Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Abdul-Malik Badruddin al-Houthi, kiongozi wa Ansarullah ya Yemen, alieleza kwa kina kuhusu kutangazwa kwa “haki ya Wilayah” kwa Imam Ali (as) na amri ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume Muhammad (saww) ya kuitangaza katika “Ghadir Khum”.
Kiongozi wa Ansarullah katika hotuba yake kwa mnasaba wa kuhuisha Siku ya Wilayah ya mwaka 1447 Hijria alifafanua kwamba; uzito na unyeti wa suala hili katika mazingira ya watu wa wakati huo ulikuwa mkubwa sana, hili linaonekana katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema:
﴿وَاللَّهُ یَعْصِمُکَ مِنَ النَّاسِ﴾
“Na Mwenyezi Mungu atakulinda dhidi ya watu.”
Kwa kuzingatia kwamba suala la Wilayah na uongozi wa mambo ya Umma ni miongoni mwa masuala nyeti zaidi katika tabaka na makundi mbalimbali ya kijamii, kuanzia wanasiasa, wanafikra hadi wanazuoni.
Alieleza kwamba; kinachodhihirisha zaidi umuhimu wa tangazo hili ni muda wake, kwa kuwa lilifanyika katika siku za mwisho za maisha ya Mtume (saww), baada ya Qur’ani kuwa tayari imewasilisha itikadi, hukumu na misingi muhimu ya dini, alifafanua kwamba kushuka kwa aya tukufu:
﴿یَا أَیُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنْزِلَ إِلَیْکَ مِنْ رَبِّکَ وَإِنْ لَمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ﴾
“Ewe Mtume! Fikisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako; na ikiwa hutafanya, basi hujafikisha ujumbe Wake.”
Kunadhihirisha nafasi ya jambo hili na athari yake ya msingi katika mwenendo wa risala na mustakabali wa Umma.
Sayyid al-Houthi aliongeza kwamba; Mtume Mtukufu (saww), mara tu baada ya kushuka kwa aya hiyo, alichukua hatua za kipekee kwa ajili ya kutangaza ujumbe huo. Hivyo aliamuru mahujaji wakusanyike katika eneo la “Ghadir Khum”, na akaagiza wale waliokuwa wametangulia warejee nyuma na waliokuwa wamebaki nyuma waharakishe kufika, licha ya ukali wa joto na kukaribia muda wa adhuhuri, pia eneo la mkusanyiko liliandaliwa, na mimbari ilitengenezwa kwa vifaa vya kupandia ngamia ili atoe hotuba.
Kiongozi wa Ansarullah aliendelea kusema: Katika eneo hilo, mkusanyiko mkubwa wa Waislamu uliundwa, na Mtume (saww), baada ya kumaliza Swala ya Adhuhuri, alipanda mimbari akiwa pamoja na Imam Ali (as), kisha alianza hotuba ambayo ndani yake alikumbusha tena kuhusu kukaribia kwa kufariki kwake duniani, na akaitaja “Hadith al-Thaqalayn” kama utangulizi unaolingana na uzito na msingi wa tangazo lililokuwa linafuata.
Kuhusu maudhui ya hotuba hiyo, Sayyid al-Houthi alieleza kwamba Mtume (saww) alitangaza wazi Wilayah ya Amirul-Muuminina Ali (as) kwa kusema:
(یا أیها الناس إن الله مولای وأنا مولی المؤمنین أولی بهم من أنفسهم، فمن کنت مولاه فهذا علی مولاه)
“Enyi watu! Hakika Mwenyezi Mungu ni kiongozi wangu, na mimi ni kiongozi wa Waumini, na nina haki zaidi juu yao kuliko nafsi zao wenyewe. Basi yeyote ambaye mimi ni kiongozi wake, huyu Ali ni kiongozi wake.”
Kisha alishika mkono wa Imam Ali (as) na kuuinua mbele ya mkusanyiko wa watu na kuomba:
(اللهم والِ من والاه، وعادِ من عاداه، وانصر من نصره، واخذل من خذله)
“Ewe Mwenyezi Mungu! Mpende anayempenda, na mfanyie uadui anayemfanyia uadui, na mnusuru anayemnusuru, na mdhalilishe anayemdhalilisha.”
Pia alieleza kwamba Mtume Mtukufu (saww) ili kukamilisha hoja aliwauliza waliokuwepo:
"Je, nimefikisha?"
Na walipojibu:
"Ewe Mwenyezi Mungu, ndiyo."
Akasema:
"Ewe Mwenyezi Mungu, basi shuhudia."
Na akawapa jukumu la kufikisha ujumbe huo kutoka kwa waliokuwepo kwenda kwa wasiokuwepo ili upeo wake uenee na uhusishe Umma wote.
Katika muktadha huo, Sayyid al-Houthi alifafanua kwamba aya tukufu:
﴿الْیَوْمَ أَکْمَلْتُ لَکُمْ دِینَکُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَیْکُمْ نِعْمَتِی وَرَضِیتُ لَکُمُ الْإِسْلَامَ دِینًا﴾
“Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimewatimizieni neema Yangu na nimeridhia Uislamu kuwa dini yenu.”
ilishuka baada ya kutangazwa kwa ujumbe huo, na akaeleza kwamba; ukamilifu wa dini na kutimia kwa neema haviwezi kueleweka mbali na tukio hili, ambalo alilielezea kuwa ni hatua muhimu ya kihistoria katika maisha ya Umma.
Alisisitiza kwamba; umuhimu wa tangazo hili ni kwamba; liliuchorea Umma wa Kiislamu njia iliyo wazi na yenye uhakika kwa ajili ya mustakabali wake, na baada ya kufariki Mtume Mtukufu (saww), liliwapatia dhamana kuu ya mustakabali wa Umma, aliongeza kwamba; ikiwa Umma utabaki kushikamana na njia hii, utakuwa na ukamilifu wa Uislamu katika uhalisia wa maisha yake na utafaidika na matunda yake makubwa katika nafsi na maisha yao; kwa sababu Uislamu ni dini ambayo athari zake huonekana katika kuinua hadhi ya mwanadamu na katika nyanja mbalimbali za maisha, pamoja na yale ambayo Mwenyezi Mungu ameahidi duniani na Akhera.
Kiongozi wa Ansarullah alibainisha kwamba; tangazo la “Ghadir Khum” halikuwa tukio lililojitenga na muktadha wa jumla wala misimamo iliyo wazi ambayo ilithibitisha nafasi ya Amirul-Muuminina Imam Ali (as); bali tangazo hili lilikuwa taji ya mfululizo wa matamko ya kinabii yaliyopokewa kwa njia ya mutawatir yaliyokuwa yameainisha daraja lake, miongoni mwa matamko hayo muhimu zaidi ni kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) kwa Imam Ali (as):
"Wewe kwangu una nafasi sawa na Harun kwa Musa, isipokuwa hakuna Nabii baada yangu."
Pia kuna hadithi zinazomfungamanisha na haki na Qur'ani, kama vile:
"Ali yuko pamoja na Qur'ani na Qur'ani iko pamoja na Ali,"
na:
"Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali."
Zaidi ya hayo, yeye ni kipimo cha imani, kama ilivyokuja katika kauli yake:
"Hakupendi isipokuwa Muumini, na hakuchukii isipokuwa mnafiki."
Pamoja na dalili nyingine nyingi madhubuti zinazokubalika miongoni mwa Waislamu.
Pia alifafanua kwamba; tangazo hili lina mizizi muhimu ndani ya Qur'ani Tukufu na katika idadi ya aya tukufu, hasa zile zilizopo katika Suratul-Maida, alisisitiza umuhimu wa kuelewa suala hili ndani ya muktadha wa Qur'ani, dalili zake na maana zake ambazo zina uhusiano na hali halisi ya Umma na changamoto zake.
