Jumatano 27 Mei 2026 - 13:30
Lengo la Serikali ya Bahrain ni Kuondoa Madhehebu ya Shia Nchini Bahrain

Hawza/ Jumuiya ya Kiislamu ya Al-Wefaq ya Taifa la Bahrain imesisitiza kwamba; juhudi za utawala wa Bahrain za kuonyesha ibada na nembo za dini kuwa ni vitendo vya uhalifu, pamoja na kuhusisha tuhuma dhidi ya madhehebu ya Ja‘fari, ni hatua ya kimadhehebu na isiyo na uhalali wowote.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Jumuiya ya Kiislamu ya Al-Wefaq ya Taifa la Bahrain, ambayo ipo katika safu za wanamapinduzi wa Bahrain, imesisitiza kwamba; juhudi za utawala wa Bahrain za kuhalalisha uhalifu dhidi ya nembo za kidini zenye historia ya miaka 1400 zinazohusiana na utoaji wa haki za kisheria za Kiislamu, pamoja na kuhusisha tuhuma zinazoyafanya madhehebu ya Ja‘faria kuonekana kuwa ni ya kihalifu, ni hatua ya kimadhehebu na isiyo na uhalali.

Jumuiya hiyo ilisema katika taarifa yake kwamba; hali hii inaonesha mgogoro wa kiuongozi ambao umegeuza mamlaka na taasisi zote za nchi kuwa vyombo vya kuhalalisha uhalifu dhidi ya uwepo wa Mashia nchini Bahrain. Aidha, kufanya moja ya matawi ya dini kwa mujibu wa Mashia kuwa kosa la jinai, kupitia unyakuzi wa mamlaka kwa nguvu na kiburi, kunaingia katika mfumo wa adhabu ya pamoja inayotolewa kwa misingi ya madhehebu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa; jambo hilo linafanyika sambamba na kuwafanya raia wa Kishia kuwa dhaifu kwa kuwabagua, kuwapeleka pembezoni mwa jamii, na kuondoa uwakilishi wao katika muundo wa dola kwa njia ya kimfumo na iliyopangwa kwa muda mrefu.

Jumuiya ya Al-Wefaq iliongeza kuwa; kukamatwa kwa wanazuoni walioko mstari wa mbele katika shughuli za kidini, wahubiri wakuu, pamoja na wasomi wanaofanya kazi katika nyanja za kidini kutoka maeneo yote ya Bahrain, na pia wawakilishi wa maraji' wote wa Kishia, ni hatua ya uadui dhidi ya uwepo mzima wa Mashia bila ya kuwa na sababu yoyote au msingi wa kisheria.

Kwa mujibu wa Al-Wefaq, hatua hiyo ni jaribio la kuwafanya wahalifu kwa sababu tu ya kushikamana kwao na itikadi zao pamoja na ibada na mila zao za kidini na kijamii; jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa katika historia ya Bahrain wala katika tawala za nchi nyingine za Kiislamu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa; kinachotokea Bahrain kinaendeshwa kupitia mkusanyiko wa vyombo vya serikali kwa namna ya wazi kabisa ya kisiasa, kisheria, kiutendaji na kimahakama, kiasi kwamba taasisi zote hizo zinafuata maagizo ya pamoja na yaliyoratibiwa. Pia vyombo vya habari vya serikali vinatumika kueneza uongo, kuchochea chuki, uchochezi na kuongeza uhasama ili kuhalalisha hatua hizi za kulenga kundi fulani.

Al-Wefaq ilisisitiza kwamba; kile ambacho Bahrain inashuhudia siku hizi, kuanzia kuongezeka kwa mashinikizo na ulengaji maalumu hadi tabia zisizo na mipaka na wazimu wa kimadhehebu usio na mfano, hufanyika bila ya sababu yoyote ya ndani na kuunda historia hatari yenye lengo la kuwatisha na kuwaogopesha raia wa Kishia ili waache kutekeleza ibada na nembo zao za kidini.

Jumuiya hiyo ya Kiislamu ilionya kwamba; kuendelea kuendesha nchi kwa mtazamo wa kimadhehebu unaotegemea ukandamizaji na vitisho, pamoja na kutenga na kuondoa uwepo wa kundi kubwa na la asili katika jamii, na kulichukulia kama kundi linalopaswa kufutwa na kubeba gharama ya usalama wa pamoja pamoja na usalama wake wa kidini na kijamii, kunahitaji msimamo wa pande zote husika katika ngazi ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa na taasisi za kibinadamu na za kutetea haki za binadamu.

Kwa mujibu wa jumuiya hiyo, dunia inapaswa kubeba wajibu wake wa kisheria na kimaadili kuhusu yanayoendelea nchini Bahrain.

Al-Wefaq ilisisitiza kwamba; suluhisho la Bahrain liko katika kuanzishwa kwa mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia uliojengwa juu ya uhuru na ushiriki wa kisiasa, kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kuhakikisha uwepo wa utofauti na wingi wa mitazamo ya kisiasa.

Aidha, Jumuiya ya Kiislamu ya Al-Wefaq ya Taifa la Bahrain, ilibainisha kwamba; tawala za kiimla na kidikteta haziwezi kuleta usalama, uthabiti, uhuru na amani kwa mataifa yao. Hasa kutokana na uzoefu na vipindi vinavyojirudia katika historia ngumu ya Bahrain, ambapo waathirika wake wamefikia makumi ya maelfu ya watu katika nyanja za maisha yao, ajira, uhuru wa kidini, mwenendo wa kijamii, utambulisho wa kimadhehebu na hata haki za msingi kabisa za kibinadamu; haki ambazo hata katika tawala kali zaidi za kidikteta duniani hazishambuliwi kwa kiwango hiki.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha