimisha kumbukumbu ya miaka thelathini na saba tangia kuaga dunia Imam Khomeini (r.a) katika hali ambayo maadui wa Uislamu, hasa Wazayuni na Mabeberu wa kimataifa, wamefanya juhudi nyingi za kupambana na mkondo wa Mapinduzi ya Kiislamu, wao walidhani kwamba; kwa kumuua kishahidi Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye alikuwa akiendeleza njia na fikra za Imam marehemu, wangeweza kuzuia kuenea na ushawishi wa Mapinduzi ya Kiislamu, lakini kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, mapinduzi haya bado yanaendelea kwa nguvu, heshima na uchangamfu katika njia yake na malengo yake yameendelea kuwa hai na yenye kuhamasisha.

Mwanachuoni huyu mashuhuri wa Pakistan, akirejelea sifa za kimaadili na kielimu za Imam Khomeini (r.a), ameeleza: Imam marehemu kwa kuongozwa na mwenendo na njia za Mitume wa Mwenyezi Mungu, alikusudia kuamsha vipaji, maadili ya kiroho na uwezo uliojificha ndani ya wanadamu, tangu mwanzo wa harakati zake mpaka dakika za mwisho za maisha yake matukufu, daima alikuwa katika medani ya vitendo na kama mrekebishaji mkubwa wa kijamii na kidini alibeba jukumu la kuiongoza jamii.

Aiendelea kukumbusha kuwa: Imam Khomeini (r.a) kupitia uongozi wake wa hekima na malengo ya juu ya Mwenyezi Mungu aliliongoza taifa kubwa la Iran kuelekea heshima, uhuru na kujitegemea, na alitekeleza majukumu yake mazito kwa namna bora kabisa, maisha yake yenye thamani na yaliyojaa juhudi yanafikisha ujumbe kwa mataifa kwamba; kwa kuimarisha roho ya kujiamini, nia ya mabadiliko na kusimama dhidi ya ubeberu, inawezekana kushirikiana na njama za madola ya kiistikbari kushindwa na kuweka mazingira ya maendeleo na utukufu wa mataifa.

Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia wa Pakistan katika sehemu nyingine ya ujumbe wake alisisitiza: Ukubwa wa shakhsia ya Imam Khomeini (r.a) hauishii katika kuongoza Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran tu, yeye pamoja na kulikomboa taifa la Iran kutoka katika mfumo wa zamani, fisadi na tegemezi wa kifalme, pia alijitokeza katika kiwango cha kimataifa kama mwenge unaotoa mwanga na msukumo; mwenge ambao katika giza la zama za utawala wa mabavu na kiburi uliangaza nuru ya matumaini, uhuru na kujitegemea.

Ameongeza kuwa: Katika kipindi hicho watu wachache walikuwa wakidhani kwamba harakati huru zingeweza kuundwa nje ya mfumo wa nguvu za Mashariki na Magharibi na kufikia ushindi.

Lakini Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa kaulimbiu yake ya kudumu “Si Mashariki wala Magharibi” yaliweza kubadilisha mlinganyo huo na kuutambulisha ulimwengu mfano mpya wa uhuru wa kisiasa, kitamaduni na kidini; mfano ambao bado unaendelea kwa mafanikio katika njia yake.

Rais wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia wa Pakistan pia huku akirejelea mafanikio ya fikra na kisiasa ya Imam Khomeini (r.a) alisema: Baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa Kiislamu uliojengwa juu ya fikra za Imam marehemu, propaganda nyingi na hofu zilizokuwa zikienezwa kuhusu kutoweza Uislamu kuongoza jamii na serikali zilipoteza nguvu na uhalali wake. Imam Khomeini (r.a) kupitia kuwasilisha nadharia ya Wilayatul Faqih na kuanzisha serikali ya Kiislamu, alithibitisha kwa vitendo kwamba Uislamu si dini ya ibada pekee, bali ni mfumo kamili wa kuendesha maisha ya binafsi na kijamii ya wanadamu katika nyanja zote.

Amesisitiza: Uzoefu wenye mafanikio wa Jamhuri ya Kiislamu umeonesha kwamba; Uislamu una mipango na njia za utatuzi kwa nyanja zote za maisha, kuanzia siasa na uchumi hadi utamaduni, uadilifu wa kijamii na mahusiano ya kimataifa, kwa sababu hiyo mataifa na jamii mbalimbali zinaweza kwa kutumia fikra na mafundisho ya Imam Khomeini (r.a), kujifunza njia za kupambana na dhulma, ukoloni na ukosefu wa haki na kuweka mazingira ya ukombozi wa wanyonge na wanaodhulumiwa duniani.

Mwisho, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi amesisitiza kwa kusema: Shakhsia, fikra na urithi wa Imam Khomeini (r.a) bado ni chanzo cha msukumo kwa mataifa huru duniani, na kadiri muda unavyopita, nyanja mbalimbali za fikra na harakati zake zinaendelea kujitokeza wazi zaidi. Leo pia ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kufikia heshima, umoja, uhuru na uadilifu unahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote kutumia mafundisho na malengo ya kiongozi huyo mkubwa wa Mwenyezi Mungu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha