Kwa mujibu wa kitengo cha kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kongamano la pili la “Umoja wa Washairi” limehitimishwa kwa hotuba ya Sheikh Ibrahim Zakzaky katika mji wa Abuja.
Sheikh Zakzaky katika hafla hiyo, kupitia hotuba yake, alieleza kwa ufafanuzi nafasi ya juu ya Ahlul-Bayt wa Mtume (as) na kusisitiza kwamba; katika historia yote kumefanyika juhudi nyingi za kupunguza na kuficha fadhila na hadhi yao.
Akiashiria nafasi ya uongozi ya madrasah ya Ahlul-Bayt (as), alibainisha kuwa; kushikamana na madrasah hii ndiyo njia ya kufikia heshima na ushindi kwa umma wa Kiislamu. Ustahimilivu na mafanikio ya leo ya Iran kwa kiasi kikubwa yanatokana na kusimama imara katika njia na mafundisho ya Ahlul-Bayt (as) licha ya mashinikizo na juhudi kubwa za kupambana nayo.
Pia alilinganisha juhudi hizi na hatua zilizochukuliwa katika mwanzo wa Uislamu na Mayahudi, Wakristo na wanafiki kwa lengo la kuuangamiza Uislamu wakati wa Mtume Mtukufu (saww), na akaongeza kuwa; hata leo kuna mifano ya aina hiyo ya muungano dhidi ya mkondo wa muqawama na hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria katika sehemu nyingine ya hotuba yake alizungumzia nafasi muhimu ya mashairi na sanaa katika kufikisha ujumbe wa kidini na kijamii, na akasema kuwa mashairi ni miongoni mwa nyenzo zenye athari kubwa katika kuelimisha na kuongoza fikra za jamii.
Kwa kukumbusha nafasi ya washairi katika zama za Mtume Mtukufu (saww), aliwataka washairi na wanaharakati wa kitamaduni kutumia uwezo wa mashairi kwa ajili ya kutoa mwanga, kupambana na njama na kuzima juhudi zinazochochea tofauti za kikabila kwa lengo la kuleta mgawanyiko miongoni mwa Waislamu.
Mwishoni, Sheikh Zakzaky alisisitiza kwamba; ingawa kuna tofauti za kikabila miongoni mwa Waislamu, dini ya Uislamu iko juu ya ukabila na inapaswa kuwa mhimili wa umoja na mshikamano wa umma wa Kiislamu.
Maoni yako