Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul Islam Sheikh Salah Al-Karbalaei, Khatibu wa Swala ya Idi ya Adh-ha huko Karbala Tukufu, katika khutba za Swala ya Idi zilizofanyika katika eneo la Bainal-Haramain, alisisitiza kuwa; misimamo ya taifa la Iraq katika mazingira magumu ni dhihirisho la uhalisia wa mshikamano kwa taifa lao na mwitikio unaostahili kwa wito wa Marjaiyya ya juu ya kidini.
Alisema kuwa: Miongoni mwa mambo muhimu zaidi yanayoweza kutajwa katika siku hizi ambazo Umma wa Kiislamu hususan watu wetu watukufu wanakabiliwa na shida na migogoro mikubwa, majonzi ya kuwapoteza wapendwa wao, kutowezekana kwa kuzikwa baadhi ya miili hadi leo, kuhama kutoka makazi yao na madhara yenye uchungu yanayotokana na hali hiyo, ni misimamo yenu ya heshima na kishujaa. Misimamo hii inaonesha uhalisia wa mshikamano wenu safi na wenye baraka pamoja na mwitikio wenu wa heshima kwa wito wa Marjaiyya ya juu ya kidini huko Najaf Tukufu; kiasi cha kwamba; misimamo yenu, dua zenu, hisia zenu na msaada wenu vinaendelea kuwa chanzo cha fahari na kujivunia.
Khatibu wa Swala ya Idi ya Adh-ha aliongeza kusema: Taifa letu lenye heshima ni shule iliyojaa mafunzo na mazingatio ya vitendo; huenda baadhi ya viongozi wakajifunza kutoka katika shule hii kubwa na kupata sehemu na mafanikio katika njia ya mageuzi, ujenzi na kupunguza mizigo iliyoko mabegani mwa watu wasiojiweza pamoja na vijana, taifa letu linastahili mema yaliyo bora zaidi na daima limekuwa tayari kujitolea, kuzilea nafsi na kutoa kwa ukarimu.
Dunia ni nyumba ya kupita, si makazi ya milele wala sehemu ya kudumu; ni makazi ya kutoweka na kuporomoka ambayo daima yanabadilika, anayedanganywa ni yule ambaye dunia imemdanganya, na mwenye mashaka ni yule ambaye fitna zake zimemshughulisha.
Sheikh Al-Karbalaei alihitimisha khutba zake kwa kusema: Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atujaalie uongofu mwema ambao hatutauuza kwa kitu chochote, atuthibitishe katika njia ya haki ili tusipotoke humo, na atujalie nia iliyokomaa ambayo haitakuwa na shaka ndani yake.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu aishike mikono yetu na atuongoze kuyaelekea yale anayoyapenda na kuyaridhia, atupe tawfiq ya kutenda matendo yaliyo safi zaidi na yenye kupendeza zaidi, atuthibitishe katika njia ya haki, na atufanye sote kuwa miongoni mwa wale watakaokufa na kufufuliwa juu ya dini yake.
Maoni yako