Alibainisha kwamba; muktadha huu una umuhimu wa pekee katika kipindi cha sasa, akaeleza kuwa Waislamu katika vipindi mbalimbali walihitaji kulielewa suala hili na kufahamu vipengele vyake, lakini hitaji hilo limeongezeka mara mbili kutokana na mazingira na changamoto zinazoukabili Umma leo, alisisitiza kwamba; kushikamana na tangazo la kihistoria la Siku ya Ghadir kungeliulinda Umma dhidi ya hali iliyopo sasa ya mgawanyiko na kurudi nyuma, pamoja na yale unayokabiliana nayo leo dhidi ya maadui wake, yaani Mayahudi na Wakristo, pia alieleza kwamba; Qur'ani Tukufu imezungumzia suala la Wilayah kwa namna iliyo wazi na ya moja kwa moja katika Suratul-Maida.
Sayyid al-Houthi alinukuu kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
﴿إِنَّمَا وَلِیُّکُمُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ وَالَّذِینَ آمَنُوا الَّذِینَ یُقِیمُونَ الصَّلَاةَ وَیُؤْتُونَ الزَّکَاةَ وَهُمْ رَاکِعُونَ﴾
"Hakika kiongozi wenu ni Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wale walioamini, ambao husimamisha Swala na hutoa Zaka wakiwa katika rukuu."
Na aliichukulia aya hii kuwa ni uthibitisho wa Qur'ani juu ya suala la Wilayah ambalo limewasilishwa kama jambo la msingi katika mwenendo na mustakabali wa Umma.
Kiongozi wa Ansarullah alifafanua kwamba; matini ya Ghadir Khum inaambatana na matini hii tukufu ya Qur'ani na ndiyo inayoiweka wazi maana yake, alieleza kwamba; uongofu wa Mwenyezi Mungu katika suala la Wilayah uliendelea baadaye katika kauli Yake:
﴿وَمَنْ یَتَوَلَّ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَالَّذِینَ آمَنُوا فَإِنَّ حِزْبَ اللَّهِ هُمُ الْغَالِبُونَ﴾
"Na yeyote anayemfanya Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na Waumini kuwa viongozi wake, basi hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo litakaloshinda."
Alisisitiza kwamba; muktadha wa Qur'ani ambapo suala la Wilayah limekuja unafichua umuhimu wake mkubwa na unaonyesha nafasi yake katika kujenga hali ya Umma na kuilinda dhidi ya hatari na changamoto, pamoja na matokeo na athari za kushikamana nayo katika kiwango cha nguvu, heshima na ushindi.
Sayyid al-Houthi alisisitiza kwamba; Qur'ani Tukufu imeonya waziwazi dhidi ya kuwafanya Mayahudi na Wakristo kuwa viongozi wa karibu, akitoa ushahidi kwa kauli ya Mwenyezi Mungu:
"Msiwafanye Mayahudi na Wakristo kuwa viongozi wenu; baadhi yao ni viongozi wa baadhi yao, na yeyote miongoni mwenu atakayewafanya wao kuwa viongozi wake, basi huyo ni miongoni mwao."
Alifafanua kwamba; muktadha huu unaonyesha ulazima wa kupambana nao kama upande ambao ni hatari ya kweli kwa Umma wa Kiislamu na ambao unajaribu kuushambulia kwa uadui wa pande zote.
Kiongozi wa Ansarullah alisema kwamba: Qur'ani Tukufu imezungumzia juhudi za maadui wa Umma za kuugeuza Umma kuwa Umma uliopotea na ulioachwa, kuunyang'anya heshima ya kubeba ujumbe wa Mwenyezi Mungu, na kuugeuza kuwa Umma wa watumwa, ulioshindwa na uliodhalilika.
Alibainisha kwamba; aya za Qur'ani zimeweka wazi tabia ya mienendo yao ya uvamizi, mbinu zao za kupotosha, kudanganya, kuharibu na kudhoofisha, pamoja na hatari ya mradi wao dhidi ya Umma wa Kiislamu, alisema kwamba; msingi wa Wilayah katika Uislamu ni nguzo muhimu katika kuufanya Uislamu uwe na ufanisi katika maisha ya Waislamu na katika kutimia kwa matunda na ahadi za Mwenyezi Mungu duniani na Akhera. Aidha alisisitiza kwamba miongoni mwa matokeo muhimu zaidi ya msingi huu ni kuuilinda Umma dhidi ya Wilayah ya maadui wake, yaani Mayahudi, Wakristo na mawalii wa Shetani.
Maoni yako