Jumapili 10 Mei 2026 - 13:41
Magharibi na Mahdawiyya (Sehemu ya Mwisho)

Hawza/ Kuonesha sura ya ukatili na ya kutisha kuhusu mwokozi wa mwisho wa zama katika Uislamu mbele ya watu wa dunia ni jukumu la pamoja linaloonekana katika kazi nyingi za Kimagharibi, zikiwemo filamu, vitabu, riwaya, michezo, muziki na hotuba. Hata hivyo juhudi hizi zote zinafanyika ilhali Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya nyingi za Qur’ani Tukufu amewapa bishara watu wote kuhusu kudhihiri kwa mwokozi huyo wa ulimwengu kwa mwanadamu, kusimamishwa kwa uadilifu na kuondolewa kwa dhulma na ufisadi; na hakika Mwenyezi Mungu kamwe havunji ahadi Yake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, mfululizo wa tafiti za Mahdawiyya zikiwa na anuani isemayo “Kuielekea Jamii Bora”, umetolewa kwa lengo la kueneza mafundisho na maarifa yanayohusiana na Imam wa Zama (ajtf), kwa ajili yenu wasomi waheshimiwa.

Katika sehemu mbili zilizopita ilielezwa kwamba; dunia ya vyombo vya habari vya Hollywood tangu mwaka 1990, kwa mabadiliko ya polepole lakini yanayoonekana wazi, ilielekeza mazingira makuu ya kazi zake kuelekea mada za uokozi na mwisho wa dunia. Miongoni mwa kazi hizi pamoja na kazi nyingine zinazofanana nazo nje ya mazingira ya Hollywood, tunakutana na mifano ambayo kwa namna maalumu na kwa malengo maalumu, imemlenga mwokozi anayetarajiwa na Waislamu, Imam Mahdi (Ajjalallahu Ta‘ala Farajahu), ambapo hapa tutataja baadhi yake tu.

Filamu ya “DUNE”

Utawala mkubwa usio na mipaka wa mkondo wa Kiyahudi-Kizayuni juu ya sinema ya Hollywood umesababisha uadui dhidi ya Uislamu na Waislamu kuwa miongoni mwa misingi yake ya kiitikadi. Katika filamu nyingi za Hollywood tunashuhudia kuharibiwa kwa sura ya Uislamu na Waislamu. Hata hivyo, kuingia moja kwa moja kwa tasnia hii ya sinema katika mada ya mwisho wa dunia na mwokozi wa Kiislamu halikuwa jambo la kawaida hapo awali, na hata kama lilikuwepo katika baadhi ya filamu, lilikuwa kwa namna ya mafumbo na ishara zisizo za moja kwa moja.

Kuoneshwa kwa filamu ya “DUNE” kulibadilisha mlingano wa sinema ya Hollywood kuhusu mada ya mwokozi wa Kiislamu na kusababisha uadui pamoja na kuharibiwa kwa sura ya mwokozi wa Kiislamu katika sinema hiyo kuingia katika hatua ya wazi na ya hadharani.

Kwa hakika, mwongozaji wa filamu hii, katika kuoanisha mada ya kubuniwa kwa fikra ya mwokozi anayesubiriwa, aliingia katika njia yenye chuki na kuifananisha na mwokozi wa Kiislamu kwa jina la “Mahdi”, ili mtazamaji wa filamu hiyo, sambamba na kufahamiana na hali ya kubuniwa na uongo ya mwokozi huyo wa mwisho, amchukulie “Mahdi” au “Lisan al-Ghayb” kuwa ndiye mfano wa mwokozi huyo wa kubuniwa.

Mchezo wa Kompyuta wa Persian Gulf Inferno (Jahannamu ya Ghuba ya Uajemi)

Katika mchezo huu wa kompyuta, mtoto anapaswa mara tu anaposikia sauti ya “Allahu Akbar” na “Ya Mahdi” aanze kupiga risasi, na jambo hili husababisha kulelewa kwa roho ya chuki dhidi ya Uislamu na mwokozi anayetarajiwa na Waislamu miongoni mwa watoto. Mambo haya yote yanafanyika kwa ajili ya kufikia malengo ya muda mrefu ya adui; kwani adui anajua vizuri kwamba ili kutawala jamii, kwanza lazima atawale fikra zao, na kipindi cha utotoni ndiyo wakati bora zaidi wa kuanza kazi hiyo.

Imam wa Kumi na Mbili katika Albamu ya Muziki wa Rock wa Kimagharibi

Ingawa kuzungumzia mada ya Mahdawiyya na mwokozi wa Kiislamu katika tovuti na vyombo vya habari vya Magharibi ni jambo la kawaida sana, lakini kuashiria mada hii katika muziki wa Kimagharibi ni jambo ambalo halijazoeleka sana.

Hata hivyo mwaka 2010 albamu ya sauti iliyopewa jina la The Godless The Godforsaken and the God Damned (Asiyemjua Mungu, Aliyeachwa na Mungu na Aliyelaniwa na Mungu) ilitolewa, ambapo moja ya sehemu zake iliitwa The Twelfth Imam (Imam wa Kumi na Mbili).

Katika muziki huu ambao umetayarishwa kwa mhimili wa Imam Mahdi(a.s), sambamba na mada kama ghaiba ya Imam, kuzungumza akiwa tumboni na ruhusa ya Mwenyezi Mungu ya kumalizika kwa ghaiba, pia zimeashiriwa dhana hasi na zenye ukatili, ambapo wamejaribu kuonesha sura ya kutisha na ya kuogopesha ya Imam huyo na 

kumtambulisha kama nguvu ya uharibifu na ya kudhibiti watu.

Maudhui makuu katika muziki huu ambayo yanarudiwa mara nyingi ni madai ya kwamba Imam anadhibiti roho za wanadamu.

Inafaa kutajwa kuwa muziki huu umetengenezwa na kundi linaloitwa BABYLON MYSTERY ORCHESTRA (Orkestra ya Siri ya Babeli), ambalo katika mitindo ya rock na metal huashiria shakhsia za kimungu na kishetani, na kujihusisha na mada za kidini, kifalsafa na za mitholojia, huku likichunguza masuala ya kina na wakati mwingine ya giza ya kibinadamu na kiteolojia.

Kuandikwa Riwaya za Kupinga Mahdawiyya

Moja ya nyanja za uadui wa kimedia wa Magharibi dhidi ya Mahdawiyya ni kuandikwa riwaya zinazopinga Mahdawiyya. Katika vitabu vya aina hii, waandishi kwa kuunda hofu au kuharibu fikra ya Mahdawiyya, huiwasilisha kama jambo hatari kwa watu duniani hususan Wakristo.

“James Parker” ambaye ni mfamasia, tangu mwaka 2006 alipendezwa na kufanya utafiti kuhusu unabii wa mwisho wa dunia katika Uislamu.

Kwa kuandika riwaya mpya, alikamilisha trilojia yake ya riwaya za kupinga Mahdawiyya:

Imam wa Kumi na Mbili; Kusimama kwa Mpinga Kristo

Imam wa Kumi na Mbili; Mateso na Dhiki Zaanza

Imam wa Kumi na Mbili; Hukumu za Mungu (kitabu cha mwisho)

Parker katika kitabu hiki pia, kwa kufuata mwenendo wa vitabu vyake vya awali, amejaribu katika dibaji ya riwaya kuwasilisha sura ya kikatili na ya kutisha ya Imam wa Kumi na Mbili kwa wasomaji.

Mwandishi huyo, kwa kuchora mapambano kati ya Imam wa Kumi na Mbili na jamii ya Wayahudi, amewatambulisha Waislamu na Imam wa Kumi na Mbili kama upande wa batili unaowakandamiza wapinzani kupitia kunyongwa hadharani pamoja na hotuba kali dhidi ya itikadi zisizo za Kiislamu.

Kwa upande mwingine, shakhsia ya Kiyahudi iitwayo Is’haq pamoja na watoto wake katika riwaya hiyo wamewasilishwa kama kundi la kidini, lenye kujitolea na alama ya kizazi kipya kinachotafuta haki na uadilifu.

Inafaa kutajwa kuwa kabla ya hapo pia “Joel Rosenberg”, kwa kuandika riwaya tatu, alifanya juhudi zote katika njia ya kuonesha uadui dhidi ya Waislamu na Imam Mahdi (a.s).

Sambamba na mifano iliyotajwa, kuna filamu, vitabu, riwaya, michezo, muziki na hotuba nyingine nyingi ambazo zote zimeungana katika lengo moja, nalo ni kuonesha sura ya ukatili na ya kutisha ya mwokozi wa mwisho wa zama wa Uislamu mbele ya watu duniani.

Hata hivyo juhudi hizi zote zinafanyika ilhali Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya nyingi za Qur’ani Tukufu ametoa bishara kwa watu wote kuhusu kudhihiri kwa mwokozi huyo wa ulimwengu wa mwanadamu, kusimamishwa kwa uadilifu na kuondolewa kwa dhulma na ufisadi; na hakika Mwenyezi Mungu kamwe havunji ahadi Yake…

Utafiti huu utaendelea…

Kazi ya Kituo Maalumu cha Mahdawiyya cha Hawza ya Qum (Kikundi cha Magharibi na Mahdawiyya) – ikifanyiwa mabadiliko kiasi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha